6- Ni haramu kwa kafiri kumuoa mwanamke wa Kiislamu. Kwa sababu ni kafiri na kafiri si halali kwake kumuoa mwanamke wa Kiislamu, jambo ambalo limethibitishwa kwa dalili za kiwahyi na maafikiano. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا جَاءَكُمُ الْمُؤْمِنَاتُ مُهَاجِرَاتٍ فَامْتَحِنُوهُنَّ ۖ اللَّـهُ أَعْلَمُ بِإِيمَانِهِنَّ ۖ فَإِنْ عَلِمْتُمُوهُنَّ مُؤْمِنَاتٍ فَلَا تَرْجِعُوهُنَّ إِلَى الْكُفَّارِ ۖ لَا هُنَّ حِلٌّ لَّهُمْ وَلَا هُمْ يَحِلُّونَ لَهُنَّ

“Enyi mlioamini! Wanapokujieni waumini wa kike wahamaji, basi wajaribuni! Allaah anazijua imani zao, kisha mkiwatambua kuwa ni waumini basi msiwarejeshe kwa makafiri; wao [wake] si halali [tena] kwao na wala wao [waume] hawahalaliki kwao.”[1]

Ibn Qudaamah amesema:

“Kuhusiana na makafiri wengine mbali na watu wa Kitabu, wanachuoni wamekubaliana juu ya kwamba ni haramu kuwaoa wanawake wao na kula vichinjwa vyao.”[2]

Amesema vilevile:

“Ni haramu kumuoa mwanamke mwenye kuritadi pasi na kujali dini gani aloingia. Hazingatiwi kuwa na hukumu moja kama wafuasi wa dini hiyo aloingia, seuze awe halali.”

Amesema tena katika mlango kuhusu kuritadi:

“Akioa hivo ndoa yake itakuwa si sahihi kwa sababu haifai kwake akabaki katika hali hiyo. Ikiwa ni haramu kubaki katika hali fulani basi ni haramu vilevile kuoa katika hali hiyo kama mfano wa kafiri kumuoa mwanamke wa Kiislamu.”

Imekuja katika kitabu cha Hanafiyyah “Majmaa´-ul-Anhar”:

“Kwa mujibu wa maafikiano ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) si sahihi kumuoa mwenye kuritadi.”[3]

Unaona namna ambavyo anasema wazi kuwa ni haramu kumuoa mwanamke mwenye kuritadi na kwamba ndoa ya mwenye kuritadi si sahihi. Kuna nini lau kuritadi kutatokea baada ya kufunga ndoa? Ibn Qudaamah amesema:

“Mmoja katika wanandoa ataporitadi, ndoa inafutika moja kwa moja. Katika hali hiyo hakuna atayemrithi mwenzie. Ikiwa mwanaume ataritadi baada ya kufanya jimaa, Imaam Ahmad ana maoni mawili. Moja inasema kuwa mtengano utapitika papo hapo na maoni mengine yanasema kuwa atakaa eda yake.”[4]

Amesema vilevile kwamba wanachuoni wengi wanaonelea kuwa kuritadi kabla ya jimaa kunasababisha mtengano papo hapo na wakataja dalili juu ya hilo. Maalik na Abu Haniyfah wanaonelea pia kuwa kuritadi baada ya jimaa kunasababisha mtengano wa papo hapo ambapo ash-Shaafi´iy anaonelea kuwa anatakiwa kukaa eda yake[5].

Haya yanapelekea kwamba maimamu wanne wote wameafikiana juu ya kwamba ndoa ni yenye kutenguka kwa mmoja katika wanandoa kuritadi. Ikiwa kuritadi kutatokea kabla ya jimaa, basi ndoa inafutika papo hapo. Ikiwa ni baada ya jimaa, Maalik na Abu Haniyfah wanaonelea kuwa inatenguka papo hapo ambapo ash-Shaafi´iy anaonelea kuwa akae eda yake. Kutoka kwa Ahmad kama ilivyosemwa kumepokelewa maoni yote mawili. Ibn Qudaamah amesema:

“Wanandoa wote wawili wakiritadi, basi hukumu yao ni ile ile lau kama mmoja wao angeritadi; kuritadi kukitokea kabla ya jimaa ndoa inafutika moja kwa moja. Ikiwa ni baada ya jimaa je ndoa inafutika papo hapo au anatakiwa kukaa eda? Ahmad ana maoni mawili kuhusiana na suala hili. Haya ndio maoni ya ash-Shaafi´iy vilevile.”[6]

Kisha akataja maoni ya Abu Haniyfah ya kwamba ndoa yao haitenguki kwa sababu dini zao hazitofautiani na kwamba wanafanana na wale wanandoa wanaosilimu pamoja. Baada ya hapo akarudisha kipimo chake cha kufukuza na cha kukanusha.

Pindi itapobainika kuwa si sahihi kwa muislamu kuoa/kuolewa na mwenye kuritadi kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah na kwamba asiyeswali ni kafiri kwa mujibu wa Qur-aan, Sunnah na maoni ya wengi katika Maswahabah, itakuwa wazi kwamba si sahihi kwa mwanaume ambaye haswali kumuoa mwanamke muislamu. Mwanamke huyo hawi halali kwake kwa kumuoa. Endapo atatubu kwa Allaah na akarudi katika Uislamu basi ni wajibu kwao kufunga ndoa upya tena. Hukumu iko vivyo hivyo ikiwa ni mwanamke ndiye ambaye haswali.

Mambo kama haya hayahusu ndoa za makafiri. Iwapo mwanaume kafiri atamuoa mwanamke wa kikafiri kisha mwanamke huyu akasilimu kabla ya jimaa, ndoa inafutika papo hapo. Ikiwa amesilimu baada ya jimaa, ndoa haifutiki. Lakini anatakiwa kusubiri. Mume akisilimu kabla ya eda yake kuisha, atabaki kuwa mke wake. Na ikiwa eda yake itakwisha kabla ya yeye kusilimu, basi atakuwa hana haki yoyote juu yake. Itabaini kuwa ndoa imefutika tangu pale aliposilimu.

Makafiri katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakisilimu pamoja na wake zao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwakubalia ndoa zao. Isipokuwa ikiwa kama kutakuwa kikwazo kingine cha ndoa kama kwa mfano wanandoa walikuwa ni waabudu moto au wanandugu ambao ni haramu kuoana. Wanandoa kama hawa wakisilimu watatenganishwa kwa sababu bado watakuwa ni haramu kuoana.

Masuala haya sio kama suala la muislamu ambaye amekufuru kwa sababu haswali kisha akamuoa mwanamke wa Kiislamu. Mwanamke wa Kiislamu sio halali kwake kuolewa na mwanaume kafiri, kama ilivyothibitishwa kwa dalili za kiwahyi na maafikiano, hata kama atakuwa ni kafiri wa asli na sio mwenye kuritadi. Lau mwanaume kafiri atamuoa mwanamke wa Kiislamu ndoa yao itakuwa ni batili na ni wajibu kuwatenganisha. Ikiwa mwanaume huyu atasilimu na akataka kumuoa wanatakiwa kufunga ndoa upya.

[1] 60:10

[2] al-Mughniy (6/592).

[3] 1/302.

[4] al-Mughniy (6/298).

[5] al-Mughniy (6/639).

[6] al-Mughniy (6/640).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Hukm Taarik-is-Swalaah, uk. 18-21
  • Imechapishwa: 22/10/2016