Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

15- Mwenye kufufua bila ya uzito wowote.

MAELEZO

Haya ni miongoni mwa maajabu ya uwezo Wake ya kwamba anawafisha viumbe na kuwateketeza mpaka wakawa udongo na mchanga kiasi cha kwamba mpaka yule mtu ambaye ni mjinga anafikia kusema kwamba Yeye (´Azza wa Jall) hawezi kuwafufua. Kitendo cha kuwafufua hakina uzito wowote Kwake:

مَّا خَلْقُكُمْ وَلَا بَعْثُكُمْ إِلَّا كَنَفْسٍ وَاحِدَةٍ

“Hakukuwa kuumbwa kwenu na wala kufufuliwa kwenu isipokuwa ni kama nafsi moja tu.”[1]

وَهُوَ الَّذِي يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَهُوَ أَهْوَنُ عَلَيْهِ

“Naye ndiye aliyeanzisha uumbaji, kisha anaurudisha, nayo ni rahisi mno Kwake.”[2]

Washirikina wamekanusha kitendo cha kufufuliwa kwa sababu wameona kuwa hakiwezekani. Allaah amesimulia kwamba wamesema:

مَن يُحْيِي الْعِظَامَ وَهِيَ رَمِيمٌ قُلْ يُحْيِيهَا الَّذِي أَنشَأَهَا أَوَّلَ مَرَّةٍ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ خَلْقٍ عَلِيمٌ

“Ni nani atakayehuisha mifupa hii na hali imeshaoza na kusagika na kuwa kama vumb? Sema: “Ataihuisha Yule aliyeianzisha mara ya kwanza – Naye ni mjuzi wa kila kiumbe.”[3]

Mwanzoni Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amemuumba kiumbe kutoka katika chochote. Je, Yule ambaye amewaumba kutoka katika chochote si ana haki zaidi ya kuwafufua? Hapa ni pale ambapo tutaenda kwa kutumia akili, vinginevyo Allaah (Subhaanah) halinganishwi na viumbe. Hili ni kwa njia tu ya mfano:

وَلَهُ الْمَثَلُ الْأَعْلَىٰ

“Naye ana Sifa za juu kabisa.”[4]

Hapa anarudiwa mkanushaji. Amesema (Ta´ala):

وَضَرَبَ لَنَا مَثَلًا وَنَسِيَ خَلْقَهُ

“Akatupigia mfano, akasahau kuumbwa kwake.”[5]

Mtu amesahau kwamba kuna wakati ambapo alikuwa hayupo kabisa:

هَلْ أَتَىٰ عَلَى الْإِنسَانِ حِينٌ مِّنَ الدَّهْرِ لَمْ يَكُن شَيْئًا مَّذْكُورًا

”Je, mtu hakufikiwa na kipindi fulani katika dahari, hakuwa kitu kinachotajwa?”[6]

Amesahau kuwa Allaah amemuumba kutoka katika chochote. Kisha baadaye atawarudisha watu katika maumbile yao kama walivyokuwa hapo kabla:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَن تَقُومَ السَّمَاءُ وَالْأَرْضُ بِأَمْرِهِ ۚ ثُمَّ إِذَا دَعَاكُمْ دَعْوَةً مِّنَ الْأَرْضِ إِذَا أَنتُمْ تَخْرُجُونَ

“Miongoni mwa ishara Zake, ni kwamba mbingu na ardhi zimesimama kwa amri Yake kisha atakapokuiteni wito mmoja, tahamaki mtatoka ardhini.”[7]

وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَصَعِقَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ إِلَّا مَن شَاءَ اللَّـهُ ۖ ثُمَّ نُفِخَ فِيهِ أُخْرَىٰ فَإِذَا هُمْ قِيَامٌ يَنظُرُونَ

“Itapulizwa katika baragumu, basi watazimia wale walioko mbinguni na ardhini isipokua amtakaye Allaah. Kisha litapulizwa humo jengine, tahamaki hao wanasimama wakitazama.”[8]

Upulizwaji wa kwanza wa baragumu ni wa mshtuko na kifo. Upulizwaji wa mara ya pili wa baragumu ni wa kufufuliwa:

وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَإِذَا هُم مِّنَ الْأَجْدَاثِ إِلَىٰ رَبِّهِمْ يَنسِلُونَ قَالُوا يَا وَيْلَنَا مَن بَعَثَنَا مِن مَّرْقَدِنَا ۜ ۗ هَـٰذَا مَا وَعَدَ الرَّحْمَـٰنُ وَصَدَقَ الْمُرْسَلُونَ

“Litapulizwa baragumu, basi tahamaki wanatoka makaburini mwao wakienda mbiombio kwa Mola wao. Waseme: “Ole wetu! Nani ametufufua katika malazo yetu?” [Wataambiwa]: “Haya ndio aliyoahidi Mwingi wa rehema na Mitume wakasema kweli.”[9]

Allaah ni muweza wa kila jambo. Hapa wanajibiwa wale makafiri ambao wamemfanya Allaah kuwa si muweza wa kuwahuisha wafu na kuwarudisha kama walivyokuwa. Amesema (Ta´ala):

أَيَحْسَبُ الْإِنسَانُ أَلَّن نَّجْمَعَ عِظَامَهُ بَلَىٰ قَادِرِينَ عَلَىٰ أَن نُّسَوِّيَ بَنَانَهُ

“Je, mtu anadhani kwamba hatutoikusanya mifupa yake? Ndio, tuna uwezo wa  kusawazisha sawasawa ncha za vidole vyake.”[10]

Namna hii ndivo ulivyo uwezo wa Allaah, utashi na matakwa Yake. Hakuna chochote kinachomshinda. Lakini kwa masikitiko makubwa wako ambao wanamlinganisha Allaah na viumbe Wake ambapo hatimaye wanaona kuwa jambo la kufufuliwa haliwezekani. Kwa sababu kufufuliwa kwa mtazamo wao wanaona kuwa ni jambo lisilowezekana, lakini hawatazami uwezo wa Allaah. Hawakumuadhimisha Allaah ipasavyo, jambo ambalo linafahamisha ujinga wao juu ya Allaah (´Azza wa Jall).

[1][1] 31:28

[2] 30:27

[3] 36:78

[4] 30:27

[5] 36:78

[6] 76:01

[7] 30:25

[8] 39:68

[9] 36:51-52

[10] 75:03-04

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 40-42
  • Imechapishwa: 16/09/2019