19. Namna mbalimbali ya kuswali swalah ya Tarawiyh na Witr

Ndugu wapendwa! Allaah amewawekea Shari´ah waja Wake ´ibaadah za aina mbalimbali ili waweze kuchuma fungu katika kila aina na ili wasichoke kwa aina moja na matokeo yake wakaacha kutenda na mmoja wao akala maangamivu na kuharibikiwa. Pia amejaalia ndani yake faradhi na hivyo haijuzu kuzifanyia upungufu wala kasoro. Ndani yake vilevile mna Nawaafil ambazo mtu anajikurubisha kwa Allaah zaidi na kukamilisha.

Miongoni mwa hayo ni swalah. Allaah amewafaradhishia waja Wake vipindi vitano mchana na usiku ambapo ni tano kimatendo na khamsini katika mizani. Allaah akapendekeza kuzidi kujitolea kwa swalah za sunnah mbalimbali ambazo zitakuja kukamilisha faradhi hizi na ziada ya kujikurubisha Kwake. Miongoni mwa Nawaafil hizo ni Rawaatib zilizoambatana na swalah zilizofaradhishwa; Rak´ah mbili kabla ya swalah ya Fajr, Rak´ah nne kabl ya Dhuhr na Rak´ah mbili baada yake, Rak´ah mbili baada ya Maghrib na Rak´ah mbili baada ya ´Ishaa. Miongoni mwazo ni swalah za usiku ambazo Allaah amewasifu ndani ya Kitabu Chake wale wenye kuziswali kwa kusema (Subhaanah):

وَالَّذِينَ يَبِيتُونَ لِرَبِّهِمْ سُجَّدًا وَقِيَامًا

“Na wale wanaokesha usiku kwa ajili ya Mola wao hali ya kusujudu na kusimama.”[1]

تَتَجَافَىٰ جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ خَوْفًا وَطَمَعًا وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Mbavu zao zinatengana na vitanda wakimuomba Mola wao kwa khofu na matumaini na katika yale tuliyowaruzuku wanatoa. Hivyo basi, nafsi yoyote haijui yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho – ni malipo kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah bora baada ya faradhi ni swalah ya usiku.”

Ameipokea Muslim.

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Enyi watu! Enezeni salamu, lishizeni chakula, waungeni ndugu na swalini usiku wakati watu wamelala mtaingia Peponi kwa usalama.”

Amepokea at-Tirmidhiy ambaye amesema:

“Nzuri na Swahiyh.” al-Haakim pia ameisahihisha.

Miongoni mwa swalah za usiku ni pamoja na Witr. Uchache wake ni Rak´ah moja na wingi wake ni Rak´ah kumi na moja. Inafaa kwa mtu kuwitiri kwa Rak´ah moja kivyake. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kutaka kuswali Witr kwa moja na afanye hivo.”

Ameipokea Abu Daawuud na an-Nasaa´iy.

Pia inafaa kwake kuswali Witr kwa Rak´ah tatu. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kutaka kuswali Witr kwa tatu na afanye hivo.”

 Ameipokea Abu Daawuud na an-Nasaa´iy.

Akitaka kuzifululiza zote kwa salamu moja inafaa. Hilo ni kutokana na yale aliyopokea at-Twahaawiy kwamba ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) aliswali Witr Rak´ah tatu na hakutoa salamu isipokuwa katika ile ya mwisho. Vilevile akitaka ataswali Rak´ah mbili kisha atatoa salamu kisha aswali nyingine ya tatu. Hayo ni kutokana na yale aliyopokea al-Bukhaariy kwamba ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alikuwa akitoa salamu baina ya Rak´ah mbili na Rak´ah moja katika Witr mpaka akiamrisha baadhi ya haja zake. Inafaa pia kuswali Witr kwa Rak´ah tano akazifululiza zote ambapo hatoketi chini wala hatotoa salamu isipokuwa katika ile ya mwisho. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kutaka kuswali Witr kwa tano na afanye hivo.”

Ameipokea Abu Daawuud na an-Nasaa´iy.

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali sehemu katika usiku Rak´ah kumi na tatu. Akiswali Witr kwa tano na haketi chini kwenye yoyote katika hizo isipokuwa katika ile ya mwisho wake.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Vilevile inafaa kuswali Witr kwa Rak´ah saba akazifululiza zote kama alivofanya kwa zile tano. Hilo ni kutokana na maneno ya Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesimulia:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali Witr kwa saba na kwa tano. Hapambanui kati yazo kwa salamu wala maneno.”

Ameipokea Ahmad, an-Nasaa´iy na Ibn Maajah.

Vilevile inafaa kuswali Witr kwa Rak´ah tisa akazifululiza zote na hatoketi chini isipokuwa katika ile Rak´ah ya nane ambapo atasoma Tashahhud na ataomba du´aa, kisha baada ya hapo atasimama na hatotoa salamu halafu ataswali ile Rak´ah ya tisa ambapo ataomba du´aa na kutoa salamu. Hayo ni kutokana na Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiy Allaahu ´anhaa) kuhusu Witr ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo amesimulia:

“Alikuwa akiswali Rak´ah tisa ambapo haketi chini isipokuwa katika ile ya nane ambapo anamdhukuru Allaah na kumhimidi na anamuomba du´aa. Kisha anainuka na hatoi salamu. Halafu anasimama na kuswali ile ya tisa kisha anaketi chini na kumdhukuru Allaah na kumhimidi na kumuomba du´aa. Halafu anatoa salamu anayotusikilizisha nayo… “

Ameipokea Ahmad na Muslim.

Mswaliji aswali Rak´ah kumi na moja. Akitaka anaweza kutoa salamu kwa kila baada ya Rak´ah mbili na akaswali Witr Rak´ah moja. Hayo ni kutokana na Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiswali kuanzia pale anapomaliza swalah ya ´Ishaa kwenda mpaka Fajr Rak´ah kumi na moja ambapo akitoa salamu kila baada ya Rak´ah mbili na akiswali Witr kwa moja… “

Wameipokea jopo isipokuwa at-Tirmidhiy.

Akipenda vilevile anaweza kuswali Rak´ah nne, kisha nne na kisha tatu. Hayo ni kutokana na Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesimulia:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali [Rak´ah] nne[3]; usiulize juu ya uzuri wazo na urefu wazo, kisha akiswali [Rak´ah] nne; usiulize juu ya uzuri wazo na urefu wazo, kisha akiswali [Rak´ah] tatu.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Kufululiza Rak´ah tano, saba au tisa inakuwa pale ambapo mtu anaswali peke yake au kundi la waswaliji wamechagua jambo hilo. Ama kuhusu msikitini bora kwa imamu atoe salamu kila baada ya Rak´ah mbili ili asije kuwatia watu uzito. Kitendo hichi ndio chepesi zaidi kwao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote katika nyinyi atawaongoza watu basi achunge; kwani nyuma yake kuna mzee, mnyonge na wenye haja.”

Katika tamko lingine imekuja:

“Akiswali peke yake basi  aswali atakavyo.”

Jengine ni kwa sababa haikunakiliwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaswalisha Maswahabah zake namna hii. Alikuwa akifanya hivo pale anaposwali peke yake.

[1] 25:64

[2] 32:16-17

[3] Kuna uwezekano hizi Rak´ah nne ni kwa salamu moja. Haya ndio yenye kudhihiri katika tamko. Kuna uwezekano vilevile hizi Rak´ah nne alikuwa akitoa salamu kila baada ya Rak´ah mbili. Lakini akiswali Rak´ah nne kisha akaswali tena Rak´ah nne inafaa. Kitendo hichi [cha pili] ndio chenye kuafikiana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Swalah ya usiku ni [Rak´ah] mbilimbili.”

Jengine ni kutokana na Hadiyth ya ´Aaishah iliyotajwa kabla yake ambapo amebainisha kuwa alitoa salamu baina ya kila Rak´ah mbili.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 24-28
  • Imechapishwa: 15/04/2020