Hii ndio jumla ya ´Aqiydah ya Salaf na Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Tunamuomba Allaah atujaalie sote kwa fadhilah na ukarimu Wake kuwa katika wao. Tunamuomba aturuzuku kushikamana na haki, kuwa na subira juu yake na kuwa na uimara juu yake mpaka siku tutakutana Naye.

Ambaye anashikamana barabara na ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah anakuwa juu ya elimu na uongofu. Vilevile ukiongezea juu ya hayo ni kwamba moyo wake unakuwa na utulivu na uthabiti. Hilo si kwa jengine isipokuwa ni kwa sababu ameishi juu ya Qur-aan na Sunnah na pia juu ya dalili ya wazi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake. Kwa ajili hiyo ndio maana anakuwa na utulivu na uthabiti juu ya jambo la dini yake. Mtu kama huyu hupata mambo mazuri, uthabiti na sifa za kipekee kuu ambazo hawazipati wale wengine waliopinda. Watu kama hawa wanakuwa katika dhiki siku zote popote pale wanapokwenda. Kuhusu Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wako imara juu ya haki. Hawateteleki. Hawazui matamanio, maoni na tofauti kutoka kwao. Hili si kwa jengine ni kwa sababu mfumo na njia yao ni moja.

Allaah amewaahidi heshima, Pepo, kudumu ndani ya Nyumba yenye neema zisizoisha wale wenye kushikamana na ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Amesema (Ta´ala):

فَإِمَّا يَأْتِيَنَّكُم مِّنِّي هُدًى فَمَنِ اتَّبَعَ هُدَايَ فَلَا يَضِلُّ وَلَا يَشْقَىٰ

“Utakapokufikieni kutoka Kwangu mwongozo, basi atakayefuata mwongozo Wangu hatopotea na wala hatotaabika.”[1]

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Allaah amemuahidi yule mwenye kusoma Qur-aan na kutendea kazi yale yaliyomo ndani yake kutompoteza duniani na wala hatotaabika huko Aakhirah.”

Amesema (Ta´ala):

الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُم مُّهْتَدُونَ

“Wale walioamini na hawakuchanganya imani zao na dhulma, hao ndio watakaopata amani nao ndio walioongoka.”[2]

Huko Aakhirah watasalimika kutokana na adhabu na ndio walioongoka duniani kutokana na upotevu. Duniani wameongoka pasi na kupotea na kupoteza. Vilevile huko Aakhirah watakuwa na amani na usalama. Hiyo ni siku ambayo watu watakuwa na khofu, watakuwa na mfazaiko na nyoyo zitapigwa na bumbuwazi. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na Ahl-ul-Haqq watakuwa katika amani. Amesema (Ta´ala):

لَا يَحْزُنُهُمُ الْفَزَعُ الْأَكْبَرُ وَتَتَلَقَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ هَـٰذَا يَوْمُكُمُ الَّذِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ

“Haitowahuzunisha mfazaiko mkubwa na Malaika watawapokea [na huku wakiwaambia]: “Hii ni ile siku yenu mliyokuwa mkiahidiwa.””[3]

إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ نَحْنُ أَوْلِيَاؤُكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَشْتَهِي أَنفُسُكُمْ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَدَّعُونَ نُزُلًا مِّنْ غَفُورٍ رَّحِيمٍ

“Hakika wale waliosema: “Mola wetu ni Allaah” kisha wakathibitika imara, Malaika huwateremkia [wanapofishwa kuwaambia]: “Msikhofu na wala msihuzunike na pokeeni bishara njema ya Pepo ambayo mlikuwa mkiahidiwa. Sisi ni wapenzi wenu katika uhai wa dunia na Aakhirah na mtapata humo yale yanayotamani nafsi zenu na mtapata humo yale mtakayoomba – ni takrima kutoka kwa Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.””[4]

Haya ndio matunda ya kuwa na ´Aqiydah sahihi duniani na Aakhirah. Amesema (Ta´ala):

مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً ۖوَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Mwenye kutenda mema miongoni mwa wanamume au wanawake naye ni muumini, Tutamhuisha maisha mazuri na bila shaka tutawalipa ujira wao kwa mazuri zaidi ya yale waliyokuwa wakitenda.”[5]

Hizi ni dhamana kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na Ahl-ul-Haqq. Si kwa jengine ni kwa sababu wako katika kheri duniani na Aakhirah.

Tunamuomba Allaah sote kwa fadhilah na ukarimu Wake atujaalie kuwa katika wao. Tunamuomba (Subhaanah) atuonyeshe haki kuwa ni haki na atujaalie kuweza kuifuata na atuonyeshe batili kuwa ni batili na atujaalie kuweza kuiepuka.

Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, familia yake na Maswahabah zake wote.

[1] 20:123

[2] 06:82

[3] 21:103

[4] 41:30-32

[5] 16:97

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mujmal ´Aqiydat-is-Salaf as-Swaalih, uk. 16-18
  • Imechapishwa: 24/05/2022