2. Fadhila za Tawhiyd na madhambi yanayosamehewa kwayo

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُم مُّهْتَدُونَ

”Wale ambao wameamini na hawakuchanganya imani zao na dhulma. Hao ndio watakaopata amani nao ndio walioongoka.”(al-An´aam 06 : 82)

2- ´Ubaadah bin as-Swaamit (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kushuhudia ya kwamba hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa ni mmoja asiyekuwa na mshirika, na kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake na kuwa ´Iysa ni mja, Mtume Wake na ni Neno Lake Alilompelekea Maryam na roho iliyotoka Kwake na kwamba Pepo ni kweli na Moto ni kweli, basi  Allaah Atamuingiza Peponi pasi na kujali atachofanya.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

3- al-Bukhaariy na Muslim wamepokea wote wawili Hadiyth kupitia kwa ´Utbaan (Radhiya Allaahu ´anh):

“Hakika Allaah kamharamishia Moto yule mwenye kusema hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah akikusudia kwa kufanya hivo Uso wa Allaah.”[2]

4- Abu Sa´iyd al-Kudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Muusa alisema: “Ee Mola Wangu! Nifunze kitu ambacho nitakukumbuka kwacho na kukuomba kwacho.” Akamwambia: “Ee Muusa! Sema: “Hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah.” Akasema: “Ee Mola! Waja Wako wote wanasema hivi.” Akasema: “Ee Muusa! Lau mbingu saba na vyote vilivyomo ndani yake mbali na Mimi na ardhi saba na vyote vilivyomo ndani yake vitawekwa kwenye kitanga kimoja cha mzani na “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” ikawekwa kwenye kitanga kingine, basi “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” ingevizidi uzito.”

Ameipokea Ibn Hibbaan na al-Haakim ambaye ameisahihisha.

5- at-Tirmidhiy ameipokea na kuifanya kuwa ni nzuri kutoka kwa Anas (Radhiya Allahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Allaah (Ta´ala) amesema: “Ee mwanaadamu! Lau utanijia kwa madhambi yaliyojaa ardhi kisha ukakutana na Mimi pasi na kunishirikisha na chochote, basi ningelikujia na kiasi hicho hicho cha msamaha.”

MAELEZO

Mwandishi anachotaka ni kuonesha fadhila za Tawhiyd na kuwa hakuna kitendo kinachofuta madhambi kama Tawhiyd. Kwa sababu Tawhiyd ndio asli na ndio msingi wa matendo. Matendo hayasihi bila ya Tawhiyd. Ameitaja ili muumini aweze kuitambua na kuipupia na kuitamani.

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُم مُّهْتَدُونَ

”Wale ambao wameamini na hawakuchanganya imani zao na dhulma. Hao ndio watakaopata amani nao ndio walioongoka.”(al-An´aam 06 : 82)

Wameamini ina maana ya kwamba wamempwekesha Allaah na kumtakasia Yeye ´ibaadah na kuwamini kuwa Yeye ndiye mungu wao wa haki. Imani maana yake Tawhiyd. Hawakuchanganya imani zao na shirki. Bali wanamuabudu tu Yeye (Subhaanah) peke yake. Hao ndio watakaopata amani na uongofu mkamilifu kwa sababu imano zao zilisalimika na sampuli zote za shirki na yote yaliyo chini yake katika maasi na kuwadhulumu waja.

Pindi ilipoteremshwa Aayah hii Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) iliwatatiza. Wakaenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumuuliza ni nani hajapatae kuitendea nafsi yake dhuluma. Walidhani kuwa Allaah anamaanisha madhambi. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Je, hamkusikia maneno ya mja mwema alivyosema:

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

“Hakika shirki ni dhulma kubwa mno!”[3] (Luqmaan 31 : 13)

Makusudio ya dhuluma hapa ni shirki. Hili ni tofauti na mshirikina. Hatopata amani yoyote. Ataingia Motoni. Muumini mwenye kusalimika na shirki kubwa na ndogo na kuwadhulumu waja basi huyo ana uongofu na amani kamilifu duniani na Aakhirah. Yule mwenye kusalimika na shirki kubwa na asisalimike na shirki ndogo na akatumbukia katika baadhi ya maasi hapati uongofu na amani kamilifu. Kuna khatari kwa mtu huyo akaingia Motoni kutokana na madhambi aliyokufa juu yake. Pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoifasiri Aayah alibainisha ya kwamba uongofu na amani kamilifu havipatikani isipokuwa kwa kuepuka shirki kubwa. Hata hivyo kuna dalili zingine zenye kuonesha kuwa uongofu na amani kamilifu havipatikani isipokuwa kwa kuepuka maasi, kuwadhulumu waja na aina nyinginezo za shirki na ndogo.

2- ´Ubaadah bin as-Swaamit (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kushuhudia ya kwamba hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa ni mmoja asiyekuwa na mshirika, na kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake na kuwa ´Iysa ni mja, Mtume Wake na ni Neno Lake Alilompelekea Maryam na roho iliyotoka Kwake na kwamba Pepo ni kweli na Moto ni kweli, basi  Allaah Atamuingiza Peponi pasi na kujali atachofanya.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Roho kutoka Kwake ina maana ya kwamba ni roho iliyoumbwa na Allaah.

Mwenye kushuhudia haya kikweli basi Allaah atamuingiza Peponi. Hadiyth hii ni miongoni mwa Hadiyth ambazo hazikufungamanishwa [Mutlaq] zenye kuonesha fadhila za Tawhiyd. Lakini pamoja na hivyo kuna dalili zingine zenye kuonesha kuwa hukumu hii ambayo haikufungamanishwa imefungamanishwa na kule kutekeleza haki ya Shahaadah. Shahaadah yenye maazimio ambayo ndani yake kuna kumtakasia ´ibaadah Allaah peke yake kwa ukweli, unyenyekeaji, mapenzi, kukubali na kwa nia safi kwa kumfuata na kumtii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mwenye kushuhudia Shahaadah hii na akaichafua na maasi na madhambi au akaitamka kwa ulimi tu na huku anashirikisha kwa moyo au matendo yake, kama wanafiki, huyu Shahaadah haitomfaa kitu. Shahaadah ni lazima itamkwe kwa maazimio na kutekeleza maamrisho na kujiepusha na makatazo. Kadhalika ni lazima Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) afuatwe. Vingenvyo Shahaadah itakuwa ni yenye kuchafuliwa na haitoweza kumwingiza mwenye nayo Peponi isipokuwa kwa kutaka Kwake Allaah.

3- al-Bukhaariy na Muslim wamepokea wote wawili Hadiyth kupitia kwa ´Utbaan (Radhiya Allaahu ´anh):

“Hakika Allaah kamharamishia Moto yule mwenye kusema hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah akikusudia kwa kufanya hivo Uso wa Allaah.”

Anayetamka Shahaadah kwa ukweli na akafa katika hali hiyo Allaah atamwingiza Peponi. Ama kuhusu yule mwenye kufanya madhambi bila ya kutubu hilo anaachiwa Allaah kama atamsamehe au kumuadhibu.

Mwenye kutamka Shahaadah kwa nia safi na kwa ukweli habaki kwenye madhambi. Imani na Ikhlaasw yake kamilifu inamzuia na kuendelea kwa madhambi. Huyu ataingia Peponi pamoja na wale wa kwanza wataoingia. Dalili yenye kuonesha kuwa mwenye kufa hali ya kuwa ni mtendaji madhambi anaingia katika matakwa ya Allaah ni Kauli Yake (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa Amtakae.” (04:48)

 Kuna Hadiyth zenye kuonesha kuwa mtenda madhambi kuna khatari juu yake akaadhibiwa na kutumbukia Motoni. Kisha watatolewa kutokana na uombezi wa Mitume na wengine. Watu hawa Tawhiyd yao ilikuwa dhaifu. Waliichafua kwa madhambi. Huu ndio mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na uelewa sahihi ambao Ahl-ul-Bid´ah kama Khawaarij, Mu´tazilah na Murji-ah wameuacha. Pamoja na hivyo yule mwenye kukufuru Shahaadah haitomfaa kitu hata kama ataitamka.

4- Abu Sa´iyd al-Kudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Muusa alisema: “Ee Mola Wangu! Nifunze kitu ambacho nitakukumbuka kwacho na kukuomba kwacho.” Akamwambia: “Ee Muusa! Sema: “Hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah.” Akasema: “Ee Mola! Waja Wako wote wanasema hivi.” Akasema: “Ee Muusa! Lau mbingu saba na vyote vilivyomo ndani yake mbali na Mimi na ardhi saba na vyote vilivyomo ndani yake vitawekwa kwenye kitanga kimoja cha mzani na “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” ikawekwa kwenye kitanga kingine, basi “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” ingevizidi uzito.”

Ameipokea Ibn Hibbaan na al-Haakim ambaye ameisahihisha.

Hadiyth hii inaonesha fadhila za neno hili na kuwa ni Dhikr na du´aa yote mawili kutokana na kwamba Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema:

“Nifunze kitu ambacho nitakukumbuka kwacho na kukuomba kwacho.”

Mtu anamdhukuru Allaah kwa neno hili na kushuhudia kupwekeka Kwake. Neno hili vilevile ni du´aa kwa sababu yule mwenye kulitamka anatarajia thawabu. Kama ilivyo kwa du´aa nyenginezo kama “Subhaan Allaah”, “al-Hamdu lillaah” na “Laa hawlaa wa laa quwwata illa billaah”. Hadiyth inaonesha vilevile nafasi ya neno hili. Neno hili ni Dhikr na du´aa. Hadiyth inaonesha pia kuwa fadhila Zake zinaweza kuwa hata hazijulikana kwa baadhi ya Mitume. Inaonesha pia ukubwa wa neno hili kwa kumuhakikishia ´ibaadah Allaah peke yake, kumthibitishia nayo na kumkanushia nayo mwingine yeyote. Neno hili maana yake ni hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Bi maana kubatilisha waungu wengine wote.

Allaah amesema “Lau mbingu saba na vyote vilivyomo ndani yake mbali na Mimi… “. Allaah (Subhanaah) Amejiondoa kwa kuwa Yeye ni Mkubwa. Hakika Yeye (Subhaanah) Yuko juu ya mbingu. Ameumba mbingu na ardhi. Yeye ndiye mwenye kuzizuia na kuzisimamisha, ´Arshi na Kursiy. Yeye ndiye amevisimamisha viumbe Hivi. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَن تَقُومَ السَّمَاءُ وَالْأَرْضُ بِأَمْرِهِ

“Na katika alama Zake ni kwamba mbingu na ardhi zimesimama kwa amri Yake.” (30:25)

إِنَّ اللَّـهَ يُمْسِكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ أَن تَزُولَا

“Hakika Allaah Anazuia mbingu na ardhi zisitoweke.” (35:31)

Lau vyote vingeliwekwa kwenye kitanga cha mzani na “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” ikawekwa kwenye kitanga kingine, basi “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” ingevizidi uzito. Kwa maana ya kwamba maana ingelikuwa na uzito zaidi na sio vitu hivi. Kutokamana na maana na uhakika neno la Tawhiyd ni kubwa, la kweli na muhimu zaidi. Ndio maana lina uzito zaidi kuliko vitu vyote. Kama jinsi neno hili lina uzito zaidi kuliko viumbe basi linafanya vilevile kwa yule mwenye kulitamka kushinda madhambi yake yote.

5- at-Tirmidhiy ameipokea na kuifanya kuwa ni nzuri kutoka kwa Anas (Radhiya Allahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Allaah (Ta´ala) amesema: “Ee mwanaadamu! Lau utanijia kwa madhambi yaliyojaa ardhi kisha ukakutana na Mimi pasi na kunishirikisha na chochote, basi ningelikujia na kiasi hicho hicho cha msamaha.”

Hadiyth inaonesha kuwa madhambi yote yanashindwa na neno la Tawhiyd lenye kuhakikishwa kama jinsi neno hilo lilivyo na uzito zaidi kuliko viumbe vingine vyote.Wanachuoni wameifasiri Hadiyth hii kwa njia mbili:

Ya kwanza: Inahusu yule ambaye ataitamka kwa ukweli na kwa nia safi pasi na kuendelea juu ya maasi. Huyu analitendea kazi neno hili mpaka anatekeleza mambo yote ya wajibu, kuacha mambo yote yaliyokatazwa na kushikamana na Shari´ah ya Allaah katika mambo yote.

Ya pili: Inahusu yule mwenye kuitamka na akamjia Allaah hali ya kuwa ameshatubu kwa madhambi yake na kujivua nayo. Madhambi yote yanaondoka kwa neno hili.

Hadiyth hii ni lazima ifahamike namna hii. Kuna Aayah na Hadiyth zenye kuonesha kuwa watenda madhambi kuna khatari juu yao wakaadhibiwa na kutumbukizwa Motoni. Maandiko haya hayagongani. Ndio maana ni wajibu Hadiyth hizi zikafasiriwa namna hii ili kuepuka tofauti na mgongano.

Kuna wajinga ambao wameshikamana na maandiko haya ambayo hayakufungamanishwa na kufikiri ya kwamba inatosha kwa mtu kutamka Shahaadah hata kama ataacha mambo ya wajibu na kufanya maasi. Hili linakwenda kinyume na maafikiano ya Salaf wa Ummah huu yenye kusema kuwa ni lazima kufanya mambo ya wajibu, kujiepusha na mambo ya haramu na kusimama katika mipaka ya Allaah. Mwenye kuacha mambo ya wajibu na akafanya mambo yaliyokatazwa kuna khatari akaadhibiwa na Allaah (Ta´ala). Katika hali hii haijalishi kitu hata kama atatamka na kuyakinisha neno hili. Ikiwa atafanya kitu kinachotengua Uislamu wake anakuwa kafiri aliyeritadi. Hapa hatonufaika na neno hili. Kwa msemo mwingine ni lazima kuhakikisha yale yenye kulazimishwa na neno hili. Vinginevyo mtu yuko katika hali ya khatari ikiwa hakutubia.

[1] al-Bukhaariy (3435) na Muslim (28).

[2] al-Bukhaariy (425) na Muslim (33).

[3] al-Bukhaariy (4776) na Muslim (124).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 15-19
  • Imechapishwa: 21/10/2017