19. Fanya kazi ujitafutie riziki yako


90- Huenda mtu akafikiria ya kwamba mtu akifanya kazi ili aweze kupata riziki basi ngazi yake inashuka. Sivyo kabisa. Kufanya sababu hakupingani na kumtegemea Allaah. Mitume na watu wema walikuwa wakifanya kazi ili waweze kupata riziki.

91- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Bora ambacho mtu anakula ni kile kinachotokamana na kazi ya mkono wake. Mtume wa Allaah Daawuud alikuwa akila kwa kazi ya mkono wake.”[1]

92- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Riziki yangu inatoka chini ya kivuli cha mkuki wangu, yule mwenye kwenda kinyume na amri yangu basi atakuja kudhalilika na kufedheheka na yule mwenye kujifananisha na watu ni katika wao.”[2]

Allaah (Ta´ala) alikuwa akimruzuku Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa riziki ilio bora kabisa. Alikuwa akihifadhi malighafi kwa ajili ya familia yake kwa mwaka mzima. Wakati Salmaan al-Faarisiy aliponunua kiasi kikubwa ya chakula akamuuliza juu yake ambapo akajibu kwa kusema:

“Mtu anakuwa na utulivu pindi kunakuwa chakula cha kutosha.”

93- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Ndugu zetu katika Muhaajiruun walikuwa ni wenye kushughulishwa na kuyatembelea masoko wakati ndugu zetu katika Answaar walikuwa ni wenye kushughulishwa na kuziangalia mali zao.”[3]

94- Sahl bin ´Abdillaah amesema:

“Yule mwenye kutukana kazi basi ameitukana imani.”

95- al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw amesema:

“Lau kweli mtu angelimgemea Allaah na kwamba atamruzuku mtu, basi Allaah angelifanya yote. Lakini hivyo hawakufanya Mitume na watu wema. Walikuwa wakijikodesha wao wenyewe kwa ajili ya kazi na hawakai chini na huku wakisubiri riziki.”

96- Allaah (Ta´ala) amesema:

وَابْتَغُوا مِن فَضْلِ اللَّـهِ

“Na tafuteni katika fadhila za Allaah.” (62:10)

Ni lazima kwa mtu kutafuta riziki. Haiwezekani kusema kuwa Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) wametumwa tu ili kuwajengea njia madhaifu. Hakuna wenye kusema hivi isipokuwa wajinga na wapumbavu au wenye kuitukana Qur-aan na Sunnah.

97- Allaah (Ta´ala) ameeleza katika Kitabu Chake jinsi Mitume Wake wateuzi na Manabii walivyokuwa wakifanya kazi na walikuwa na kazi. Amesema:

وَعَلَّمْنَاهُ صَنْعَةَ لَبُوسٍ لَّكُمْ لِتُحْصِنَكُم مِّن بَأْسِكُمْ

“Tukamfunza uundaji wa mavazi ya vita kwa ajili yenu ili yakuhifadhini katika mapigano yenu.” (21:80)

وَمَا أَرْسَلْنَا قَبْلَكَ مِنَ الْمُرْسَلِينَ إِلَّا إِنَّهُمْ لَيَأْكُلُونَ الطَّعَامَ وَيَمْشُونَ فِي الْأَسْوَاقِ

“Na Hatukupeleka kabla yako Mtume yeyote isipokuwa bila shaka walikuwa wanakula chakula na wanatembea masokoni.” (25:20)

Wanachuoni wamesema kuwa maana yake ni kwamba walikuwa ni wafanya kazi na watu wa biashara. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَكُلُوا مِمَّا غَنِمْتُمْ حَلَالًا طَيِّبًا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ

“Kuleni katika mlivyopata ngawira vilivyo vya halali vizuri na mcheni Allaah.” (08:69)

98- Maswahabah walikuwa ni wafanya biashara na wafanya kazi na wakifanya kazi kwa mali zao pamoja na kupambana na makafiri wenye kwenda kutofautiana na wao. Unaona kuwa walikuwa madhaifu? Ninaapa kwa Allaah kwamba walikuwa ni wenye nguvu. Vizazi vyema baada yao vilifuata nyayo zao na uongofu wao.

99- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Lau mngelikuwa mnamtegemea Allaah ukweli wa kumtegemea, basi angekuruzukuni kama anavyowaruzuku ndege. Wanaruka hali ya kuwa hawana kitu tumboni na wanarudi matumbo yamejaa.”[4]

Ndege inaruka asubuhi kutafuta chakula. Haidemi isipokuwa pale inapoona chakula. Inaruka na kuruka mpaka inaona maji na kudema karibu na maji hayo. Inafanya yote hayo ili kujipatia riziki. Kule kuruka kwake na kurudi ni sababu. Ni jambo la kustaajabisha sana kuona jinsi baadhi ya watu wanasema kuwa wanamtegemea Allaah kisha wanakaa tu na kuacha njia iliyonyooka na mfumo wa wazi.

100- Imethibiti katika al-Bukhaariy ya kwamba Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Wayemen walikuwa wakienda kuhiji bila ya kupeleka akiba ya chakula. Wanasema kuwa wanamtegemea Allaah. Wanapofika wanaanza kuwaomba watu. Ndipo Allaah akateremsha:

وَتَزَوَّدُوا

“Na chukueni masurufu.” (02:197)

Nimefafanua hili zaidi katika kitabu “al-Jaami´ li Ahkaam-il-Qur-aan.” Haikupokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala kutoka kwa Swahabah yoyote ya kwamba walisafiri bila ya kuwa na akiba ya chakula. Walikuwa wakimtegemea Allaah vile inavyopaswa. Uhakika wa kutegemea ni moyo ufungamane na Allaah na wakati huo huo mtu akatumia njia mbali mbali. Hii ndio haki.

101- Kuna mtu alimwambia Imaam Ahmad bin Hanbal kwamba anafikiri kwenda kuhiji na kumtegemea Allaah. Imaam Ahmad akamwambia:

“Basi toka peke yako.” Mtu yule akasema: “Hapana, nataka kusafiri pamoja na wengine.” Ndipo Imam Ahmad akamwambia: “Basi unawategemea watu.”

Imaam Ahmad (Radhiya Allaahu ´anh) amesema kweli. Ikiwa mtu anamtegemea Allaah (Subhaanah) kweli kweli na anaamini kuwa Atamruzuku bila ya kupeleka chochote na anaona kuwa riziki inamshughulisha na ´ibaadah, asafiri hali ya kuwa peke yake na Allaah atamruzuku. Ama akiwa ni mdhaifu na anachelea juu yake, ni wajibu kwake kwenda na akiba ya chakula.

102- ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Enyi vijana! Unueni vichwa vyenu! Njia iko wazi. Yule asiyefanya kazi katika nyinyi basi tunamtuhumu na yule mwenye kufanya kazi katika nyinyi tunamsifu.”

103- al-Hajjaaj bin al-Minhaal amesema:

“Nilikuwa natembea na Hammaad bin Salamah kwa ajili ya haja. Alipopita pembezoni mwa mlango wa mfalme akasimama, akashika ndevu na kusema: “Himdi zote ni za Allaah ambaye ametuonyesha njia ya kwenda sokoni na kututosheleza na milango ya watu hawa.”

104- al-Hajjaaj amesema:

“Hammaad bin Salamah alikuwa akienda sokoni na kukaa mpaka achume dirhamu mia moja. Kisha baada ya hapo anaondoka na kusema: “Kiwango hichi kinanitosheleza. Hii ni riziki yangu na riziki ya familia yangu.”

105- Sufyaan amesema:

“Marafiki zetu walijifedhehesha pale walipokuwa ni wenye kuhitajia.”

106- Sufyaan amesema:

“Ikiwa mwanachuoni hawezi kujihudumia ndipo huanza kuwategemea madhalimu. Na mfanya ´ibaadah ikiwa hawezi kujihudumia ndipo huanza kula katika pato la dini yake.”

[1] al-Bukhaariy (2072), Ahmad (4/131) na at-Twabaraaniy (20/631).

[2] Ahmad (3/50).

[3] al-Bukhaariy (1/40).

[4] at-Tirmidhiy (2344).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 67-72
  • Imechapishwa: 18/03/2017