Allaah (Ta´ala) amesema:

فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ

Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi ili wapate kuongoka.”[1]

Hii ni dalili inayofahamisha kuwa Allaah anatuitikia tukimuitikia Yeye. Ni kama maneno ya Allaah (Ta´ala):

إِن تَنصُرُوا اللَّـهَ يَنصُرْكُمْ

“Mkimnusuru [dini ya] Allaah Naye Atakunusuruni.”[2]

Na hapa Allaah anasema:

فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ

Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi ili wapate kuongoka.”[3]

Hii ina maana kwamba endapo mja atamuitikia na kumuomba Mola wake, basi ni sababu ya yeye kuongozwa. Moja katika sababu ya uongofu ni wewe kuwa umeongozwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَالَّذِينَ اهْتَدَوْا زَادَهُمْ هُدًى وَآتَاهُمْ تَقْوَاهُمْ

“… na wale walioongoka, Anawazidishia uongofu na kuuongeza uchaji wao.[4]

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْفَاسِقِينَ

“Hakika Allaah hawaongozi watu mafasiki.”[5]

Ni vipi mtenda dhambi atatarajia Allaah amwongoze ikiwa atafanya uzinzi, kunywa pombe, kula ribaa na kula mali ya haramu? Hilo ni jambo halitotokea isipokuwa ikiwa kama Allaah atamwongoza katika wema, maombi na unyenyekevu. Pindi anapomwita katika jambo la kheri, basi analikimbilia. Pindi anapomtahadharisha na jambo la shari, anajiepusha nalo. Huyu ndiye ambaye anatarajia Allaah kumwongoza.

Hata hivyo hatutakiwi kumfanya yule mtu wa pili kukata matumaini na huruma ya Allaah. Badala yake tunatakiwa kumkumbusha atubie kwa Allaah ili Allaah amsamehe, amwongoze katika yale anayoyapenda na kuyaridhia na amfanye kuyamaliza maisha yake kwa uzuri. Ama kuendelea kuyashikilia madhambi yake na machafu na kutarajia kuyapata yale watayoyapata waongofu na wachaji Allaah ni matumaini ya kipumbavu na ya batili.

[1] 02:186

[2] 47:07

[3] 02:186

[4] 47:17

[5] 63:06

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tafsiyr Aayaat-is-Swiyaam, uk. 32-34
  • Imechapishwa: 02/06/2017