Mlango wa tatu: Mambo yanayopendekezwa ya swawm na machukizo yake. Ndani yake kuna masuala mawili:

Suala la kwanza: Mapendekezo ya funga

Imependekezwa kwa mfungaji kuchunga mambo yafuatayo:

1- Daku. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kuleni daku. Kwani hakika katika daku kuna baraka.”[1]

Daku inapatikana kwa chakula kingi au kidogo ijapo kwa glasi ya maji. Wakati wa daku ni kuanzia nusu ya usku mpaka pale inapochomoza alfajiri.

2- Kuchelewesha daku. Zayd bin Thaabit (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Tulikula daku pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kisha tukasimama kuswali.” Nikasema: “Kulikuwa muda kiasi gani baina yake?” Akasema: “Aayah khamsini.”[2]

3- Kuharakisha kukata swawm. Inapendekezwa kwa mfungaji kuharakisha kukata swawm pale tu ambapo atakuwa na uhakika kwamba jua limekwishazama. Sahl bin Sa´d (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu hawatoacha kuwa juu ya kheri muda wa kuwa wanaharakisha kukata swawm.”[3]

4- Kukata swawm kwa tende tosa, asipopata basi tende za kawaida, asipopata basi kwa glasi ya maji. Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifuturu kwa tende tosa kabla ya kuswali. Isipokuwa tende tosa basi tende za kawaida. Isipokuwa tende za kawaida basi glasi ya maji.”[4]

Asipopata kitu basi anuie kufungua kwa moyo wake na itamtosha kufanya hivo.

5- Kuomba du´aa wakati wa kukata swawm na kipindi cha swawm. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Watu aina tatu hayarudishwi nyuma maombi yao; mfungaji mpaka akate swawm, kiongozi mwadilifu na mdhulumiwa.”[5]

6- Kukithirisha kutoa swadaqah, kusoma Qur-aan, kuwafuturisha wafungaji na matendo mema mengine. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza:

“Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ni mkarimu zaidi wa watu. Ramadhaan alikuwa mkarimu zaidi wakati anapokutana na Jibriyl. Jibriyl alikuwa akikutana naye katika kila usiku wa Ramadhaan ambapo anamfunza Qur-aan. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati anapokutana na Jibriyl basi anakuwa ni mkarimu zaidi katika mambo ya kheri kuliko upepo ulioagizwa.”[6]

7- Kujitahidi swalah ya usiku na khaswa katika zile siku kumi za Ramadhaan. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza:

“Zinapoingia zile kumi basi anafunga vizuri kikoi chake, anauhuisha usiku wake na anawaamsha familia yake.”[7]

Pia kutokana na kuenea kwa maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule mwenye kufunga Ramadhaan kwa imani na kwa matarajio basi atasamehewa dhambi zake zilizotangulia.”[8]

8- Kufanya ´Umrah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kufanya ´Umrah katika Ramadhaan ni sawa na hijjah.”[9]

9- Kusema “Mimi nimefunga” kumwambia yule mwenye kumtukana. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Itapokuwa ni siku ya funga ya mmoja wenu, basi asizungumze maneno machafu wala asipige kelele. Mtu akimtukana au akamgombeza, basi amwambie: “Mimi ni mtu nimefunga.”[10]

[1] al-Bukhaariy (1923) na Muslim (1095).

[2] al-Bukhaariy (575) na Muslim (1097).

[3]al-Bukhaariy (1957) na Muslim (1098).

[4] Abu Daawuud (2356) na at-Tirmidhiy (696) ambaye ameifanya kuwa nzuri.

[5] at-Tirmidhiy (2526) ambaye ameifanya kuwa nzuri na al-Bayahqiy (03/345).

[6] al-Bukhaariy (06) na Muslim (2308).

[7] al-Bukhaariy (2024) na Muslim (1174).

[8] Muslim (759).

[9] al-Bukhaariy (1782) na Muslim (1256).

[10] al-Bukhaariy (1904) na Muslim (1151).

  • Mhusika: Nukhbatin minal-´Ulamaa´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fiqh-ul-Muyassar, uk. 159-160
  • Imechapishwa: 26/04/2020