Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Maana ya waniabudu ni wanipwekeshe.

MAELEZO

Tambua kwamba kuna aina mbili ya ´ibaadah:

1- ´Ibaadah ya kilimwengu. Aina hii maana yake ni kule kunyenyekea maamrisho ya Allaah ya kilimwengu na hii imeenea kwa viumbe wote pasi na yeyote kutoka ndani yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِن كُلُّ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ إِلَّا آتِي الرَّحْمَـٰنِ عَبْدًا

“Hakuna yeyote yule katika mbingu na ardhi isipokuwa atamfikia Mwingi wa rehema hali ya kuwa mja.” (Maryam 19 : 93)

Hii imemuenea muumini na kafiri, mwema na muovu.

2- ´Ibaadah ya Kishari´ah. Aina hii maana yake ni kule kunyenyekea kwa maamrisho Allaah (Ta´ala) ya Kishari´ah. ´Ibaadah hii ni maalum kwa yule anayemtii Allaah (Ta´ala) na akafuata yale waliyokuja nayo Mitume. Mfano wa hii ni maneno Yake (Ta´ala):

وَعِبَادُ الرَّحْمَـٰنِ الَّذِينَ يَمْشُونَ عَلَى الْأَرْضِ هَوْنًا

“Waja wa Mwingi wa rehema ni wale wanaotembea katika ardhi kwa unyenyekevu.” (al-Furqaan 25 : 63)

Aina ya kwanza mtu hasifiwi kwayo, kwa sababu mja hafanyi kwa kutaka kwake mwenyewe. Lakini huenda akasifiwa akionyesha shukurani wakati wa kipindi kizuri na kusubiri wakati wa majanga. Tofauti na aina ya pili, mtu anasifiwa kwayo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 39
  • Imechapishwa: 19/05/2020