19. Mtazamo wa Ahl-us-Sunnah juu ya imani na mtenda dhambi kubwa

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wamesema kuwa mwenye kufanya dhambi kubwa ambayo ni chini ya shirki ni muumini mwenye imani pungufu. Pia mtu anaweza kusema kuwa ni muumini kwa imani yake na ni fasiki kwa dhambi yake kubwa. Akifa basi yuko chini ya matakwa ya Allaah; Allaah akitaka, atamsamehe, na akitaka, atamuadhibu. Lakini akimuadhibu hatomdumisha ndani ya Moto milele:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[1]

Imekuja katika Hadiyth:

“Muondosheni Motoni yule ambaye ndani ya moyo wake mna imani chembe ndogo ndogo ndogo sawa na uzani wa hardali.”[2]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hiyo ni imani dhaifu kabisa.”[3]

Kuna wakati imani inakuwa yenye nguvu na kuna wakati imani dhaifu. Yule mwenye imani hakufuru ijapokuwa atafanya baadhi ya maasi hakufuru. Lakini hata hivyo imani yake inapungua. Hapewi jina la imani kamilifu na wala hapokonywi jina la imani kikamilifu kwa ajili ya kuoanisha kati ya maandiko. Kwa ajili hii Shaykh Taqiyy-ud-Diyn (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hapewi imani ya moja kwa moja na wala hapokonywi imani ya moja kwa moja.”[4]

Hapewi imani ya moja kwa moja, kama wanavoona Murji-ah, wala hapokonywi imani ya moja kwa moja, kama wanavoona Khawaarij na Wa´iydiyyah. Bali anapewa kwa kiasi alichonacho.

Haya ndio madhehebu ya haki na ya kati na kati yanayokusanya kati ya maandiko. Maasi yanaipunguza imani na kuidhoofisha – Radd kwa Murji-ah – lakini hayamtoi mwenye nayo nje ya imani – Radd kwa Khawaari na Wa´iydiyyah.

Mu´tazilah wamezua – kama tulivyotangulia kusema – kitu kinachoitwa nafasi “Nafasi ilio kati ya nafasi mbili” na wakasema kuwa sio muumini na wala sio kafiri. Maneno yao ni batili. Kwa sababu hakuna mtu ambaye sio muumini wala sio kafiri. Ima mtu awe muumini au awe kafiri. Amesema (Ta´ala):

هُوَ الَّذِي خَلَقَكُمْ فَمِنكُمْ كَافِرٌ وَمِنكُم مُّؤْمِنٌ

“Yeye ndiye kakuumbeni, hivyo miongoni mwenu yuko aliye kafiri na miongoni mwenu yuko aliye muumini.”[5]

Ima kafiri au muumini. Muumini ima awe ni muumini mwenye imani kamilifu au awe ni muumini mwenye imani pungufu.

[1] 04:48 na 116

[2] al-Bukhaariy (7510), Muslim (193) na tamko ni lake, kupitia kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh).

[3] Muslim (49) kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh).

[4] al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 40.

[5] 64:02

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 38-39
  • Imechapishwa: 09/03/2021