Imaam al-Barbahaariy (Rahimahu Allaah) amesema:

9- Tambua kupinda kutoka katika Njia iliyonyooka ni kwa namna mbili. Wa kwanza ni mtu ameteleza akapinda na Njia, pamoja na kuwa hakukusudia isipokuwa kheri. Kosa lake lisichukuliwe kama kiigizo, kwa sababu ni mwenye kuangamia. Mwingine, ameenda kinyume na haki na yale wachaji Allaah waliyokuwemo kabla yake. Huyo ni mpotevu na ni mwenye kuwapoteza wengine na ni shaytwaan aliyeasi katika Ummah huu. Yule mwenye kumfahamu ni lazima kwake kutahadharisha naye na kuwabainishia watu hali yake ili asije yeyote akatumbukia katika Bid´ah yake na akaangamia.

MAELEZO

Wakati Shaykh (Rahimahu Allaah) katika maneno yake yaliyotangulia kuelezea njia sahihi ambayo ni wajibu kwa Muislamu kupita juu yake katika ´Aqiydah na dini yake, akasema kuwa mwenye kutoka nje ya njia hii ni mmoja kati ya watu wawili:

Mtu wa kwanza: Ambaye sio mwenye kukusudia. Malengo yake anataka kheri lakini pamoja na hivyo amepita njia isiyokuwa ya kheri. Kwa kuwa ametoka nje ya njia ya kheri. Ijtihaad haitoshelezi hata kama mtu atakuwa na njia nzuri na makusudio mazuri. Hili halitoshelezi. Pamoja na hivyo ni lazima awe katika njia sahihi. Huyu anazingatiwa kuwa ni mkoseaji. Kadhalika anayeafikiana naye katika hilo na akawa pamoja naye katika kosa, naye ni mwenye kuangamia. Kwa kuwa hii ni njia ya maangamivu. Njia inayotoka nje ya njia ya haki ni maangamivu hata kama mwenye nayo hakukusudia kufanya hivyo na malengo yake yeye alikuwa anakusudia kheri. Hii ndio hali ya wengi ambao wanazua mambo kutoka kwao wenyewe. Hili ni jambo lisilojuzu na wala mtu huyu hafuatwi. Mwenye nayo hayuko katika usawa. Allaah (Jalla wa ´Allaa) amesema:

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ

“Hii ni njia Yangu iliyonyooka, hivyo basi ifuateni na wala msifuate njia za vichochoro vitakufarikisheni na njia Yake.” (06:153)

Njia yoyote ile ambayo inatutoa nje ya njia iliyonyooka, basi sisi tunaikataa hata kama mwenye nayo atakuwa anakusudia kheri na atakuwa na nia njema. Sisi hatumfuati katika hilo. Akiendelea hivyo mwisho wake itakuwa ni maangamivu. Kwa kuwa mwenye kuacha njia sahihi katika safari yake na akachukua njia iliyopinda anaangamia. Vilevile huyu ikiwa kama hakujirudi anaangamia. Vipi basi tumfuate mtu ambaye anapita katika njia ya maangamivu na kusema huyu makusudio na nia yake ni nzuri. Hili halitoshelezi. Mtu azinduke kwa hili.

Mtu wa pili: Ni yule anayekusudia kutoka [nje ya njia iliyonyooka]. Anaijua haki na anajua kwamba anayofuata ni batili, lakini hata hivyo akakusudia jambo hili kwa minajili ya kuwapoteza watu. Mtu wa kwanza nia yake ilikuwa nzuri ya kutaka kutengeneza hali za watu lakini hata hivyo akawa amefuata njia ambayo si sahihi. Huyu wa pili nia yake ni kutaka kuwapoteza watu na kuwatoa katika njia sahihi. Huyu ni shaytwaan. Kwa sababu mashaytwaan kazi yao ni kuwatoa watu katika njia iliyonyooka. Hii ndio kazi ya mashaytwaan wa kibinaadamu na wa kijini. Ibliys anamwambia Mola Wake (´Azza wa Jall):

لَأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ

“Nitawakalia katika njia Yako iliyonyooka.” (07:16)

Anataka kuwatoa katika njia iliyonyooka na kuwapeleka katika njia zilizopinda. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipigia hili mfano pindi alipopiga msitari uliyonyooka na pembezoni mwake akapiga misitari mingine. Halafu akasema kuhusu njia ile iliyonyooka:

“Hii ni njia ya Allaah.”

Kisha akasema (Swalla Allaah ´alayhi wa sallam) kuhusu ile misitari mingine:

“Hizi ni njia za vichochoro. Katika kila kichochoro kuna shaytwaan anayewaita watu kwayo.”[1]

Huu ni mfano ulio wazi kabisa na unaafikiana na haya yaliyosemwa na Shaykh hapa. Yule anayewatoa watu katika njia iliyonyooka na kuwapeleka katika njia za vichochoro zilizozuliwa, hakika hawatakii kheri. Uhakika wa mambo ni kuwa anachowatakia ni maangamivu. Huyu ni shaytwaan. Ni mamoja kama atakuwa ni katika mashaytwaan wa kibinaadamu au wa kijini.

Ni juu yetu kutahadhari na mtu huyu zaidi kuliko tutakavyotahadhari na yule mtu wa kwanza. Kwa kuwa huyu wa pili ni mwenye kukusudia kuwapoteza watu.

[1] an-Nasaa´iy (06/343), Ahmad (01/435) na wengineo.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Sharh-is-Sunnah, uk. 46-47
  • Imechapishwa: 28/12/2017