19. Radd juu ya utata wa kwamba tunaomba kupitia mawalii kwa sababu wana nafasi mbele ya Allaah

Saba: Miongoni mwa shubuha zao ni pale wanaposema kwamba mawalii na waja wema wana nafasi mbele ya Allaah. Amesema (Ta´ala):

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ لَهُمُ الْبُشْرَىٰ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ

“Tanabahi! Hakika mawalii wa Allaah hakuna khofu juu yao na wala hawatohuzunika – wale ambao wameamini na wakawa wanamcha Allaah. Watapata bishara katika uhai wa dunia na wa Aakhirah.”[1]

Kufungamana nao, kutafuta baraka kwa athari zao kunatokamana na kuwaadhimisha na kuwapenda. Kadhalika kumuomba Allaah kwa jaha na kwa haki zao. Wanatoa sababu zengine zisizokuwa hizo.

Jibu ni kwamba waumini wote ni mawalii wa Allaah. Lakini hata hivyo uwalii wao huu unatofautiana kwa kutegemea imani na matendo yao mema. Lakini kukata moja kwa moja kwamba mtu ni walii wa Allaah ni jambo linahitajia dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Yule ambaye Qur-aan na Sunnah vinamshuhudilia kwamba ni walii basi na sisi tunamshuhudilia. Yule ambaye Qur-aan na Sunnah havikumshuhudilia kwamba ni walii basi sisi hatuwezi kumkatia jambo hilo. Lakini hata hivyo tunatarajia kheri kwa waumini. Hata yule ambaye imethibiti katika Qur-aan na Sunnah kwamba ni walii wa Allaah haijuzu kwetu kuchupa mipaka kwake, kutafuta baraka kwake, kumuomba Allaah kwa jaha au kwa haki yake. Hizo ni njia za shirki na ni katika Bid´ah zilizoharamishwa.

Sisi tunawapenda waja wema na tunawaiga katika matendo mema na zile sifa nzuri. Pamoja na hivyo hatupetuki mipaka kwao na kuwanyanyua zaidi ya nafasi zao. Kwani kupetuka mipaka kwa waja wema ndio msingi wa shirki. Hivo ndivo ilivokuwa kwa watu wa Nuuh pindi walipovuka mipaka kwa waja wema. Hatimaye jambo likapelekea kuwaabudu badala ya Allaah. Hivo pia kumetokea shirki katika ´ibaadah kwa sababu ya kuchupa mipaka kwa waja wema.

[1] 10:62-64

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Haqiyqat-it-Tawhiyd, uk. 33-34
  • Imechapishwa: 28/03/2019