Swali 18: Ni upi mfumo mzuri wa nasaha na khaswa kuwanasihi watawala? Je, makosa yao yaanikwe juu ya minbari? Wanasihiwe kwa siri?

Jibu: Hakuna yeyote aliyekingwa na kukosea isipokuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Watawala wa waislamu ni watu wa kawaida wenye kukosea. Ni jambo lisilokuwa na shaka ya kwamba wanakosea na hawakukingwa na kukosea. Lakini hata hivyo haitakikani kutumia fursa ya makosa yao ili kuwakashifu na kuacha kuwatii hata kama watakuwa wenye kukandamiza, wenye kudhulumu na kufanya madhambi muda wa kuwa sio kufuru ya wazi[1]. Haya ni maamrisho ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[2]. Haijalishi kitu hata kama wanatenda madhambi, wanakandamiza na wanadhulumu. Hakika kuwa na subira katika kuwatii[3] ndio kunawafanya waislamu kuwa na umoja na kuilinda miji ya waislamu. Kuwaasi na kukinzana nao kunapelekea katika madhara makubwa[4]; kun madhara makubwa zaidi ya dhambi za mtawala muda wa kuwa maovu haya sio kufuru na shirki.

Hatusemi kuwa makosa ya mtawala yanatakiwa kunyamaziwa. Yanatakiwa kutatuliwa, lakini kwa njia sahihi. Wanatakiwa kunasihiwa kwa siri. Wanatakiwa kuandikiwa barua kwa siri[5]. Haitakiwi kuwa barua ambayo inapigwa muhuri na watu wengi kisha inatawanywa kati ya watu. Hili halijuzu. Nasaha inatakiwa kuandikwa kwa siri halafu ndio itumwe kwa mtawala. Njia nyingine ni mtu kuzungumza naye moja kwa moja. Ama kuandika, kukopi na kugawanywa kwa watu ni jambo lisilojuzu. Huku ni kukashifu bali ni kubaya zaidi kuliko kuzungumza juu ya minbari. Maneno yanaweza kusahauliwa, lakini uandishi unabaki na kuzunguka kwa watu. Hili si sawa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Dini ni kupeana nasaha.” Tukasema: ”Kwa nani, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: ”Kwa Allaah, Kitabu Chake, Mtume Wake, viongozi wa waislamu na watu wao wa kawaida.”[6]

Katika Hadiyth nyingine imekuja:

“Hakika Allaah anaridhia kwenu mambo matatu: mumuabudu na wala msimshirikishe na chochote, mshikamane na kamba ya Allaah nyote na wala msifarakane na muwanasihi wale ambao Allaah amewafanya kukutawalini.”[7]

Watu wenye haki zaidi ya kuwanasihi watawala ni wanazuoni na watu wenye ushawishi. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَإِذَا جَاءَهُمْ أَمْرٌ مِّنَ الْأَمْنِ أَوِ الْخَوْفِ أَذَاعُوا بِهِ ۖ وَلَوْ رَدُّوهُ إِلَى الرَّسُولِ وَإِلَىٰ أُولِي الْأَمْرِ مِنْهُمْ لَعَلِمَهُ الَّذِينَ يَسْتَنبِطُونَهُ مِنْهُمْ وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ لَاتَّبَعْتُمُ الشَّيْطَانَ إِلَّا قَلِيلًا

“Linapowafikia jambo lolote la amani au la khofu huharakia kulitangaza. Na lau wangelirudisha kwa Mtume na kwa wale wenye madaraka kati yao, basi wale wanaotafiti miongoni mwao wangelilijua. Lau si fadhilah za Allaah juu yenu na rehema Zake, basi hakika mngelimfuata shaytwaan isipokuwa wachache tu.” [8]

Si kila mmoja jambo hili linampasa. Usambazaji wa makosa na kashfa sio nasaha kabisa. Bali ni jambo linaloeneza maovu na machafu kati ya wale waumini. Haikuwa katika mfumo wa Salaf. Haijalishi kitu hata kama mwenye kufanya hivyo malengo yake ni mazuri na anachotaka yeye tu ni kukemea yale anayodai kuwa ni maovu. Aliyofanya ni maovu zaidi kuliko maovu anayokataza. Kukataza maovu kunaweza kuwa maovu kwa dhati yake ikiwa kunaenda kinyume na njia iliyowekwa na Shari´ah na Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu hakufuata njia aliyoweka Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote yule mwenye kuona maovu, basi ayabadilishe kwa mkono wake. Ikiwa hawezi, ayabadilishe kwa mdomo wake. Ikiwa hawezi, ayabadilishe kwa moyo wake – na hiyo ni imani dhaifu.”[9]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewagawanya watu katika makundi matatu:

1 – Mtu ambaye anaweza kuyaondosha maovu kwa mkono wake. Ni mtawala, naibu wake katika makamati, wakuu na viongozi.

2 – Mwanachuoni asiyekuwa na utawala. Abainishe na kunasihi na kuwafikishia wenye mamlaka kwa hekima na mawaidha mazuri.

3 – Mtu asiyekuwana elimu wala utawala. Mtu huyu anatakiwa kuyakataza maovu kwa moyo wake, kuchukia madhambi na watenda madhambi na kuwaepuka.

[1] Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah inapokuja kwa watawala waislamu. at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hatuonelei kufanya uasi kwa viongozi na watawala wetu hata kama watadhulumu. Hatuombi du´aa dhidi yao. Hatuwaasi. Tunaonelea kuwatii ni katika utiifu wa faradhi kwa Allaah (´Azza wa Jall) muda wa kuwa hawatuamrishi maasi. Tunawaombea kutengemaa na mafanikio. Tunafuata Sunnah na mkusanyiko na tunajiepusha na upindaji, mpasuko na mfarakano.” (al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 379)

Haya ndio ambayo walinganizi wa haki wanafuata mpaka hii leo. Maneno haya na mfano wake yanakariri mara nyingi katika darsa na mihadhara ya Shaykh wetu ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz (Rahimahu Allaah). Tazama vitabu ”al-Ma´luum min Waajib-il-´Ilaaqah bayn al-Haakim wal-Mahkuum” na ”Naswiyhat-ul-Ummah fiy Jawaab ´Asharah As-ilah Muhimmah” pamoja na utangulizi wa kitabu cha ´Abdul-´Aziyz al-´Askar ”Nubdhah fiy Huquuq Wulaat-il-Amr”. Kadhalika maneno yake yaliyochapishwa katika gazeti “al-Buhuuth al-Islaamiyyah” (50). Humo mna Radd ya wazi kabisa kwa wale wenye kudai ya kwamba yeye (Rahimahu Allaah) haonelei kuzungumza na kuandika kuhusu maudhui hizi.

[2] Anaashiria (Hafidhwahu Allaah) Hadiyth ya ´Ubaadah bin as-Swaamit (Radhiya Allaahu ´anh) ambapo alisema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituita na tukampa kiapo cha usikivu juu ya kusikiza na kutii, katika uchangamfu wetu na yale tunayoyachukia, katika kipindi chepesi na kigumu, pindi mtu anapopendelewa juu yetu na kwamba tusivutane na watawala mpaka pale mtakapoona ukafiri wa wazi ambao tuna dalili kwao kutoka kwa Allaah.” (Fath-ul-Baariy (05/13))

Ahmd amepokea na nyongeza:

“Na ukiona kuwa katika jambo hili uko na haki, usitendee kazi dhana. Sikiliza na tii mpaka ulifikie pasi na kuasi.”

Ibn Hibbaan na Ahmad wamepokea tena na nyongeza:

“… hata kama watachukua mali yako na kukupiga mgongo wako.” (Fath-ul-Baariy (08/13))

[3] Shaykh (Hafidhwahu Allaah) anaashiria Hadiyth ya Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) pale ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuona kwa kiongozi wake kitu anachokichukia basi asubiri. Kwani hakika yule mwenye kutengana na mkusanyiko kiasi cha shibri moja na akafa, basi amekufa kifo cha kipindi kabla ya kuja Uislamu.” (al-Bukhaariy (7054))

Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika baada yangu mtaona mapendeleo na mambo mnayoyakemea.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Unatuamrisha nini?” Akasema: “Watimizeni haki zao na nyinyi mumuombe Allaah haki zenu.” (al-Bukhaariy (7052) na at-Tirmidhiy (2090))

[4] Ni kama mfano wa maandamano yanayoendelea katika baadhi ya miji jirani. Maandamano haya yanatokamana na makafiri na hayatoki kwa waislamu. Hayana lolote kuhusiana na Uislamu. Yanapelekea kumwagika damu, kuzikiuka heshima na kuishambulia Sunnah na Ahl-us-Sunnah. Watu wenye kulingania katika hamasa hizi za siasa hawafikirii matokeo haya?

[5] Huu ndio mfumo wa Salaf inapokuja katika kuwanasihi watawala ili kujitenga mbali na kujionyesha na kuwepo uwezekano mkubwa wa watawala kukubali na kitendo kukubaliwa na Allaah vilevile.

[6] Muslim (55).

[7] Muslim (1715), Maalik (02/756) na Ahmad (02/367).

[8] 04:83

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kuamrisha mema na kukataza maovu kunatakiwa kuwa kwa urafiki. Ndio maana ikasemwa kitendo cha mmoja kuamrisha mema kinatakiwa iwe wema na kukataza maovu isiwe maovu. Ikiwa kuamrisha mema na kukataza maovu ni katika mambo ya wajibu makubwa au yanayopendeza, basi ni lazima manufaa yawe makubwa zaidi kuliko madhara… Yote ambayo Allaah ameamrisha ni mazuri. Allaah amesifia wema na watengenezaji na akasema vibaya maharibifu na wenye kuharibu maeneo mengi. Ikiwa madhara ya kuamrisha au kukataza ni makubwa zaidi kuliko manufaa, basi sio kitu ambacho Allaah ameamrisha hata kama kutaachwa jambo la wajibu au kukafanywa jambo la haramu. Kwani muumini anatakiwa kumcha Allaah kutokana na waja wa Allaah. Yeye kazi yake sio kuwaongoza.” (al-Amr bil-Ma´ruuf wan-Nahiy ´an-il-Munkar, uk. 19)

[9] Muslim (49).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 45-49
  • Imechapishwa: 31/05/2023
  • mkusanyaji: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy