19. Ukweli kuhusu mawalii wa Allaah


Salaf na maimamu wa Ummah huu wamekubaliana juu ya kwamba kila mmoja yanachukuliwa maneno yake na kuachwa isipokuwa tu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hii ni moja ya tofauti kati ya Mitume na wasiokuwa wao.  Ni lazima kuamini yale yote ambayo Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) wamekhabarisha kuhusu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Pia ni lazima kuwatii katika wanayoamrisha. Hilo ni tofauti na mawalii wa Allaah ambao si lazima kuwatii na kuamini katika yale yote wanayoamrisha na kueleza. Bali jambo lao na khabari zao zitapimwa juu ya Qur-aan na Sunnah; yale yatayoafikiana na Qur-aan na Sunnah basi italazimika kuyakubali, na yale yanayokwenda kinyume na Qur-aan na Sunnah yatakuwa ni yenye kurudishwa nyuma. Haijalishi kitu hata kama mwenye nayo atakuwa ni walii wa Allaah na aidha atakuwa ni mujtahid na mwenye kupewa udhuru katika yale aliyoyasema. Ni mwenye kulipwa jema juu ya ijtihaad yake, lakini ikiwa ameenda kinyume na Qur-aan na Sunnah atakuwa ni mwenye kukosea kosa ambalo ni lenye kusamehewa muda wa kuwa mwenye nalo amemcha Allaah kiasi na vile anavyoweza…

Haya niliyotaja ya kwamba ni lazima kwa mawalii wa Allaah kushikamana na Qur-aan na Sunnah na kwamba hakuna kati yao aliyekingwa na makosa ambaye inamjuzishia yeye au mwengine kufuata yale yanayomtokea moyoni mwake bila kuzingatia Qur-aan na Sunnah ni miongoni mwa mambo waliyokubaliana mawalii wa Allaah. Anayekwenda kinyume katika hilo basi huyo si katika mawalii wa Allaah (Subhaanah) ambao Allaah ameamrisha kuwafuata. Bali ima akawa ni kafiri au akawa amezembea katika ujinga…

Watu wengi wanakosea katika jambo hili na wakafikiri juu ya mtu kuwa ni walii wa Allaah na wakadhani kuwa yanakubaliwa yale yote yanayosemwa na walii wa Allaah, wakajisalimisha kwake kwa kile atachokisema na wakajisalimisha kwake kwa kila atachokifanya ingawa yatapingana na Qur-aan na Sunnah. Hivyo akaafikiana naye na akaenda kinyume na yale ambayo Allaah amemtumiliza kwayo Allaah na Mtume Wake ambaye Allaah amewaamrisha viumbe wote kumsadikisha katika yale anayoeleza, kumtii katika yale aliyoamrisha na akamfanya kuwa ni kipambanuzi kati ya mawalii na maadui Wake, kati ya watu wa Peponi na watu wa Motoni, kati ya wenye furaha na waliokula maangamivu. Yule anayewafuata basi anakuwa ni miongoni mwa mawalii wenye kumcha Allaah, wanajeshi wake waliofaulu na waja Wake wema. Na yule asiyewafuata anakuwa ni miongoni mwa maadui wa Allaah waliokhasirika watenda mavou. Kwenda kwake kinyume na Mtume na kuafikiana na mtu huyo kutamvuta katika Bid´ah na upotevu na hatimaye katika ukafiri na unafiki… Utawapata wengi katika watu hawa mategemezi yao kumzingatia mtu kuwa ni walii wa Allaah ni kule kuwa kumepatikana kutoka kwake kuyajua baadhi ya mambo yaliyofichikana au amefanya baadhi ya mambo ya ajabu yasiyokuwa ya kawaida… Hakuna chochote katika mambo haya kinachojulisha kuwa mwenye nayo ni walii wa Allaah. Bali mawalii wa Allaah wamekubaliana kwamba mtu akiruka hewani au akatembea juu ya maji basi watu hawatodanganyika naye mpaka kutazamwe kumfuata kwake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuafikiana naye katika amri na makatazo yake… Makarama ya mawalii wa Allaah ni jambo kubwa zaidi kuliko mambo hayo.

Mambo haya yasiyokuwa ya kawaida, ingawa yamefanywa na mawalii wa Allaah, huenda akawa ni adui wa Allaah. Mambo haya yasiyokuwa ya kawaida hufanywa na wengi katika makafiri, washirikina, mayahudi na manaswara, wanafiki, wazushi na mashaytwaan. Kwa ajili hiyo haijuzu kudhani kila ambaye anafanya chochote katika mambo haya kwamba eti ni walii wa Allaah. Bali walii wa Allaah huzingatiwa kwa sifa zake, matendo yake na hali zake zilizojulishwa na Qur-aan na Sunnah na hutambuliwa kwa nuru ya Qur-aan, imani, ukweli wa imani ya ndani na Shari´ah ya Uislamu ya nje.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 30-32
  • Imechapishwa: 24/06/2021