2. Sura ya kwanza: Hukumu ya swawm


Kufunga Ramadhaan ni faradhi iliyothibiti katika Qur-aan, Sunnah na maafikiano. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ ۚ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۚ وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ ۖ فَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ ۚ وَأَن تَصُومُوا خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۗ يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

“Enyi mlioamini! Mmeandikiwa [fardhi ya] swawm kama ilivyoandikwa kwa walio kabla yenu mpate kuwa na taqwa. [Kufunga swawm kwenyewe ni] siku za idadi maalum. Basi atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu, au yuko safarini [akafunga baadhi ya siku], basi [akamilishe] idadi [ya siku anazotakiwa kufunga] katika siku nyinginezo. Na ni juu ya wale wanaoiweza [kufunga swawm] lakini kwa tabu watoe fidia kulisha masikini. Na atakayejitolea kwa jema lolote lile basi ni bora kwake, na mkifunga swawm ni bora kwenu – mkiwa mnajua [ni ubora kiasi gani kwa nyinyi kufanya hivo]! Mwezi wa Ramadhaan ambao [kumeanzwa] kuteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo [la haki na ubatilifu]. Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi [mpya] na afunge  swawm. Na atakayekuwa mgonjwa au safarini basi [atimize] idadi katika siku nyinginezo. Allaah Anakutakieni mepesi na wala Hakutakieni magumu. [Fungeni siku mlizowekewa] ili mkamilishe idadi na ili mumkabiri Allaah kwa kuwa Amekuongozeni na mpate kushukuru.” (02:183-185)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uilsamu umejengwa juu ya [mambo] matano: Kushuhudia kuwa hapana mola mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume Wake, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kwenda kuhiji katika nyumba takatifu ya Allaah na kufunga Ramadhaan.”[1]

Katika upokezi wa Muslim imekuja:

“… kufunga Ramadhaan na kwenda kuhiji katika nyumba takatifu ya Allaah.”[2]

Waislamu wamekubaliana juu ya ufaradhi wa kufunga Ramadhaan. Hivyo yule mwenye kupinga faradhi hii ni kafiri aliyeritadi. Anatakiwa kuambiwa atubie. Ima atubie na kukiri ufaradhi wake au uawe hali ya kuwa ni kafiri.

Kufunga Ramadhaan ilikuwa faradhi miaka miwili baada ya kuhajiri. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifunga Ramadhaan mara tisa. Kila muislamu ambaye kishabeleghe na ni mwenye akili ni lazima kwake kufunga. Sio wajibu kwa kafiri kufunga. Na lau atafunga swawm yake haikubaliwi mpaka asilimu kwanza.

Mtoto mdogo sio wajibu kwake kufunga mpaka abaleghe. Alama zifuatazo ni zenye kuashiria kubaleghe:

1- Miaka kumi na tano.

2- Nywele sehemu ya siri.

3- Kumwaga.

4- Hedhi.

Pindi mtoto anapopata moja katika mambo haya basi amebaleghe. Lakini hata mtoto mdogo anatakiwa kuamrishwa kufunga maadamu anaweza kufanya hivo na hadhuriki kwa kufunga. Lengo la swawm ya mtoto ni kwa ajili ya kumzoweza nayo.

Mtu ambaye amepoteza akili yake kwa sababu ya wendawazimu, ubongo wake kubadilika au mfano wa hayo sio lazima kwake kufunga. Mtu ambaye amekuwa mzee sana kiasi cha kwamba amepatwa na wazimu na hawezi kuyapambanua mambo sio lazima kwake kufunga wala kulisha.

[1] al-Bukhaariy (8) na Muslim (16).

[2] Muslim (16).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Utaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fusuwl fiys-Swiyaam wat-Taraawiyh waz-Zakaah, uk. 3-4
  • Imechapishwa: 03/06/2017