Allaah (Ta´ala) Amesema:

وَقُل رَّبِّ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ وَأَعُوذُ بِكَ رَبِّ أَن يَحْضُرُون

“Na sema: “Mola wangu! Najikinga Kwako kutokana na mnong’ono (uchochozi na wasiwasi) wa mashaytwaan. Na najikinga Kwako Mola wasinihudhurie (wasije karibu yangu).” (al-Muuminuun 23 : 97-98)

106- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anasema:

أَعوذ بالله السميع العليم من الشَّيْطانِ الرَّجِيمِ من هَمْزِهِ ونَفْخِهِ ونَفثِه

”Ninajikinga kwa Allaah, Msikivu, Mjuzi, kutokana na Shaytwaan aliyewekwa mbali na Rahmah za Allaah; kwa kiburi chake, kupulizia kwake na kutia kwake wasiwasi.”

Akifanya hivyo kutokana na Kauli Yake (Ta´ala):

وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ

“Na utakapokuchochea uchochezi kutoka kwa shaytwaan, basi omba kinga kwa Allaah (useme: A’uwdhu biLLaahi minash-shaytwaanir-rajiym). Hakika Yeye Ndiye As-Samiy’ul-‘Aliym (Mwenye kusikia yote daima – Mjuzi wa yote daima).” (Fuswswilat 41 : 36)

Adhaana inamkimbiza Shaytwaan.”

107- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wakati kunaponadiwa kwa ajili ya Swalah Shaytwaan hugeuka na kuachia pumzi ili asiweze kusikia adhaana. Wakati adhaana inapokwisha hurudi. Wakati kunapokimiwa kwa ajili ya Swalah hugeuka. Wakati kunapomalizwa kukimiwa hurudi.”

108- Suhayl bin Abiy Swaalih amesema:

“Baba yangu alinituma mimi pamoja na vijana wetu wawili watumwa – au marafiki – kwenda kwa Banuu Haarithah. Mtu akaita jina lake nyuma ya kuta. Mtu aliyekuwa na mimi akapanda juu ya kuta na hakuona kitu. Nikamweleza hilo baba yangu. Akasema: “Lau ningelijua utakutana na hayo nisingelikutuma. Lakini lau utasikia sauti toa adhaana. Mimi nimemsikia Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhu) akieleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wakati kunaponadiwa kwa ajili ya Swalah Shaytwaan hugeuka.”

109- Abu Dardaa (Radhiya Allaahu ´anhu) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisimama kwa ajili ya kuswali. Tukamsikia akisema: “Ninajikinga kwa Allaah na wewe.” Kisha akasema: “Ninakulaani kwa laana ya Allaah” mara tatu. Akanyoosha mkono wake kana kwamba ameshika kitu. Alipomaliza kuswali tukamwambia: “Ee Mtume wa Allaah! Tumekusikia ukisema kitu katika Swalah ambacho hatujawahi kusikia ukikisema na tumeona jinsi umenyoosha mkono wako.” Akasema: “Adui wa Allaah Iblisi alikuja na kimondo cha moto ili kuunguza uso wangu. Hivyo nikasema: “Ninajikinga kwa Allaah na wewe” mara tatu. Halafu nikasema: “Ninakulaani kwa laana kamilifu ya Allaah” mara tatu. Hakurudi nyuma. Ndio nikawa nimetaka kumshika. Ninaapa kwa Allaah, lau isingelikuwa Du´aa ya ndugu yetu Sulaymaan kungelipambazuka hali ya kuwa amefungwa kamba ili watoto wa al-Madiynah waweze kucheza naye.”

110- ´Uthmaan bin Abiyl-´Aasw amesema:

“Ee Mtume wa Allaah! Hakika ya Shaytwaan anijia kati yangu mimi na Swalah yangu na kisomo changu. Ananitatiza. Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Huyo ni Shaytwaan aitwae Khanzab. Ukimuhisi omba kinga kwa Allaah kutokana naye na tema upande wa kushoto mara tatu.”

Nikafanya hivyo na Allaah Akamfanya kuniacha.”

111- Abu Zumayl ameeleza:

“Nilimuuliza Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhu) kuhusu kitu ninachohisi ndani ya nafsi yangu – bi maana kitu katika mashaka. Akajibu: “Ukihisi kitu ndani ya nafsi yako sema:

هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Yeye Ndiye Al-Awwal (wa Awali hakuna kitu kabla Yake) na Al-Aakhir (wa Mwisho hakuna kitu baada Yake) na Adhw-Dhwaahir (Hakuna kitu juu Yake), na Al-Baatwin(Hakuna kitu karibu kuliko Yeye), Naye kwa kila kitu ni ‘Aliym (Mjuzi daima).” (Faatwir 35 : 10)

  • Mhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 73-76
  • Imechapishwa: 21/03/2017