18. Mwenye busara na hisia za watu II


1- Makhlad Abu ´Aaswim amesema:

“Ninapomchukia mtu basi huchukia mpaka sehemu ya mwili wangu ulio karibu na yeye.”

2- Abu Bakr al-Marruudhiy amesema:

“Nilimuuliza Ahmad bin Hanbal kuhusu wachoshaji. Akasema: “Nilimuuliza Bishr al-Haafiy juu yao akasema: “Inasikitisha kuwatazama.” Nilimuuliza Ahmad ni wepi wachoshaji.. Akasema: “Ni Ahl-ul-Bid´ah.”

3- Alichotaja Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) ni njia maalum ya kuwaangalia watu wenye kuchosha. Wakijua kuwa ni mwenye kuipa mgongo Sunnah wanamchukia kwa sababu ya Bid´ah zake. Kuhusu wasiokuwa wasomi na kwa njia maalum, huwachukia na kuwapenda tu wale walio na tabia njema na mbaya.

4- Abu Usaamah amesema:

“Nileteeni mtu aliye na moyo mwepesi, lakini tahadharini na wale wenye kuchosha. Tahadharini na wale wenye kuchosha.”

5- Ibn Siyriyn amesema:

“Nilimsikia bedui akisema kuwa alizimia wakati siku moja alipomwangalia mtu mwenye kuchosha.”

6- Ibraahiym bin Bukayr amesema:

“Pindi Abu Hurayrah alipokuwa anaona kikao kimechosha husema: “Ee Allaah! Tusamehe sisi na yeye na utuafu naye katika hali salama.”

7- Ni wajibu kwa aliye na busara kujiepusha na sifa ambazo watu wanaona kuwa ni zenye kuchosha na badala yake awe na sifa zitazofanya watu wampende.”

8- Miongoni mwa mambo yanayochangia zaidi mtu kupendwa na watu ni kuwahudumikia wao na kuwaondolea maudhi yao. Asiyekuwa na pesa atangamane nao kwa uso wenye bashasha. Hilo linachukua nafasi ya kuwahudumikia.

9- Haaruun bin ´Abdil-Khaaliq al-Maaziniy ameeleza kwamba Ibn-ul-Mubaark aliulizwa kuhusu tabia nzuri. Akasema:

“Ni kuwa na uso wenye bashasha na kuwafanyia watu mema.”

10- Mujaahid amesema:

“Muislamu anapokutana na nduguye akapeana naye mkono na kumuonyesha uso wa bashasha huanguka majani yake kama jinsi linavyoanguka rundo la tende kutoka kwenye mti.” Ndipo mwanaume mmoja akasema: “Ee Abul-Hajjaaj! Hiki ni kitendo chepesi!” Mujaahid akasoma:

هُوَ الَّذِي أَيَّدَكَ بِنَصْرِهِ وَبِالْمُؤْمِنِينَ وَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ ۚ لَوْ أَنفَقْتَ مَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا مَّا أَلَّفْتَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ أَلَّفَ بَيْنَهُمْ

“Yeye ndiye ambaye kakusaidia kwa nusra Yake na kwa waumini na akaunganisha nyoyo zao. Lau ungelitoa vyote vilivyomo ardhini, basi usingeliweza kuunganisha nyoyo zao.”[1]

Haya ni mepesi?”

[1] 08:62-63

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 67-70
  • Imechapishwa: 06/02/2018