18. Sababu ya kujifunza vitenguzi vya Uislamu

Wao wanaosema “ni kwa nini mnasoma Tawhiyd na mnasoma shirki ilihali nyinyi ni watoto wa ´Aqiydah, watu wa maumbile na mko katika nchi ya Tawhiyd?” Wanaonelea kuwa hakuna haja ya kusoma Tawhiyd na kuzijua aina za shirki. Vilevile wanaonelea kuwa hakuna haja ya kuweka vitabu vya ´Aqiydah na kuwafunza watoto mambo haya katika silebasi za masomo. Wao wanaona kuwa watu hawana haja ya kujua shubuha, madhehebu ya watu waliopinda na upotevu wao. Wanaona kuwa watu hawana haja ya mambo haya. Huku ni kughurika, ujinga au upotevu.

Ni wajibu kwa mtu ayajue mambo haya ili aweze kusalimika na shari zake na fitina zake. Huwezi kukiepuka kitu ilihali hukijui. Huwezi kuijua haki na wewe huijui. Kwa sababu unaweza kuitakidi haki kuwa batili na batili kuwa ndio haki na wewe hujui. Hili ni jambo muhimu sana.

Wanasema kuwa sisi tunawakufurisha watu. Wanauliza ni kwa nini tunadhihirisha mambo haya? Tunawajibu kwa kusema: sisi hatuwakufurishi watu isipokuwa yule aliyekufurishwa na Allaah na Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini hata hivyo tunachelea juu ya nafsi zetu na wala hatuzitakasi nafsi zetu. Kwa ajili hiyo tunachukua zile sababu za kuokoka, tunawatahadharisha watu na kuwanasihi.

Jengine ni kwamba tunajifunza mambo haya ili tuwabainishie watu na tulinganie kwa Allaah kwa ujuzi. Lengo ni ili tusalimike sisi na Allaah asalimishe kupitia mikono yetu wale awatakao katika waja Wake. Uhakika wa mambo ni kwamba jambo ni la khatari sana.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 38-39
  • Imechapishwa: 26/06/2018