Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah inapokuja katika dalili ni kufuata yaliyokuja katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa ndani na kwa nje. Sambamba na hilo kufuata yale waliyokuwemo Maswahabah ambao ni Muhaajiruun na Answaar kwa ujumla na khaswa makhaliyfah waongofu kwa vile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye ambaye kausia kufanya hivo pale aliposema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu.”[1]

Hawatangulizi mbele ya maneno ya Allaah na maneno ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) maneno ya yeyote yule. Kwa ajili hii ndio maana wameitwa “Ahl-ul-Kitaab was-Sunnah”. Baada ya kutendea kazi Qur-aan na Sunnah, wanatendea kazi yale waliyoafikiana kwayo wanazuoni wa Ummah. Huu ndio msingi wa pili wanautegemea baada ya misingi miwili inayotangulia:

1 – Qur-aan.

2 – Sunnah.

Kuhusu yale watu wanayotofautiana kwayo wanayarudisha katika Qur-aan na Sunnah kwa kutendea kazi maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ

“Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi.”[2]

Hawaamini kuwa kuna yeyote aliyekingwa na kukosea asiyekuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hawana ushabiki juu ya maoni ya yeyote mpaka pale yawe ni yenye kuafikiana na Qur-aan na Sunnah. Wanaonelea kuwa Mujtahid mara hupatia na mara nyingine hukosea. Hawamruhusu yeyote kufanya Ijtihaad isipokuwa kwa kutimia sharti zinazojulikana kwa wanazuoni. Hawana kukemeana katika masuala ya Ijtihaad yenye kuzingatiwa. Tofauti zinazotokea katika masuala ya Ijtihaad hayapelekei katika uadui na kuhamana, kama wanavyofanya watu wenye ushabiki na Ahl-ul-Bid´ah. Kinyume chake wanapendana na hawa wanaswali nyuma ya wengine pamoja na tofauti zao katika baadhi ya mambo ya vitaga. Hili ni tofauti na wanavyofanya Ahl-ul-Bid´ah ambapo wanajenga uadui, kutiana upotevuni au kumkufurisha yule anayepingana nao.

[1] Abu Daawuud (4609), at-Tirmidhiy (2676), Ibn Maajah (42) na Ahmad (17184)

[2] 04:59

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Usuwl ´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 39-41
  • Imechapishwa: 13/05/2022