[2] Usiku bora ni usiku wa makadirio kujengea maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule mwenye kusimama usiku wenye cheo kwa imani na kwa matarajio kisha akawafikishwa nao, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[1]

[3] Maoni yenye nguvu yanasema kuwa ni usiku wa tarehe ishirini na saba Ramadhaan. Hadiyth nyingi zinasema hivo. Moja wapo ni Hadiyth ya Zirr bin Hubaysh aliyesema:

“Nimesikia Ubayy bin Ka´b akiambiwa: “´Abdullaah bin Mas´uud anasema kwamba yule mwenye kuswali mwaka mzima basi ataupata usiku wa makadirio.” Ndipo Ubayy (Radhiya Allaahu ´anh) akasema: “Allaah amuwie radhi kwani hakupenda watu wabweteke. Ninaapa kwa yule ambaye hakuna mungu mwengine wa haki asiyekuwa Yeye ya kwamba ni katika Ramadhaan. Ninaapa kwa Allaah pia kuwa najua ni usiku gani! Usiku ambao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametuamrisha tuswali ni usiku wa tarehe ishirini na saba. Alama yake ni jua kuchomoza asubuhi leupe likiwa halichomi.””

Katika upokezi mwingine amemnasibishia hayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[2].

[1] al-Bukhaariy, Muslim na wengineo kutoka kwa Abu Hurayrah na Ahmad (05/318) kutoka kwa ´Ubaadah bin as-Swaamit. Nyongeza ni ya kwake na vilevile Muslim kutoka kwa Abu Hurayrah. Tanbihi! Katika chapa iliyotangulia mwishoni mwa Hadiyth nilitaja nyongeza nyingine yenye kusema: “… na yatayokuja huko mbele.” Nilikuwa nimemtegemea al-Mundhiriy na al-´Asqalaaniy waliosema kuwa ni Swahiyh. Kisha Allaah (Ta´ala) akanisahilishia kupeleleza njia nyenginezo za Hadiyth na mapokezi kutoka kwa Abu Hurayrah na ´Ubaadah kwa njia ambayo sijawahi kuona imefanywa na yeyote. Nikapata kubainikiwa kuwa ni nyongeza hiyo ni Shaadhdh kutoka kwa Abu Hurayrah Munkar kutoka kwa ´Ubaadah. Yule aliyeifanya hii kuwa nzuri na ile nyingine kuwa Swahiyh, amefanya hivo kwa kudanganyika na udhahiri wa mlolongo wa wapokezi pasi na kufuatilia njia nyenginezo za mapokezi. Nimeiweka katika “Silsilah al-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah” (5083). Sikutaja nyongeza hii katika Hadiyth ya Abu Hurayrah kwa sababu nimeitaja katika “Swahiyh at-Targhiyb wat-Tarhiyb” (982). Hata hivyo sikutaja Hadiyth ya ´Ubaadah pamoja nayo tofauti na asili yake “at-Targhiyb” – na Allaah (Ta´ala) ndiye Mwenye kuwafikisha.

[2] Muslim na wengineo. Imetajwa katika “Swahiyh Abiy Daawuud” (1247).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qiyaam Ramadhwaan, uk. 18-19
  • Imechapishwa: 07/05/2019