20. Allaah amezungumza kwa Qur-aan

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Qur-aan ni maneno ya Allaah na hayakuumbwa.”

Allaah amezungumza kwayo. Vitabu vilivyoteremshwa ni katika maneno ya Allaah ambavyo ameviteremsha kwa waja Wake. Alimzungumzisha Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) maneno ya kikweli. Alimzungumzisha Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)  usiku wa Israa´. Ataita siku ya Qiyaamah:

“Wako wapi washirika Wangu?”

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

وَإِذْ نَادَىٰ رَبُّكَ مُوسَىٰ أَنِ ائْتِ الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ

“[Kumbuka] wakati Mola wako alipomwita Muusa kwamba:  “Nenda kwa watu madhalimu.”[1]

Wito hauwi isipokuwa kwa herufi na sauti yenye kulingana na Allaah. Havilingani na sauti, herufi wala maneno ya viumbe. Allaah anazungumza na maneno Yake ni sifa ya ukamilifu. Vitu visivyokuwa na uhai havizungumzi. Wanyama, ambao wako duni ya mwanaadamu anayezungumza, wao pia hawazungumzi. Allaah amemtukuza na kumkamilisha mwanaadamu. Ukamilifu mkubwa kwa mwanaadamu ni maneno ambayo yanamtofautisha na viumbe wengine. Allaah amewatunuku wanaadamu, Malaika na majini kwa uwezo wa kuzungumza. Maneno ni sifa ya ukamilifu. Allaah ni mkamilifu na anampa ukamilifu Wake yule amtakaye. Kama tulivyosema maneno ni sifa ya ukamilifu. Ujuzi pia ni sifa ya ukamilifu. Yule mwenye kukanusha maneno kwa Allaah, ujuzi na uwezo amemuumbua ubaya wa kumuumbua. Wakati kafiri mmoja wa Quraysh aliposema:

إِنْ هَـٰذَا إِلَّا قَوْلُ الْبَشَرِ

“… hii si chochote isipokuwa ni kauli ya binaadamu!”[2]

Allaah alisema:

سَأُصْلِيهِ سَقَرَ

“Nitamuingiza kumuunguza kwenye moto mkali mno.”[3]

Maneno ya mwanaadamu yameumbwa. Allaah alimtisha kwa matishio haya makali. Kuituhumu Qur-aan kuwa ni uchawi na ni maneno ya mwanaadamu ni kuitukana Qur-aan. Huku ni kuiumbua na kuitukana Qur-aan hii ambayo ni maneno ya Allaah. Ameiteremsha (Subhaanahu wa Ta´ala) ili imwongoze mwanaadamu. Haikuumbwa.

Mu´tazilah, Jahmiyyah, Baatwiniyyah, Raafidhwah, Khawaarij na mapote mengine yote potevu wana madhehebu mbalimbali lakini wote ni wenye kuafikiana kuwa Allaah hazungumzi. Hata Ashaa´irah wameathiriwa na Mu´tazilah. Ashaa´irah wa kale walikuwa wakisema kuwa maneno ni sifa iliyosimama kivyake katika dhati ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), ya kwamba Qur-aan sio maneno ya Allaah bali ni simulizi/hikaaya ya maneno ya Allaah. Wakimaanisha kuwa maneno Yake ni sifa iliyosimama kwenye dhati Yake na haina herufi wala sauti. Pamoja na hivyo hawaonelei kuwa alizungumza na hawaonelei vilevile kuwa Qur-aan ni maneno Yake. Ama kuhusiana na Ashaa´irah waliokuja nyuma, wakisema waziwazi kuwa Qur-aan imeumbwa.

Qur-aan ni maneno ya Allaah na hayakuumbwa. Hakuna kitu katika maneno ya Allaah kilichoumbwa. Watu hawa mwanzoni walikuwa wakisema kuwa Allaah aliumba maneno Yake pasi na sehemu. Wanasema “maneno ya Allaah” kama inavyosemwa “ngamia wa Allaah” na “nyumba ya Allaah”, bi maana kiumbe anayetokamana na Muumba. Haya ni katika utata na uongo wao.

[1] 26:10

[2] 74:25

[3] 74:26

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 384-385
  • Imechapishwa: 07/08/2017