Pamoja na misingi hii ambayo tumetangulia kuitaja wanasifika kwa sifa kubwa ambazo zinakamilisha ´Aqiydah. Miongoni mwa sifa hizo kuu ni zifuatazo:

1 – Wanaamrisha mema na kukataza maovu kwa mujibu wa Shari´ah. Amesema (Ta´ala):

كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ

“Mmekuwa Ummah bora kabisa ulioteuliwa kwa watu – mnaamrisha mema na mnakataza maovu na mnamwamini Allaah.”[1]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayeona maovu katika nyinyi basi ayaondoshe kwa mkono wake, asipoweza [ayaondoshe] kwa ulimi wake, asipoweza [ayaondoshe] kwa moyo wake – na hiyo ni imani dhaifu kabisa.”[2]

Tumesema kwa mujibu wa Shari´ah tofauti na wanavyofanya Mu´tazilah ambapo wanafanya uasi kwa jina la kuamrisha mema na kukataza maovu. Wanaona kuamrisha mema na kukataza maovu ni kuwafanyia uasi watawala wa waislamu pindi watapofanya maasi hata kama yatakuwa ni chini ya kufuru.

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaonelea kuwanasihi katika hayo bila ya kufanya uasi dhidi yao. Hilo ni kwa sababu ya kuleta umoja na kuepuka mfarakano na tofauti. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Pengine inakaribia kutokujulikana kuwepo kundi lililofanya uasi dhidi ya mtawala isipokuwa katika kufanya uasi huo kulitokea ufisadi mwingi zaidi kuliko ule ulioondoshwa.”[3]

2 – Miongoni mwa sifa za Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kuhifadhi kusimamisha desturi za Kiislamu kukiwemo swalah ya ijumaa na ya mkusanyiko tofauti na wanavyofanya wazushi na wanafiki ambao hawasimamishi ijumaa wala swalah za mikusanyiko.

3 – Katika sifa zao ni kuwanasihi waislamu wote na kusaidiana katika wema na kumcha Allaah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Dini ni kupeana nasaha.” Tukasema: “Ni kwa nani?” Akasema: “Ni kwa Allaah, Kitabu Chake, Mtume Wake, viongozi wa waislamu na watu wa kawaida.”[4]

“Waumini ni kama jengo; upande mmoja unaupa nguvu upande mwingine.”[5]

4 – Miongoni mwa sifa zao ni kuwa na uimara katika hali za mitihani. Hilo linakuwa kwa kuwa na subira wakati wa majaribio, kushukuru katika kipindi cha raha na kuridhia kunapopita makadirio yenye kuumiza.

5 – Katika sifa zao ni wenye kupambika na tabia njema, matendo mazuri, kuwatendea wema wazazi, kuwaunga ndugu na kujenga ujirani mwema. Vilevile wanakataza majivuno, kiburi, mashambulizi, dhuluma na kujinyanyua mbele za watu. Amesema (Ta´ala):

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا وَبِذِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينِ وَالْجَارِ ذِي الْقُرْبَىٰ وَالْجَارِ الْجُنُبِ وَالصَّاحِبِ بِالْجَنبِ وَابْنِ السَّبِيلِ وَمَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ مَن كَانَ مُخْتَالًا فَخُورًا

“Mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote na wafanyieni wazazi wawili wema na jamaa wa karibu na mayatima na masikini na majirani wa karibu na majirani walio mbali na rafiki wa ubavuni na msafiri na wale iliyowamilikimikono yenu ya kulia. Hakika Allaah hapendi mwenye majivuno mwenye kujifakharisha.”[6]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Muumini mwenye imani kamili zaidi ni yule mwenye tabia njema.”[7]

Tunamuomba Allaah (´Azza wa Jall) kwa neema na fadhilah Zake atufanye kuwa katika wao na asizipotoshe nyoyo zetu baada ya kutuongoza.

Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, familia yake na Maswahabah zake wote.

[1] 03:110

[2] Muslim (49), at-Tirmidhiy (2172), an-Nasaa´iy (5009), Abu Daawuud (1140), Ibn Maajah (4013) na Ahmad (03/10)

[3] Majmuu´-ul-Fataawaa (28/179-180)

[4] Muslim (55), an-Nasaa´iy (4197), Abu Daawuud (4944) na Ahmad (04/102)

[5] al-Bukhaariy (467), Muslim (2585), at-Tirmidhiy (1968), an-Nasaa´iy (2560) na Ahmad (04/405)

[6] 04:36

[7] Abu Daawuud (4684), at-Tirmidhiy (1162) na Ahmad (02/250)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Usuwl ´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 42-46
  • Imechapishwa: 13/05/2022