2. Kushikamana na mfumo wa Maswahabah


Imaam al-Laalakaa´iy (Rahimahu Allaah) amesema:

‘Aliy bin Muhammad bin ‘Abdillaah as-Sukkariy ametueleza: ‘Uthmaan bin Ahmad as-Samaak ametueleza: Abu Muhammad al-Hasan bin ‘Abdil-Wahhaab bin Abiyl-´Anbar ametueleza kupitia kisomo Rabiy ‘al-Awwal 293: Abu Ja’far Muhammad bin Sulaymaan al-Manqariy al-Baswriy ametueleza Tinnis: ‘Abduws bin Maalik al-‘Attwaar ametueleza: Nilimsikia Abu ‘Abdillaah Ahmad bin Muhammad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) akisema:

“Tunaamini kuwa misingi ya Sunnah ni kushikamana bara bara na mfumo wa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuwaiga, kuepuka na Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu, kuepuka mivutano, kuepuka kukaa na Ahl-ul-Ahwaa´ na kuepuka kubadilishana maneno, mijadala na magomvi katika dini.”

MAELEZO

Hapa al-Laalakaa´iy ametaja mnyororo wake kwa Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah). Mnyororo huu unakutana na mnyororo mwingine. al-Laalakaa´iy ameutaja katika “Sharh Usuwl I´tiqaad Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah” kama ambavyo Abu Ya´laaa vilevile ameutaja katika “Twabaqaat-ul-Hanaabilah”. Nuskha hizi mbili zilizo na minyororo miwili yenye kutofautiana inapeana nguvu na kuthibitisha kuwa kijibu hichi kimeandikwa kweli na Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah), Imaam wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Kadhalika Shaykh al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) alipata miswada katika maktabah Dhwaahiriyyah na akaiandika kwa hati yake ya mkono. Nafikiri kuwa aliiandika kupitia mnyororo mwingine[1] na Allaah ndiye anajua zaidi. Mtu arejee kwenye minyororo na kuilinganisha. Tutafanya hivo – Allaah akitaka – tukipata fursa.

Ametaja mnyororo kufika mpaka kwa Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ambaye amesema:

“Tunaamini kuwa misingi ya Sunnah ni kushikamana bara bara na mfumo wa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)…”

Mfumo wa Maswahabaha wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio wenye kukata kesi kwa wale walioshikamana na haki na kushikamana na msingi huu. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake watukufu na makhaliyfah waongofu walikuwa wakifuata uongofu. ´Aqiydah yao, ´ibaadah zao, matamgamano yao na mambo yao mengine yote yalikuwa ni yenye kuafikiana na Qur-aan na Sunnah. Khaswa inapokuja katika ´Aqiydah. Ahmad (Rahimahu Allaah) anaashiria msingi na kanuni hii kubwa ambayo inatakikana kutekelezwa katika Uislamu wote na khaswa ´Aqiydah. Amesema:

“Tunaamini kuwa misingi ya Sunnah ni kushikamana bara bara na mfumo wa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)…”

Ahl-ul-Bid´ah hawafanyi hivi. Hakika wao wanachofuata ni matamanio yao na fikira zao chafu, lugha na vigezo vingine vichafu. Imaam Ahmad na waliomtangulia katika Maswahabah, waliokuja baada ya Maswahabah na maimamu wa Uislamu ni wenye kushikamana na Qur-aan na Sunnah na khaswa inapokuja katika ´Aqiydah. Wao – Allaah akitaka – hawakuacha mpaka huu. Hapa ndipo kuna njia iliyonyooka. Amesema:

“… na kuwaiga…”

Bi maana kuwaiga Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wao ndio kiigizo na mfano mwema wa kuigwa. Akiashiria Hadiyth:

“Hivyo basi jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu. Ziumeni kwa magego yenu. Tahadharini na mambo mepya.”[2]

Vilevile anaashiria Hadiyth juu ya kundi lililookolewa pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposema:

“Na Ummah wangu utagawanyika katika makundi sabini na tatu. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja.” Wakasema: “Ni wepi, ewe Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ni wale wenye kufuata yale ninayofuata mimi na Maswahabah zangu hii leo.”[3]

Amesema katika Hadiyth nyingine:

“Nimekuacheni kwenye uwazi; usiku wake ni kama mchana wake. Hatopinda nao isipokuwa tu mwangamivu.”[4]

Maswahabah walishikamana nayo. Hatuwezi kupata – Allaah akitka – yeyote katika wao aliyekuwa ameangamia. Watu walipotea mwishoni baada ya zama za mwisho za Maswahabah na katika zama za waliokuja baada ya Maswahabah. Baada ya hapo ndio Bid´ah ikaenea. Khawaarij na Raafidhwah waliopindukia wakazuka mwishoni wa uongozi wa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh). Akamtuma ´Abdullaah bin ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) akajadiliane nao. Halafu wakaanza kuwanyanyuliwa waislamu silaha ambapo ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhyu) akawaua, kama alivyoamrisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Maswahabah wote katika zama zake wakakubaliana naye na hakuna yeyote aliyempinga.

Kikusudiwacho ni kwamba uokovu unapatikana kwa kushikamana na Maswahabah. Wao ndio safina ya uokovu. Kwa sababu wameshuhudia kuteremka kwa Wahyi na wakajifunza kuielewa na kuitendea kazi Qur-aan na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wao ndio kiigizo. Ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ni wale wenye kufuata yale ninayofuata mimi na Maswahabah zangu hii leo.”

na:

“Hivyo basi jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu. Ziumeni kwa magego yenu.”

[1] Mnyororo uliohakikishwa na Shaykh al-Albaaniy uko ifuatavyo:

Shaykh na Imaam Abul-Mudhaffar ´Abdul-Malik bin ‘Aliy bin Muhammad al-Hamdaaniy ametueleza: Shaykh Abu ‘Abdillaah Yahya bin Abiyl-Hasan al-Bannaa ametueleza: Baba yangu Abu ‘ Aliy al-Hasan bin Ahmad bin al-Bannaa ametueleza: Abul-Husayn ‘Aliy bin Muhammad bin ‘Abdillaah bin Bishraan al-Mu’addal ametueleza: ‘Uthmaan bin Ahmad bin as-Samaak ametueleza: Abu Muhammad al-Hasan bin ‘Abdil-Wahhaab bin Abiyl-‘Anbar ametueleza kupitia kisomo Rabiy’ al-Awwal 293: Abu Ja’far Muhammad bin Sulaymaan al-Manqariy al-Baswriy ametueleza Tinnis: ‘Abduws bin Maalik al-‘Attwaar amenieleza: Nilimsikia Abu Ahmad ‘Abdillaah bin Muhammad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) akisema…

[2] at-Tirmidhiy (2676), Abu Daawuud (4607) na Ibn Maajah (42-43). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy.

[3] at-Tirmidhiy (2641). Ni nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy.

[4] Ibn Maajah (43). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 363-365
  • Imechapishwa: 18/03/2017