19. ´Aqiydah ya Qadariyyah na Jabriyyah

Qadariyyah wanasema kuwa matendo ya waja hayakuumbwa na Allaah na kwamba wanayafanya mbali na utashi wa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Hii ina maana ya kwamba Allaah ana washirika wanaofanya mambo Asiyoyataka.

Hakuna kinachopitika katika ulimwengu huu isipokuwa kile Allaah alichokitaka. Hii ni milki Yake. Waja wakifanya kitu basi Allaah ndiye kaumba matendo yao:

وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ وَمَا تَعْمَلُونَ

“Allaah ndiye kakuumbeni na yale mnayoyatenda.” 37:96

اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ

“Allaah ndiye Muumbaji wa kila kitu.” 13:16

Maneno, matendo, miili na vingine vyote vimeumbwa na Allaah. Waja wanafanya matendo yao kwa khiyari yao, uwezo wao na matakwa yao. Kwa ajili hiyo ndio maana wataulizwa juu ya matendo yao.

Wapinzani wa Qadariyyah ni Jabriyyah. Wanasema kuwa waja hawafanyi kitu na kwamba uhalisia wa mambo si wao wenye kutenda. Allaah ndiye mwenye kufanya kila kitu na matendo yao kwa hakika ni matendo ya Allaah. Wametenzwa nguvu juu ya matendo yao. Majini na watu hawana utashi wala khiyari. Wametenzwa nguvu. Kutikisika kwao ni kama kutikisika kwa majani ambayo yanatikiswa na upepo.

Huu ni uongo unaopingana na ukweli wa mambo. Kitendo cha kulazimishwa kinatofautiana kabisa na kitendo cha khiyari. Watu wote, hata wanyama, wanatofautisha kati ya matendo ya khiyari na matendo waliyolazimishwa. Pindi unapoirushia mbwa jiwe hailikimbizi jiwe lile kuliuma; bali itakukimbiza wewe. Kwa nini? Kwa sababu inajua kuwa jiwe halina khiyari yoyote. Inajua kuwa wewe ndiye umeirushia jiwe kwa khiyari na kwa kusudi. Wanyama wote wako namna hiyo. Watu wote wako namna hiyo.

Pindi mmoja katika watu hawa anapofanya madhambi analaumu makadirio na matakwa ya Allaah. Lakini watakuacha iwapo utaenda kuchukua mali yao? Ukiwapiga watakuacha? Hapana. Watakabiliana na wewe na kukupeleka mahakamani. Ni wenye kujigonga. Kujigonga kwao kunathibitisha kuwa ´Aqiydah yao ni batili.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qurrat-ul-´Aynayn bi Tawdhwiyh Ma´aaniy ´Aqiydat-ir-Raaziyayn, uk. 30-31
  • Imechapishwa: 15/10/2016