95- Kisha ataenda mahali pa kuchinjia Minaa na atekeleze kichinjwa chake. Hii ndio Sunnah.

96- Lakini inafaa kwake kuchinja sehemu yoyote Minaa. Vivyo hivyo Makkah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimechinja hapa na Minaa kote ni mahali ambapo mtu anaweza kuchinja. Njia zote pana za Makkah ni njia na sehemu ya kuchinjia. Kwa hiyo chinjeni pale mnapotua.”[1]

97- Sunnah ni yeye kuchinja mwenyewe kwa mikono yake akiweza kufanya hivo. Vinginevyo aweke naibu mtu mwingine amchinjie.

98- Amchinje mnyama kwa kumwelekeza Qiblah[2]. Mnyama anatakiwa kulazwa upande wake wa kushoto na mchinjaji amkanyage kwenye upande wake wa kulia[3].

99- Kuhusu ngamia Sunnah ni kumchinja hali ya kuwa amefungwa mguu wake wa kushoto[4], apate kusimama kwa miguu yake mitatu na aelekezwe Qiblah[5].

100- Aseme wakati wa kuchinja:

بسم الله والله أكبر. اللهم إن هذا منك ولك اللهم تقبل مني

“Kwa jina la Allaah na Allaah ni mkubwa. Ee Allaah! Hakika hii inatoka Kwakona ni Yako[6]. Ee Allaah! Nitakabalie.”[7]

101- Wakati wa kuchinja ni katika yale masiku nne ya ´Iyd. Haya ndio masiku ya Nahr – na ndio masiku ya Hajj kubwa[8] – na siku tatu za Tashriyq. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Masiku yote ya Tashriyq ni ya kuchinja.”[9]

102- Inafaa kwake kula katika kichinjwa chake. Vilevile inafaa kwake kuchukua baadhi ya nyama yake kwenda katika nchi yake, kama alivofanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

103- Ni lazima kwake kuwalisha katika kichinjwa hicho mafukara na wahitaji. Amesema (Ta´ala):

وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّـهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ ۖ فَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَيْهَا صَوَافَّ ۖ فَإِذَا وَجَبَتْ جُنُوبُهَا فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْقَانِعَ وَالْمُعْتَرَّ

“Budn (ngamia, ng´ombe,  kondoo na mbuzi) Tumekufanyieni kuwa ni miongoni mwa ishara za Allaah; kwa hao mnayo kheri nyingi. Basi tajeni Jina la Allaah juu yao wanapopangwa safu [kwa ajili ya kuchinjwa]. Na waangukapo ubavu, basi kuleni kutoka humo na lisheni waliokinai na wanaolazimika kuomba. Hivyo ndivyo Tulivyowatiisha kwa ajili yenu ili mpate kushukuru.”[10]

104- Inajuzu kwa watu saba kushirikiana katika ngamia na ng´ombe.

105- Yule asiyepata kichinjwa, ni wajibu kwake kufunga siku tatu katika hajj na siku tatu ataporejea kwa familia yake.

106- Inafaa kwake kufunga katika masiku ya Tashriyq kujengea juu ya Hadiyth ya ´Aaishah na Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa):

“Haikuruhusiwa kufunga katika masiku ya Tashriyq isipokuwa kwa yule ambaye hakupata kichinjwa.”[11]

107- Kisha anyoe kichwa kizima au apunguze. Hilo la kwanza ndio bora zaidi kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ee Allaah! Warehemu wanyoaji.” Wakasema: “Na waliopunguza, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ee Allaah! Warehemu wanyoaji.” Wakasema: “Na waliopunguza, ee Mtume wa Allaah?” Ilipofika mara ya nne ndipo akasema: “Na waliopunguza.”[12]

108- Sunnah kwa mnyoaji aanze kunyoa upande wa kulia, kama ilivyo katika Hadiyth ya Anas (Radhiya Allaahu ´anh)[13].

109- Kunyoa ni jambo maalum kwa wanaume pasi na wanawake. Kuhusu wanawake wao wanatakiwa tu kupunguza nywele. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Si wajibu kwa wanawake kunyoa. Kilicho cha wajibu kwao ni kupunguza.”[14]

Mwanamke anaweza kufanya hivo kwa kuzikusanya nywele zake pamoja halafu azikate mwishoni mwake kwa urefu wa kiasi cha ncha za vidole[15].

110- Imesuniwa kwa mtawala kutoa Khutbah siku ya Nahr huko huko Minaa[16] ili kuwafunza watu[17] namna ya ´ibaadah zao za hajj. Haya yanatakiwa kufanyika wakati wa dhuhaa[18] kati ya nguzo ya kutupa za kutupa mawe[19].

[1] Hadiyth hii imewarahisishia mahujaji suala la kuchinja kwa kiasi kikubwa na kuchangia kutatua tatizo la kukusanyika umati wa watu katika sehemu ya kuchinja na kuwalazimisha watawala kuwazika wanyama wengi waliochinjwa katika ardhi hapo.” Anayetaka kuzama zaidi katika jambo hili basi arejee katika “asili”, uk. 87-88.

[2] Kuhusiana na  jambo hili kuna Hadiyth kutoka kwa Jaabir, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Imepokelewa na Abu Daawuud na wengineo na imetajwa pia katika “al-Irwaa´” (1138). Nyingine imepokelewa kwa al-Bayhaqiy (09/285). Imepokelewa pia kutoka kwa Ibn ´Umar kwamba alikuwa akipendekeza kuelekea Qiblah wakati wa kuchinja. ´Abdur-Razzaaq (8585) amepokea kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kutoka kwake kwamba alikuwa akichukizwa kula kichinjwa kilichochinjwa pasi po kuelekea Qiblah.

[3] Haafidhw amesema:

“Hivi ili iwe rahisi kwa mchinjaji ashikilie kisu kwa mkono wake wa kuume na kichwa cha mnyama kwa mkono wake wa kushoto.” (Fath-ul-Baariy (10/16))a

[4] Swahiyh Abiy Daawuud (1550). Ndani yake baada yake kuna upokezi kama ushahidi kutoka katika Hadiyth ya Ibn ´Umar. Imepokelewa na al-Bukhaariy na Muslim.

[5] Ameipokea Maalik kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kutoka kwa Ibn ´Umar. al-Bukhaariy ameipokea kwa cheni ya wapokezi pungufu kwa njia ya kuthibiti. Tazama ufupisho wangu wa al-Bukhaariy (330).

[6] Ameipokea al-Bukhaariy na wengineo kutoka katika Hadiyth ya Jaabir. Ina upokezi mwingine kama ushahidi kutoka katika Hadiyth ya Abu Sa´iyd al-Khudriy iliyopokelewa na Abu Ya´laa, kama ilivyo katika “al-Majma´” (04/22). Imetajwa katika “al-Irwaa´” (1118).

[7] Ameipokea Muslim na wengineo kutoka kwa ´Aaishah. Imetajwa katika “al-Irwaa´”. Shaykh-ul-Islaam ameongeza katika “al-Mansik” yake:

“Kama Ulivyomkubalia kipenzi Wako wa hali ya juu Ibraahiym.”

Sikuipata katika kitabu chochote vya Sunnah nilivyonavyo.

[8] Ameipokea al-Bukhaariy kwa cheni ya wapokezi pungufu wakati Abu Daawuud na wengineo wameipokea kwa cheni ya wapokezi ilioungana. Tazama ”Swahiyh Abiy Daawuud” (1700-1701).

[9] Ameipokea Ahmad. Ni Swahiyh kwa mujibu wa Ibn Hibbaan. Mimi naonelea kuwa ni yenye nguvu kutokana na mkusanyiko wa njia zake. Ndio maana nimeitaja katika ”as-Swahiyhah” (2476).

[10] 22:36

[11] Ameipokea al-Bukhaariy na wengineo. Imetajwa katika “al-Irwaa´” (964). Kuhusu maoni ya Shaykh-ul-Islaam: “Ni lazima kwa Mutamatti´ kufunga baadhi ya siku tatu kabla ya kuhirimia hajj siku ya Tarwiyah”, sijui namna alivyofikia kuonelea hilo. Bali udhahiri wake ni kwamba linapingana na Aayah na Hadiyth – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[12] Ameipokea al-Bukhaariy, Muslim na wengineo kutoka kwa Ibn ´Umar na wengine. Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (1084).

[13] Ameipokea Muslim na wengineo. Imetajwa katika al-Irwaa’” (1085) na Swahiyh Abiy Daawuud” (1730). Masuala haya ni miongoni mwa mambo ambayo ´Allaamah Ibn-ul-Hammaam al-Hanafiy  amekiri kwamba Hanafiyyah wamekwenda kinyume na Sunnah. Wafuataji kichwa mchunga watasema nini hivi sasa kwa kukiri mwenyewe imamu huyu bingwa?

[14] Ni Hadiyth Swahiyh imetajwa katika ”as-Silsilah as-Swahiyhah” (605) na ”Swahiyh Abiy Daawuud” (1732).

[15] Shaykh-ul-Islaam amesema:

“Haifai kwa mwanamke kupunguza zaidi ya ncha za vidole. Ama kuhusu mwanamume anaruhusiwa kupunguza kiasi anachotaka.”

[16] Ameipokea al-Bukhaariy na Abu Daawuud kutoka kwa kundi la Maswahabah. Tazama ”Swahiyh Abiy Daawuud” (1700, 1707, 1709 na 1710) na ”Mukhtaswar al-Bukhaariy” (847).

[17] Ameipokea Abu Daawuud na wengineo. Tazama ”Swahiyh Abiy Daawuud” (1710).

[18] Ameipokea Abu Daawuud na wengineo. Tazama ”Swahiyh Abiy Daawuud” (1709).

[19] Ameipokea al-Bukhaariy kwa cheni ya wapokezi pungufu wakati Abu Daawuud ameipokea kwa cheni ya wapokezi ilioungana. Tazama ”Swahiyh Abiy Daawuud” (1700) na ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (1064).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manaasik-ul-Hajj wal-´Umrah, uk. 33-35
  • Imechapishwa: 19/07/2018