19. Sura ya pili: Shahaadah mbili, maana zake, nguzo zake, sharti zake, muqtadha zake na mambo yanayozichengua


Mosi: Maana ya shahaadah mbili.

Maana ya “Kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” ni kuamini na kukubali ya kwamba hakuna anayestahiki ´ibaadah isipokuwa Allaah, kulazimiana nalo na kulitendea kazi. Sentesi “hapana mungu” ni kukanusha kustahiki ´ibaadah kwa mwengine asiyekuwa Allaah yeyote awaye. Sentesi “… isipokuwa Allaah” ni kumthibitishia Allaah pekee ndiye anayestahiki kuabudiwa. Maana ya neno hili kwa ujumla ni kwamba hakuna mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Ni lazima makanusho yafuatiwe na neno ´kwa haki`. Haijuzu kuifuatishia waungu wengine kwa sababu hilo linapingana na ukweli wa mambo. Waungu wengine wanaoabudiwa badala ya Allaah wanapatikana kwa wingi. Hivyo itapelekea kwamba kuabudiwa kwa vitu hivi ni kuabudiwa kwa Allaah, jambo ambalo ni batili kubwa. Haya ndio madhehebu ya Wahdat-ul-Wujuud ambao ndio makafiri wakubwa wa ardhini. Neno hili limefasiriwa kwa tafsiri mbalimbali za kimakosa ikiwa ni pamoja na:

1- Kwamba maana yake ni kuwa hakuna mwabudiwa isipokuwa Allaah. Tafsiri hii ni batili. Kwa sababu hiyo ina maana kwamba kila kinachoabudiwa kwa haki au kwa batili ni Allaah. Hayo tumetoka kuyabainisha punde tu.

2- Kwamba maana yake ni kuwa hakuna muumbaji isipokuwa Allaah. Hii ni sehemu tu ya maana ya neno hili. Lakini hata hivyo sio malengo. Kwa sababu haithibitishi zaidi ya Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah isiyotosheleza. Jengine hii ni Tawhiyd ya washirikina.

3- Kwamba hakuna mwenye kuhukumu isipokuwa Allaah. Hii pia ni sehemu tu ya maana  yake na sio malengo yake. Kwani haitoshi. Kwa sababu endapo mtu atampwekesha Allaah kwa hukumu peke yake na wakati huohuo akamuomba mwengine asiyekuwa Allaah au akamfanyia kitu katika ´ibaadah hawi mpwekeshaji.

Tafsiri zote hizi ni za batili au pungufu. Tumependa kuyabainisha hayo kwa sababu yanapatikana katika baadhi ya vitabu vinavyoenezwa. Tafsiri sahihi ya neno hili kwa mujibu wa Salaf na wahakiki ni kusema ´hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah` kama tulivyotangulia kusema.

Pili: Maana ya “Kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah” ni kukubali kwa undani na kwa uinje ya kwamba ni mja wa Allaah na Mtume Wake kwenda kwa watu wote, kufanyia kazi yale yanayopelekea katika hilo katika kumtii katika aliyoamrisha, kumsadikisha katika aliyokhabarisha, kujiepusha na yale aliyokataza na kugombeza na asiabudiwe Allaah isipokuwa kwa yale aliyoyawekea Shari´ah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 44-46
  • Imechapishwa: 10/02/2020