Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

13- Muumbaji asiyekuwa na haja, mtoaji riziki bila matatizo.

MAELEZO

Muumbaji asiyekuwa na haja. Yeye ndiye ambaye kawaumba viumbe ili wamwabudu:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ مَا أُرِيدُ مِنْهُم مِّن رِّزْقٍ وَمَا أُرِيدُ أَن يُطْعِمُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu. Sitaki kutoka kwao riziki yoyote na wala sitaki wanilishe.”[1]

Amewaumba sio kwa sababu ni Mwenye kuwahitaji wamsaidie au wamnusuru. Amewaumba ili wamwabudu Yeye. Viumbe ndio wenye kuhitajia ´ibaadah. Kupitia ´ibaadah ndio inawafungamanisha na Allaah. ´Ibaadah ndio mafungamano kati ya mja na Mola wake. Kupitia ´ibaadah ndio kunamkurubisha mtu mbele ya Allaah na Allaah anamlipa thawabu mtu huyo. Kwa hivyo viumbe ndio wenye kuhitajia ´ibaadah, na si Allaah (´Azza wa Jall):

وَقَالَ مُوسَىٰ إِن تَكْفُرُوا أَنتُمْ وَمَن فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا فَإِنَّ اللَّـهَ لَغَنِيٌّ حَمِيدٌ

“Muusa akasema: “Mkikufuru nyinyi na wote walioko ardhini, basi hakika Allaah ni mkwasi, Mwenye kustahiki kuhimidiwa.”[2]

إِن تَكْفُرُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنكُمْ ۖ وَلَا يَرْضَىٰ لِعِبَادِهِ الْكُفْرَ ۖ وَإِن تَشْكُرُوا يَرْضَهُ لَكُمْ

“Mkikufuru, basi hakika Allaah ni mkwasi kwenu na wala haridhii kwa waja Wake kufuru na mkishukuru huridhika nanyi.”[3]

Yeye ndiye Mwenye kusimamia ruzuku za waja Wake pasi na kupungua chochote katika vile anavyomiliki.

[1] 51:56-57

[2] 14:08

[3] 39:07

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 39
  • Imechapishwa: 16/09/2019