Kwa hiyo mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya haki ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kwamba wanashuhudia juu yake kwa mioyo yao, midomo yao na matendo yao ya kwamba kweli ni Mtume wa Allaah. Isitoshe wanampenda mapenzi ya kumtukuza na kumuadhimisha yanayokuja baada ya mapenzi ya Allaah (´Azza wa Jall). Hawampendi mapenzi ya kumwabudu. Wanampenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa sababu yeye ni Mtume wa Mola wa walimwengu. Kumpenda yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni sehemu ya kumpenda Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Lau Allaah asingelimtuma Muhammad bin ´Abdillaah kutoka katika kabila la Quraysh ukoo wa Haashim basi asingelikuweko mtu kutoka katika ukoo wa Haashim ambaye anastahiki ngazi hii aliyoistahiki yeye kwa sababu ya ujumbe. Sisi tunampenda na kumtukuza kwa sababu tunampenda na kumtukuza Allaah. Kwa sababu yeye ni Mtume wa Allaah na Allaah amewaongoza Ummah kupitia yeye ndio maana tunampenda.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni mwenye kupendwa kwa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Kwani yeye ni mjumbe wa Mola wa walimwengu. Hapana shaka kwamba yeye ndiye mtu mwenye haki zaidi, bali ndiye kiumbe mwenye haki zaidi ya kubeba ujumbe huu mtukufu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kadhalika ni wenye kumtukuza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kikwelikweli na wanaona kuwa ndiye mtu mwenye hadhi ya juu zaidi mbele ya Allaah (´Azza wa Jall). Lakini pamoja na hivo hawamshushi juu ya cheo chake alichoshushwa na Allaah. Wanasema kuwa yeye ni mja wa Allaah. Bali yeye ndiye mtu ambaye anamwabudu Allaah zaidi kiasi cha kwamba anasimama kuswali mpaka miguu yake inapasuka na wakati anapoulizwa kwa nini anafanya hivo ilihali Allaah amekwishamsamehe madhambi yake yaliyokwishatangulia na yaliyobaki nyuma, anajibu kwa kusema:

“Je, sipendi niwe mja mwenye kushukuru?”[1]

 Ni nani anaweza kuhakikisha ´ibaadah kama alivokuwa akihakikisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Kwa ajili hiyo amesema:

“Ninaapa kwa Allaah, si vyenginevyo, ya kwamba mimi ndiye ninayemcha Allaah zaidi na mjuzi zaidi wa yale anayotakiwa kuchwa kwayo.”[2]

Yeye, pasi na shaka yoyote, ndiye mja anayefanya ´ibaadah zaidi na ambaye anaihakikisha zaidi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa ajili hiyo wakati alipozungumzia vitunguu saumu na vitunguu maji waislamu wakasema kuwa vimeharamika. Ndipo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Enyi watu! Mimi sina haki ya kuharamisha yale aliyohalalisha Allaah.”[3]

Tazama adabu hii aliokuwa nayo kwa Allaah (´Azza wa Jall). Namna hii ndio mtu anakuwa mja wa Allaah. Kwa ajili hiyo Ahl-us-Sunnah wanaona kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni mja miongoni mwa waja wa Allaah na ndiye mtu mkamilifu zaidi katika ´ibaadah.

[1] al-Bukhaariy (1130) na Muslim (2819).

[2] al-Bukhaariy (5063) na Muslim (1401).

[3] Muslim (565).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manhaj Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah fiy-´Aqiydah wal-´Amal, uk. 30-31
  • Imechapishwa: 05/08/2019