Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab amesema:

Halafu mtu anaenda kwenye Rukuu´, kuinuka kutoka kwenye Rukuu´, kusujudu juu ya viungo saba na kuinuka kutoka hapo na kukaa baina ya Sajdah mbili. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ارْكَعُوا وَاسْجُدُوا

“Enyi mloamini! Rukuuni na sujuduni.”[1]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimeamrishwa kujusudu juu ya viungo saba.”[2]

Ni lazima kuwa na utulivu katika vitendo vyote na kupangilia kati ya kila nguzo. Dalili ni Hadiyth kutoka kwa Abu Hurayrah kuhusiana na mtu aliyekuwa akiswali vibaya. Kasema:

“Wakati tulipokuwa tumekaa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuliingia mtu, akaswali kisha akamsalimia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akamwambia “Rudi ukaswali, hakika hujaswali.” Alifanya hivi mara tatu. Mwishoni akamwambia: “Naapa kwa yule aliyekutuma kwa haki; siwezi bora zaidi ya hivi. Nifunze!” Akasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Unaposimama kutaka kuswali, lete Takbiyr. Kisha soma uwezacho katika Qur-aan. Kisha utarukuu mpaka unyooke. Kisha utasimama sawa sawa. Kisha utasujudu mpaka utapotulia katika Sajdah. Kisha utainuka na kutulia katika kikao kisha utafanya hivyo katika swalah zote.”

Tashahhud ya mwisho ni nguzo na ni wajibu kama ilivyo katika Hadiyth ya Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh):

“Kabla hatujafaradhishiwa Tashahhud tulikuwa tukisema: “Salaam zimwendee Allaah kutoka kwa waja Wake, salaam zimwendee Jibriyl na Miykaaiyl.” Akasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Hapana kusema “Salaam zimwendee Allaah kutoka kwa waja Wake, kwani hakika Allaah ni ndiye as-Salaam (Mwenye kutoa amani). Lakini semeni:

التحيات لله، و الصلوات و الطيبات، السلام عليك أيها النبي و رحمة الله و بركاته، السلام علينا و على عباد الله الصالحين، أشهد أن لا إله إلا الله و أشهد أن محمداً عبده و رسوله.

“at-Tahiyyaat lillaah, was-Swalawaat wat-Twayyibaat. as-Salaamu ´alayk ayyuhan-Nabbiy wa Rahmatullaah wa Barakaatuh. as-Salaamu ´alaynaa wa ´alaa ´Ibaadillaah-is-Swaliyhiyn. Asshad an laa ilaaha illa Allaah wa ashhad anna Muhammadan ´abduh wa rasuuluh.”[3]

“at-Tahiyyaat” maadhimisho yote yanamstahiki Allaah kwa njia inayolingana na Ukubwa na Utukufu Wake, kama Rukuu´, Sujuud na kudumu milele. Vyote ambavyo Mola wa walimwengu huadhimishwa kwavyo, vinamstahiki Allaah. Atakayemfanyia katika hayo chochote asiyekuwa Allaah ni mshirikina kafiri.

“as-Swalawaat” maana yake ni du´aa zote na imesemekana kuwa maana yake ni zile swalah tano.

“at-Twayyibaat”. Allaah ni Mzuri na wala hayakubali maneno na vitendo isipokuwa mazuri tu.

“as-Salaamu ´alayk ayyuhaan-Nabiyy wa Rahmatullaah wa Barakaatuh.” Wamuombea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amani, rehema na baraka. Anaombewa, na wala haombwi pamoja na Allaah.

”as-Salaamu ´alaynaa wa ´alaa ´Ibaadillaah-is-Swaliyhiyn”. Wajiombea salaam mwenyewe na kwa kila kiumbe mwema katika mbingu na ardhi. as-Salaam ni du ´aa huombewa waja wema lakini haitakiwi kuwaomba wao pamoja na Allaah.

“Ashhad an laa ilaaha illaa Allaah wa ashhad anna Muhammadan ´abduhu wa rasuuluh”. Unashuhudia shahaadah ya yakini ya kwamba hakuna anayestahiki kuabudiwa kwa haki katika ardhi wala mbinguni isipokuwa Allaah. Kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah ina maana ni mja asiyeabudiwa na ni Mtume asiyekadhibishwa, bali anatiiwa na kufuatwa. Allaah Kamtukuza kwa kuwa mja. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

تَبَارَكَ الَّذِي نَزَّلَ الْفُرْقَانَ عَلَى عَبْدِهِ لِيَكُونَ لِلْعَالَمِينَ نَذِيرًا

“Amebarikika Yule ambaye ameteremsha Pambanuzi kwa mja Wake ili awe ni muonyaji kwa walimwengu.”[4]

اللهم صل على محمد و على آل محمد كما صليت على إبراهيم و على آل إبراهيم، إنك حميد مجيد

“Allaahumma swalli ´alaa Muhammad wa aali Muhammad kamaa swallayt ´alaa ´Ibraahiym – innaka Hamiydum-Majiyd”.[5]

Allaah kumswalia mja Wake ni kule kumsifu katika ulimwengu wa juu. Kama alivyosema al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake kutoka kwa Abul-´Aaliyah aliyesema:

“Allaah kumswalia mja Wake ni kule kumsifu katika ulimwengu wa juu.”[6]

Imesemekana vilevile kwamba ni rehema, lakini ya kwanza ndio sahihi zaidi.

Ama kuhusiana na kwamba Malaika pia wanafanya hivyo, maana yake ni kwamba wanamwombea msamaha, na kwamba wanaadamu wanafanya hivyo, maana yake ni du´aa. Ama kuhusu:

اللهم بارك على محمد و على آل محمد كما باركت على إبراهيم و على آل إبراهيم، إنك حميد مجيد

“Allaahumma baarik ´alaa Muhamma wa aali Muhammad kamaa barakta ´alaa Ibraahiym wa ´alaa aali Ibraahiym innaka hamiydun majiyd.”

na yanayokuja baada yake, yanazingatiwa kuwa ni katika maneno na matendo yaliyopendekezwa.

MAELEZO

Hizi ni nguzo zengine zilizobaki. Amesema (Rahimahu Allaah):

“Halafu mtu anaenda kwenye Rukuu´, kuinuka kutoka kwenye Rukuu´, kusujudu juu ya viungo saba na kuinuka kutoka hapo na kukaa baina ya Sajdah mbili.”

Isitoshe kunatakiwa kuwe na utulifu katika matendo yote. Vilevile matendo haya yanatakiwa kufanyiwa kwa mpangilio. Tashahhud ya mwisho, kukaa katika Tashahhud hiyo, kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Tasliym mbili pia ni nguzo. Dalili ya hilo ni maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ارْكَعُوا وَاسْجُدُوا

“Enyi mloamini! Rukuuni na sujuduni.”

Ameamrisha (Subhaanah) kurukuu na kusujuud. Amri inapelekea katika ufaradhi, ni kama mfano wa maneno Yake (Ta´ala) aliposema:

اعْبُدُوا رَبَّكُمُ

“Mwabuduni Mola wenu.”[7]

Yote haya ni maamrisho ya ufaradhi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nimeamrishwa kujusudu juu ya viungo saba.”

Ni amri ya ufaradhi. Sisi tumeamrishwa kumuiga yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema:

“Swalini kama mlivyoniona nikiswali.”

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Wakati tulipokuwa tumekaa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuliingia mtu, akaswali kisha akamsalimia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akamwambia “Rudi ukaswali, hakika hujaswali.” Alifanya hivi mara tatu. Mwishoni akamwambia: “Naapa kwa yule aliyekutuma kwa haki; siwezi bora zaidi ya hivi. Nifunze!” Akasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Unaposimama kutaka kuswali, lete Takbiyr. Kisha soma uwezacho katika Qur-aan. Kisha utarukuu mpaka unyooke. Kisha utasimama sawa sawa. Kisha utasujudu mpaka utapotulia katika Sajdah. Kisha utainuka na kutulia katika kikao kisha utafanya hivyo katika swalah zote.”

Amemfunza mambo ambayo yanaweza kuwa ni yenye kufichikana kwake. Alimfunza kwanza wudhuu´ na kwamba anatakiwa awe msafi. Kisha aelekee Qiblah. Halafu alete Takbiyrat-ul-Ihraam ambayo ni nguzo kwa mujibu wa maafikiano. Kisha akasema:

“Kisha soma uwezacho katika Qur-aan.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Halafu usome mama wa Qur-aan na kile anachotaka Allaah.”[8]

Hadiyth inayosema:

“Hana swalah yule ambaye hakusoma ufunguzi wa kitabu/swalah.”

inafasiri jambo hilo na kwamba kile awezacho mtu katika Qur-aan ni al-Faatihah na kitu kingine cha ziada. Kusoma al-Faatihah ni nguzo na Suurah nyingine zaidi ya hapo imependekezwa na ni sunnah. Halafu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Kisha utarukuu mpaka unyooke. Kisha utasimama sawa sawa. Kisha utasujudu mpaka utapotulia katika Sajdah. Kisha utainuka na kutulia katika kikao kisha utafanya hivyo katika swalah zote.”

Ni dalili inayoonyesha kwamba mambo haya yanatakiwa kufanywa na kila mtu. Kwa sababu alimfunza mtu yule aliyeswali vibaya na akamwambia ayafanye katika swalah yake yote. Kuna dalili zengine vilevile ikiwa ni pamoja na:

“Swalini kama mlivyoniona nikiswali.”

Ameyapangilia kwa mpangilio: kusimama, kurukuu, kuinuka kutoka kwenye Rukuu´, kusujudu. Ni lazima kuyapangilia kwa mpangilio huu. Ni lazima kwetu kuswali kama alivoswali (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni lazima kwetu kumuiga Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu yeye ndiye mwenye kufasiri zile Aayah za Qur-aan zilizokuja kwa jumla. Allaah amesema kwa kuachia:

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ

“Simamisheni swalah.”[9]

حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ وَالصَّلَاةِ الْوُسْطَىٰ وَقُومُوا لِلَّـهِ قَانِتِينَ

”Shikamaneni na swalah na khaswakhaswa swalah ya katikati na simameni mbele ya Allaah katika hali ya utiifu.[10]

Hata hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametufasiria namna swalah inavotakiwa kuwa kwa matendo na maneno yake. Namna hii ndivo swalah inatakiiwa kupangiliwa.

Tashahhud ya mwisho pia ni nguzo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliisoma na akaiamrisha kwa kusema:

“Lakini semeni… “

Kuamrisha kwake kunapelekea katika uwajibu. Ibn Mas´uud amesema:

“Kabla hatujafaradhishiwa Tashahhud tulikuwa tukisema… “

Ni dalili inayofahamisha kwamba Tashahhud ni faradhi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwafunza Maswahabah zake na akawaamrisha nayo. Ni dalili inayoonyesha kuwa ni faradhi. Kuna Tashahhud mbili. Tashahhud ya kwanza na Tashahhud ya pili. Tashahhud ya kwanza inahesabika ni katika wajibu. Kwa sababu pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoisahau aliilipiza kwa Sujuud mbili. Hapo swalah yake ikawa sahihi. Ni dalili inayofahamisha kwamba sio faradhi, bali ni jambo la wajibu ambalo linaanguka kwa kusahau au kwa ujinga. Kuhusu Tashahhud ya mwisho ni nguzo ambayo ni lazima ifanywe. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliihifadhi katika swalah zake zote.

Vivyo hivyo kukaa katika Tashahhud. Ni lazima itekelezwe katika hali ya kukaa na si katika hali ya kusimama.

Tasliym mbili pia ni nguzo. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitoa salamu katika swalah zake zote kuliani na kushotoni. Kwa hiyo ni nguzo. Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Swalini kama mlivoniona nikiswali.”[11]

“at-Tahiyyaat” maadhimisho yote yanamstahiki Allaah kwa njia inayolingana na Ukubwa na Utukufu Wake, kama Rukuu´, Sujuud na kudumu milele. Mwenye kumfanyia Rukuu´ au akamsjudia asiyekuwa Allaah – hali ya kumwabudu – ni shirki kubwa. Ni shirki kubwa kuamini kuwa kuna mwengine asiyekuwa Allaah ambaye ni mwenye kudumu na kwamba hawana mwanzo wala mwisho. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) peke yake ndiye mwenye kudumu:

هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ

“Yeye ndiye wa mwanzo na wa mwisho.”[12]

Yeye ndiye wa milele.

Kuhusu wakazi wa Peponi, wameumbwa. Baada ya hapo ndio watadumu maishani. Kadhalika wakazi wa Motoni; baada ya wao kuumbwa na kuingizwa Motoni kwa sababu ya matendo yao, ndipo watadumishwa Motoni milele. Hata wakazi wa Peponi ambao wameingia Peponi kwa sababu ya matendo yao watadumu humo milele. Allaah ndiye kawafanya kudumu humo milele. Hiyo ni fadhilah ya Allaah kwa watu wa Peponi na ni uadilifu wa Allaah kwa watu wa Motoni.

“as-Swalawaat” kunaingia zile swalah zote tano na du´aa. Zote zinaingia humo. Ni mamoja zile za faradhi na za sunnah.

“at-Twayyibaat” matendo na maneno yote mazuri ni kwa ajili ya Allaah pekee.

Baada ya hapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaombewa amani, rehema na baraka. Shaykh amesema:

“Anaombewa, na wala haombwi pamoja na Allaah.”

Hii ni instinbaatw kubwa. Ina maana kwamba yule mwenye kuombewa ni muhitaji. Ni vipi basi ataombwa pamoja na Allaah? Vivyo hivyo du´aa kuwaombea waja wa Allaah wema. Ni dalili inayofahamisha kwamba waja wema hawaombwi pamoja na Allaah, kwa sababu wao pia wanahitajia kuombewa. Wao wenyewe ni wenye kuhitajia Allaah awasamehe, awasalimishe na awahurumie. Vipi basi wataombwa pamoja na Allaah?

“Ashhad an laa ilaaha illaa Allaah… “ Unashuhudia shahaadah ya kweli kwamba hakuna mwabudiwa wa haki ardhini wala mbinguni isipokuwa Allaah pekee. Hii ndio haki. Amesema (Ta´ala):

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ هُوَ الْبَاطِلُ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ

“Hivyo ni kwa kuwa Allaah ndiye wa haki na kwamba vile wanavyoomba badala Yake ndiyo batili na kwamba Allaah ndiye Aliye juu kabisa, Ametukuka, Mkubwa.”[13]

 “… wa ashhad anna Muhammadan ´abduhu wa rasuuluh”. Unashuhudia shahaadah ya kweli kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, Mtume wa mwisho na kwamba ni mjumbe kutoka kwa Allaah. Yule mwenye kukanusha ujumbe wake au kwamba ndiye Mtume wa mwisho basi amekufuru.

اللهم صل على محمد و على آل محمد كما صليت على إبراهيم و على آل إبراهيم، إنك حميد مجيد

“Allaahumma swalli ´alaa Muhammad wa aali Muhammad kamaa swallayt ´alaa ´Ibraahiym – innaka Hamiydum-Majiyd.”[14]

Allaah kumswalia mja Wake ni kule kumsifu katika ulimwengu wa juu. Imesemwa pia kwamba ni rehema. Maoni ya kwanza ndio ya sawa Wakati swalah inapotajwa kwa kuachia, rehema pia inaingia ndani. Wakati swalah na rehema vinapotajwa kwa pamoja swalah inakuwa ni sifa na rehema ni kuwatendea wema waja. Amesema (Subhaanah):

أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

“Hao zitakuwa juu yao sifa kutoka kwa Mola wao na rehema; na hao ndio wenye kuongoka.”[15]

Bi maana Allaah atawasifu na kuwarehemu. Amesema (Ta´ala):

هُوَ الَّذِي يُصَلِّي عَلَيْكُمْ وَمَلَائِكَتُهُ لِيُخْرِجَكُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ ۚ وَكَانَ بِالْمُؤْمِنِينَ رَحِيمًا

“Yeye ndiye anakusifuni na Malaika Wake wanamuomba akughufurieni na akurehemuni ili akutoeni kutoka katika viza kuingia katika nuru; Naye ni Mwenye kurehemu waumini.”[16]

Bi maana anakusifuni na kukurehemuni (Subhaanah). Kwa hiyo wakati swalah inapotajwa kwa kuachia, rehema pia inaingia ndani, na wakati swalah na rehema vinapotajwa kwa pamoja, swalah inakuwa ni kusifu kutoka kwa Allaah. Abul-´Aaliyah aliyesema:

“Allaah kumswalia mja Wake ni kule kumsifu katika ulimwengu wa juu.”

“Aali” ni wale watu wa nyumbani kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wafuasi wa dini yake.  Ni wale watu wa familia yake akiwemo ´Aliy, al-´Abbaas na wengineo waliomuamini. Kadhalika wale wengine wote waliomuamini. Wote hawa wanaingia katika kizazi chake. Kutajwa Maswahabah baada ya kutaja kizazi (aali) ni kwa minajili ya kukazia. Hapa ni pale ambapo itafasiriwa kama wafuasi. Na ikiwa kizazi itafasiriwa kama watu wa nyumbani kwake, basi ni kwa minajili ya kukazia kwa sababu watu wa familia yake wana umaalum kuliko Maswahabah.

Ama kuhusiana na kwamba Malaika pia wanafanya hivyo, maana yake ni kwamba wanamwombea msamaha na rehema. Kusema kwamba wanaadamu wanafanya hivyo, maana yake ni du´aa. Kwa mfano wakati wa swalah ya jeneza waliohai wanamuombea yule maiti Allaah amrehemu.

[1] 22:77

[2] al-Bukhaariy (810) na Muslim (490).

[3] al-Bukhaariy (6251) na Muslim (397).

[4] 25:01

[5] al-Bukhaariy (3370) na Muslim (406).

[6] al-Bukhaariy (4797).

[7] 02:21

[8] Abu Daawuud (859), Ahmad (18995) na al-Bayhaqiy (2/374). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (805).

[9] 02:43

[10] 02:238

[11] al-Bukhaariy (631).

[12] 53:03

[13] 22:62

[14] al-Bukhaariy (3370) na Muslim (406).

[15] 02:157

[16] 33:43

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mumtaaz, uk. 115-117
  • Imechapishwa: 15/07/2018