20. Anayemtii Mtume ataingia Peponi na anayemuasi ataingia Motoni

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

mwenye kumtii, ataingia Peponi, na yule mwenye kumuasi, ataingia Motoni.

MAELEZO

Mwenye kumtii katika yale aliyoamrisha ataingia Peponi. Yule mwenye kumuasi katika yale aliyokataza ataingia Motoni. Haya yanasapotiwa sana ndani ya Qur-aan. Amesema (Ta´ala):

مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ

“Atakayemtii Mtume, basi kwa hakika amemtii Allaah.”[1]

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا لِيُطَاعَ بِإِذْنِ اللَّـهِ

“Hatukutuma Mtume yeyote isipokuwa atiiwe kwa idhini ya Allaah.”[2]

وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا

”Mkimtii basi mtaongoka.”[3]

وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

”Mtiini Mtume ili mpate kurehemewa.”[4]

Yule mwenye kumtii ataongoka na hatimaye kuingia Peponi. Ambaye atamuasi atapotea na hatimaye kuingia Motoni. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ummah wangu wote wataingia Peponi isipokuwa yule atakayekataa.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni nani atakayekataa?” Akasema: “Yule mwenye kunitii ataingia Peponi na yule mwenye kuniasi atakuwa amekataa.”[5]

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayekataa.”

Bi maana amekataa kuingia Peponi. Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hatosikia kuhusu mimi, myahudi wala mkristo, kisha asiamini yale niliyokuja nayo isipokuwa ataingia Motoni.”[6]

Kwa hiyo yule mwenye kumtii ataingia Peponi na yule mwenye kumuasi ataingia Motoni. Hii ndio tofauti kati ya muumini na kafiri.

[1] 04:80

[2] 04:64

[3] 24:54

[4] 24:56

[5] al-Bukhaariy (7280).

[6] Muslim (153).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 47-48
  • Imechapishwa: 01/12/2020