Kumetajwa fadhila za sehemu nyingi Shaam ambazo hatukuzitaja kwa sababu malengo ya kitabu ilikuwa kutaja fadhila za Dameski na kuhifadhiwa kwake. Lakini hata hivyo tutahitimisha kitabu kwa kutaja angalau kwa ufupi fadhila za Yerusalemu. Hata kama Yerusalemu ni Shaam hiyo hiyo.

Wanachuoni wameandika vitabu vingi kuhusu mji huo. Miongoni mwa wanachuoni waliotunga vitabu maalum kuhusu Yerusalemu ni pamoja vilevile na Ibn-ul-Jawziy na Ibn ´Asaakir.

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema kuhusu fadhila zake:

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ

“Utakasifu ni wa ambaye amemsafirisha usiku mja Wake kutoka al-Masjid al-Haraam kwenda msikiti wa mbali ambao Tumevibariki vilivyoko pembezoni mwake.”[1]

135- al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Jaabir ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Pindi Quraysh waliponikadhibisha niliketi Hijr [karibu na Ka´bah]. Ndipo Allaah akanifunulia Yerusalemu na nikaweza kuuona mji huo na kuwaelezea jinsi unavyofanana.”

136- Muslim amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nilikuwa Hijr pindi Quraysh waliponiuliza kuhusu safari yangu ya usiku. Wakaniuliza mambo mengi kuhusu Yerusalemu ambayo sikuweza kuyasimulia. Sikuwahi kujihisi vibaya kama wakati huo. Ndipo Allaah akaninyanyulia na nikawa kuuona. Hawakuniuliza juu ya kitu isipokuwa niliwaeleza nacho.”

137- al-Bukhaariy amepokea ya kwamba Ibn ´Abbaas amesema kuhusiana na maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَمَا جَعَلْنَا الرُّؤْيَا الَّتِي أَرَيْنَاكَ إِلَّا فِتْنَةً لِّلنَّاسِ

“Hatukuijaalia ndoto ambayo tulikuonyesha isipokuwa ni mtihani kwa watu.”[2]

“Ilikuwa ni maono ya kweli ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliona usiku aliyosafirishwa kwenda Yerusalemu.”

138- Hudhayfah bin al-Yamaan (Radhiya Allaahu ´anh) amepinga ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswali Yerusalemu na kusema:

“Lau angeswali ndani yake basi ingelikuwa ni wajibu kwenu kuswali ndani yake kama ilivyokuwa wajibu kuswali msikiti Mtakatifu.”

Wanachuoni wengi wana maoni haya akiwemo Abu Bakr al-Khallaal kutoka katika wenzetu [Hanaabilah].

139- al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kusifungwe safari kwenda kokote isipokuwa katika misikiti mitatu; msikiti Mtakatifu, msikiti huu wangu na msikiti wa al-Aqswaa.”

Hadiyth hii imepokelewa na Mswahabah wengi ikiwa na maana ya kutaka kufanana. Hata hivyo katika upokezi uliyopokea at-Twabaraaniy na wengineo umetaja msikiti wa Khayf badala ya msikiti wa al-Aqswaa. Upokezi huu haukuhifadhiwa.

140- an-Nasaa´iy amepokea kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Baada ya Sulaymaan bin Daawuud (´alayhimaas-Salaam) alipomaliza kujenga Yerusalemu alimuomba Allaah mambo matatu; hukumu inayoendana na hukumu Yake, ufalme ambao mfano wake hatopewa yeyote baada yake na kwamba asiwepo yeyote atayekuja katika msikiti huu na wala hakukusudia jengine isipokuwa kuswali ndani yake isipokuwa atoke ametakasika na madhambi kama ile siku aliyozaliwa na mama yake.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Amepewa hayo mawili na natarajia kuwa atapewa hilo la tatu.”[3]

141- Imaam Ahmad amepokea kupitia kwa Junaadah bin Abiy Umayyah kutoka kwa Swahabah aliyemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akihutubia na kumtaja ad-Dajjaal:

“Atakaa ardhini asubuhi arobaini na atafika kila kona. Hatosogelea misikiti mine; msikiti Mtakatifu, msikiti wa al-Madiynah, msikiti wa at-Twuur na msikiti wa al-Aqswaa.”[4]

[1] 17:01

[2] 17:60

[3] an-Nasaa´iy (2/34), Ahmad (2/176), Ibn Hibbaan (1633), Ibn Khuzaymah (1334) na al-Haakim (1/30-31).

[4] Ahmad (5/435). al-Haytamiy amesema: ”Wanaume wake ni wanaume Swahiyh.”

  • Mhusika: Imaam ´Abdur-Rahmaan bin Rajab al-Baghdaadiy al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwaa-il-ush-Shaam, uk. 152-169
  • Imechapishwa: 10/02/2017