19. Msingi wa sita: Radd juu ya utata wa kuacha kufata Qur-aan na Sunnah na badala yake kufuata maoni mbalimbali

Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimhu Allaah) amesema:

Msingi wa sita:

Kurudisha utata ambao ameuweka shaytwaan kwa kuacha Qur-aan na Sunnah na badala yake kufuata maoni na matamanio yenye kufarikiana na yenye kutofautiana. Nayo [maoni na matamanio yenyewe] ni kwamba Qur-aan na Sunnah hakuna mwenye kuvijua isipokuwa yule ambaye ni Mujtahid mutlaq [mwanachuoni mkubwa ambaye ana upeo wa kufanya Ijtihaad katika kila fani ya elimu].

MAELEZO

Huu ndio msingi wa mwisho na ni msingi muhimu sana. Wanasema kuwa hawajui Qur-aan na Sunnah na hawawezi kabisa wakavijua. Wanasema kuwa hakuna awezaye kuvijua isipokuwa tu wale wanazuoni wakubwa. Waambiwe kuwa ndani ya Qur-aan yako mambo ya wazi yenye kujulikana na mtu ambaye si msomi na mwanafunzi na hivyo hoja inakuwa ni yenye kusimama juu ya viumbe. Vilevile yako mambo yasiyojulikana isipokuwa na wanazuoni na mengine hakuna mwenye kuyajua isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) pekee.

Ni kweli ndani ya Qur-aan yapo mambo yasiyojua isipokuwa ambaye ni Mujtahid mutlaq. Lakini hata hivyo kuna mambo mengi yanayojulikana na ambao si wasomi na mwanafunzi aliyeanza kusoma ambaye kishachuma elimu kidogo. Mfano wa mambo hayo ni pamoja na maneno Yake (Ta´ala):

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote.” (04:36)

إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ

“Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah atamharamishia Pepo na makazi yake yatakuwa ni Motoni.” (05:72)

وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ

“Na wala msiikaribie zinaa.” (17:32)

حُرِّمَتْ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةُ

“Mmeharamishiwa nyamafu [mzoga].” (05:03)

قُل لِّلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ

“Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao.” (24:30)

Haya ni mambo yaliyo wazi ambayo anayajua ambaye si msomi pale anapoyasikia.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 40
  • Imechapishwa: 19/05/2021