19. Sababu ya kumi na nane ya maisha mazuri: Usitafute shukurani kwa mema unayowafanyia watu

18- Miongoni mwa mambo yenye manufaa makubwa katika kufukuza misononeko ni kuiandaa nafsi yako juu ya kwamba usitafute shukurani isipokuwa tu kutoka kwa Allaah pekee. Pindi utapomtendea wema yule ambaye unastahiki au ambaye hustahiki kumtendea haki, basi tambua kuwa hiyo ni biashara yako pamoja na Allaah. Usitilie sana manani kupokea shukurani za yule uliyemtendea wema. Amesema (Ta´ala) kuhusu wale viumbe Wake maalum:

إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللَّـهِ لَا نُرِيدُ مِنكُمْ جَزَاءً وَلَا شُكُورًا

“Hakika sisi tunakulisheni kwa ajili ya kutafuta uso wa Allaah, hatukusudii kwenu malipo na wala shukurani.”[1]

Hili linakuwa na nguvu zaidi katika kutangamana na wake, watoto na wale ambao kati yako wewe na wao kuna mahusiano ya karibu na yenye nguvu kabisa. Pindi utakuwa ni mwenye kuiandaa nafsi kutopokea shukurani kutoka kwao, basi utakuwa ni mwenye kuipumzisha nafsi yako.

Miongoni mwa mambo yanayopelekea katika utulivu ni kuchukua na kuyafanyia kazi yale mambo yenye ubora kwa kiasi cha ule msukumo wa nafsi pasi na kujilazimisha ambako kutakutia katika simanzi na masikitiko na baadaye unarudi nyuma hali ya kuwa umekosa zile fadhilah kwa sababu umefuata njia isiyokuwa ya sawa, jambo ambalo ni katika hekima. Aidha yale mambo machafumachafu ukayafanya ni mambo mazuri na matamu. Kwa njia hiyo huzidi usafi wa ladha na yakaondoka yale mambo mabayamabaya na machafumachafu.

[1] 76:09

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Wasaa-il-ul-Mufiydah lil-Hayaat-is-Sa´iydah, uk. 31
  • Imechapishwa: 01/07/2020