18. Njia ya pili namna inavyothibiti Ramadhaan


2- Miongoni mwa mambo ambayo kunahukumiwa kuwa mwezi umeingia ni kukamilisha mwezi wa kabla yake siku thelathini. Kwa sababu mwezi wa kimwezi hauwezi kuzidi siku thelathini kama ambavo hauwezi kupungua siku ishirini na tisa. Wakati fulani miezi miwili, mitatu mpaka mine ikafululiza siku thelathini. Au miezi miwili, mitatu mpaka mine ikafululiza siku ishirini na tisa. Lakini mara nyingi ni kwamba mwezi mmoja au miezi miwili inakuwa kamilifu na mwezi wa tatu unakuwa mpungufu. Pale ambapo mwezi uliotangulia utakamilisha siku thelathini basi kwa mujibu wa Shari´ah kutahukumiwa kwamba mwezi ulio baada yake umeingia ingawa mwezi mwandamo hautoonekana. Hilo ni kutokana na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Fungeni kwa kuona mwezi na fungueni kwa kuona mwezi. Mkifunikwa na mawingu basi hesabieni thelathini.”

Ameipokea Muslim na al-Bukhaariy kwa tamko:

“Mkifunikwa na mawingu basi kamilisheni Sha´baan kwa idadi ya thelathini.”

Katika “as-Swahiyh” ya Ibn Khuzaymah kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiichunga Sha´baan kiasi ambacho hachungi wakati mwingine kisha anafunga kwa kuuona mwezi mwandamo wa Ramadhaan. Akifunikwa na mawingu basi anahesabu siku thelathini kisha anafunga.”

Imepokelewa vilevile na Abu Daawuud na ad-Daraaqutwniy ambaye ameisahihisha.

Kutokana na Hadiyth hii kumebaini kuwa Ramadhaan haifungwi kabla ya kuona mwezi mwandamo. Usipoonekana mwezi mwandamo basi Sha´baan itakamilishwa siku thelathini. Haifai kufunga siku hiyo ya thelathini. Ni mamoja siku hiyo haina mawingu au ni yenye mawingu. Hayo ni kutokana na maneno ya ´Ammaar bin Yaasir (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Mwenye kufunga siku yenye kutiliwa shaka basi amemuasi Abul-Qaasim (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Ameipokea Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa´iy na al-Bukhaariy ameipokea hali ya kuiwekea taaliki.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 22-24
  • Imechapishwa: 10/04/2020