19. Vitabu vya Allaah ni maneno ya Allaah

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Qur-aan ni maneno ya Allaah na hayakuumbwa. Mtu asidhoofike kusema kuwa hayakuumbwa. Hakika maneno ya Allaah hayakutengana Naye na hakuna kitu katika Yeye ambacho kimeumbwa. Ninakuonya kujadiliana na wale waliozusha katika jambo hili. Mwenye kusema kuwa matamshi ya Qur-aan yameumbwa au akasimama na kusema:

“Sijui kama imeumbwa au haikuumbwa – si jengine Qur-aan ni maneno ya Allaah.”

ni jitu la Bid´ah ni kama yule mwenye kusema kuwa imeumbwa. Qur-aan ni maneno ya Allaah na haikuumbwa.”

MAELEZO

Hapa kunabainishwa ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kuhusu Qur-aan tukufu na madhehebu yanayokwenda kinyume na ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na Salaf kuhusu Qur-aan tukufu. Ni ´Aqiydah na mfumo mzuri ulioje walionao ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah! Ni mfumo na madhehebu mabaya yalioje walionayo wahalifu! Allaah awe radhi na Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah siku zote na kila pahali wanaosema kwamba Qur-aan tukufu ni maneno ya Allaah (´Azza wa Jall) na kwamba maneno ya Allaah ni sifa Yake.

Maneno ya Allaah ni sifa ya kidhati kwa kuzingatia ya kwamba yako kwenye dhati Yake na Mwenye kusifika nayo siku zote.

Maneno ya Allaah ni sida ya kimatendo kwa kuzingatia ushukaji wake; yanashuka kwa kutaka na kupenda kwa Allaah. Allaah aliteremsha Tawraat katika wakati wake, akateremsha Injiyl katika wakati wake, akateremsha Zabuur katika wakati wake na sahifa za Ibraahiym na Muusa katika wakati wake na Qur-aan, ambayo ndio Kitabu cha Ummah huu, katika wakati wake. Allaah aliiteremsha Qur-aan kwa muda wa miaka ishirini na tatu. Kwa hivyo Allaah anaiteremsha Qur-aan kwa kutaka na kupenda Kwake. Kwa njia hii inakuwa ni sifa ya kimatendo. Vitabu vyote hivi ni maneno ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Vyote vimeteremshwa na havikuumbwa. Pamoka na kwamba vitabu hivi vinazungumzia Qur-aan pekee.

Qur-aan tukufu iliyoteremshwa kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa lugha ya kiarabu imeteremshwa kutoka kwa Allaah kikweli. Allaah amezungumza kwayo, Jibriyl ameisikia kutoka Kwake na akaifikisha kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama alivyoisikia ambapo na yeye akawafikishia Ummah pasi na ziada, upungufu wala mabadiliko yoyote. Qur-aan yote imeteremshwa kutoka kwa Allaah. Haikuumbwa. Imeanza kutoka Kwake na itarudi Kwake.

Qur-aan ina herufi, maneno, Suurah na Aayah. Imo ndani ya misahafu. Ni maneno ya Allaah na hakuna yeyote ana haki isipokuwa kuifikisha tu. Hii ndio ´Aqiydah ya Al-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 71-72
  • Imechapishwa: 09/10/2019