19. Qur-aan ni maneno ya Allaah na hayakuumbwa


Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Qur-aan ni maneno ya Allaah na hayakuumbwa. Mtu asidhoofike kusema kuwa hayakuumbwa. Hakika maneno ya Allaah hayakutengana Naye na hakuna kitu katika Yeye ambacho kimeumbwa. Ninakuonya kujadiliana na wale waliozusha katika jambo hili. Mwenye kusema kuwa matamshi ya Qur-aan yameumbwa au akasimama na kusema:

“Sijui kama imeumbwa au haikuumbwa – si jengine Qur-aan ni maneno ya Allaah.”

ni jitu la Bid´ah ni kama yule mwenye kusema kuwa imeumbwa. Qur-aan ni maneno ya Allaah na haikuumbwa.”

MAELEZO

Kama jinsi mnavyojua wenyewe suala hili ni la khatari sana. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah walitiwa katika mtihani mkubwa juu ya suala hili. Katika kilele chao ni Imaam Ahmad. Watu walitiwa jela, wakateswa na kuuawa. Jahmiyyah na Mu´tazilah ndio walisimamia hilo wakati wa al-Ma´muun, al-Mu´taswim na al-Waathiq. Wakati wa makhaliyfah watatu wa ´Abbaasiyyah Jahmiyyah, Mu´tazilah na watu wapotevu wengine waliuweka Ummah katika mtihani mkubwa. Wakawatawala Ahl-us-Sunnah, lakini hata hivyo Allaah akaamua neno la mwisho kuwa kwa wachaji Allaah. Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) akavumilia na kustahamili mateso, jela na taabu kubwa ambayo hata mlima hauziwezi. Ndipo Allaah akainyanyua nafasi na manzilah yake. Akawa kweli ni Imaam wa Ahl-us-Sunnah. Hakuna mwenye kujionyesha kwa Sunnah isipokuwa anajitukuza kwa kujinasibisha na Imaam huyu mkubwa. Allaah aliupa nguvu Uislamu kwa Abu Bakr katika mnasaba wa kuritadi na akaupa nguvu Uislamu kwa Ahmad katika mnasaba wa mtihani, hivyo ndivyo wamevyosema baadhi ya Salaf. Allaah amrehemu na amjaza kheri.

Qur-aan na Sunnah vinatolea ushahidi kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ambayo amezungumza kwayo. Amemfunulia nayo Jibriyl na Jibriyl akamfikishia nayo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah anazungumza pale anapotaka na akitaka. Katika maneno Yake ambayo ni zaidi ya bahari ni pamoja na:

قُل لَّوْ كَانَ الْبَحْرُ مِدَادًا لِّكَلِمَاتِ رَبِّي لَنَفِدَ الْبَحْرُ قَبْلَ أَن تَنفَدَ كَلِمَاتُ رَبِّي وَلَوْ جِئْنَا بِمِثْلِهِ مَدَدًا

“Sema: “Kama bahari ingelikuwa ni wino wa [kuandikia] maneno ya Mola wangu, basi ingelimalizika bahari kabla ya kumalizika maneno ya Mola wangu japokuwa Tungelileta mfano wake kujaza tena.””[1]

Miongoni mwa maneno Yake ni pamoja vilevile na Vitabu vilivyoteremshwa ili kuwanyoosha wanaadamu, kuwaongoza na kuwaokoa kutokana na upotevu na kuwapeleka katika malengo ambayo hakuna mwenye kuyajua isipokuwa tu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hili ni kutokamana na huruma, hekima na ukubwa wa uola Wake kuwateremshia Mitume Vitabu ili vinyooshe maisha ya wanaadamu. Wakiishi kwa mujibu wa Vitabu hivi wanastahiki kuingia Peponi na kupata radhi za Mola. Mwenye kwenda kinyume navyo na kukabiliana navyo kwa ukaidi basi amesimamiwa na hoja na anastahiki adhabu ya makafiri na wale wenye jeuri katika Moto wenye kudumu, kama alivyosema Allaah.

[1] 18:109

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 383-384
  • Imechapishwa: 07/08/2017