18. Njia ya tisa: kuchagua rafiki mzuri mwenye bidii

Miongoni mwa njia za kujifunza elimu ni mwanafunzi achague rafiki mzuri ambaye ana hamu kubwa ya kusoma. Mwanafunzi! Unapotaka kuchagua rafiki, basi chagua rafiki mzuri aliye na hamu kubwa ya kusoma ambaye atakuvutia na wewe kusoma na hatokurudisha kutafuta dunia. Mwanafunzi ambaye atakufanya kukimbilia katika mizunguko ya kielimu na hatokutia uvivu. Hakika rafiki anaathiri. Rafiki ni lazima amuathiri mwenzake. Kwa ajili hii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mfano wa rafiki mzuri na rafiki muovu ni kama muuza manukato na muhunzi. Muuza manukato ima atakupa au utapata kutoka kwake harufu nzuri. Kuhusu muhunzi ima ataunguza nguo yako au utapata harufu mbaya kutoka kwake.”[1]

Mwanafunzi atapochagua rafiki mzuri mwenye hima kubwa ima akampa zawadi, akamzidishia elimu, akampa faida mbalimbali, akampeleka katika vikao vyema, akampeleka katika vikao vya wanachuoni au akajipamba kwa tabia zake. Hatimae utamuona na yeye ni mwenye bidii kubwa katika kusoma na kheri kubwa. Upande mwingine mwanafunzi akichagua rafiki ambaye ana hima zilizo chini kuliko yeye na mwema kidogo kuliko yeye, hakika hilo huenda lisimfikishe kwenye malengo. Huenda akamfanya kuiona mizunguko ya kielimu kuwa mizito na akamwambia: “Lau tutafanya kitu fulani itakuwa ni bora zaidi”. Ni wanafunzi wangapi mnaowajua ambao walikuwa na bidii katika kuhudhuria mizunguko ya kielimu, lakini pindi walipoanza kuchukua marafiki wavivu ndipo wakaanza kuacha elimu sehemu baada ya sehemu.

[1] al-Bukhaariy (5534) na Muslim (2628)

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Ilm wa Wasaaailuh wa Thimaaruh
  • Imechapishwa: 22/10/2016