18. Mikono ya Allaah (´Azza wa Jall)

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaonelea kuwa Allaah (Ta´ala) ana mikono miwili. Mikono hiyo imekunjuliwa na ni yenye kutoa. Ni katika sifa zake za kidhati. Ni ya kihakika na ni yenye kulingana Naye. Qur-aan na Sunnah vimethibitisha kuthibiti mikono mwili. Kuhusiana na Qur-aan, Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا إِبْلِيسُ مَا مَنَعَكَ أَن تَسْجُدَ لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَيَّ

“Ee Ibliys! Nini kilichokuzuia usimsujudie Niliyemuumba kwa Mikono Yangu?”[1]

Ama Sunnah Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mkono wa kuume wa Allaah umejaa. Haupungui kwa kutoa asubuhi na jioni. Mnaona vile alivyotoa tangu aumbe mbingu na ardhi pasi na kupungua chochote kilichoko kwenye mkono Wake wa kulia?”[2]

Ahl-us-Sunnah wameafikiana kwamba ni mikono miwili ya kikweli isiyofanana na mikono ya viumbe. Sio sahihi kupindisha maana yake kwamba ni nguvu, neema au kitu kingine kutokana na sababu zifuatazo:

1- Ni kuyaondosha maneno kutoka katika uhakika wake kwenda katika majazi pasi na dalili.

2- Hii ni maana inayokataliwa na lugha katika mazingira haya ambapo mikono imeegemezwa kwa Allah (Ta´ala). Allaah amesema:

لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَيَّ

“… Niliyemuumba kwa Mikono Yangu?”

Si sahihi maana ikawa:

“… Niliyemuumba kwa neema au nguvu zangu?”

3- Ni mikono miwili ndio imeegemezwa kwa Allaah. Haikuthibiti si katika Qur-aan wala Sunnah ya kwamba Allaah (Ta´ala) anaegemezewa neema au nguvu mbili. Vipi basi mtu anaweza kufasiri mikono miwili kwamba ni neema au nguvu mbili?

4- Lau ingelikuwa kweli na maana ya nguvu, basi ingelikuwa ni sahihi kusema kwamba Allaah amemuumba Ibliys kwa mkono Wake. Hili ni jambo lisilowezekana. Na kama ingelikuwa inajuzu, basi Ibliys na yeye angeliweza kutumia kama hoja yake dhidi ya Mola wake alipomwambia:

يَا إِبْلِيسُ مَا مَنَعَكَ أَن تَسْجُدَ لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَيَّ

“Ee Ibliys! Nini kilichokuzuia usimsujudie Niliyemuumba kwa Mikono Yangu?”

5- Njia ambayo Allaah amejiegemezea mkono imetajwa katika mazingira ambayo ni jambo lisilowezekana ikawa na maana ya neema au nguvu. Mkono ndio umetajwa na vivyo hivyo kiganja ndivyo ilivyo inapokuja katika vidole na mshiko. Imethibiti namna ambavyo Atashika na kutikisa kwa mkono Wake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah atazishika mbingu kwa mkono Wake na ardhi kwa mkono Wake mwingine. Halafu azitikise na kusema: “Mimi ndiye Mfalme.”[3]

[1] 38:75

[2] al-Bukhaariy (4684) na Muslim (993).

[3] al-Bukhaariy (4812), Muslim (2787), Ahmad (02/242) na at-Tirmidhiy (3045) aliyesema:

“Hadiyth hii ni nzuri na Swahiyh na inafasiri Aayah isemayo:

وَقَالَتِ الْيَهُودُ يَدُ اللَّـهِ مَغْلُولَةٌ ۚ غُلَّتْ أَيْدِيهِمْ وَلُعِنُوا بِمَا قَالُوا ۘ بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ يُنفِقُ كَيْفَ يَشَاءُ

“Mayahudi wakasema: “Mkono wa Allaah imefumbwa”. Mikono yao ndio iliyofumbwa na wamelaaniwa kwa yale waliyoyasema. Bali mikono Yake imekunjuliwa hutoa atakavyo.” (05:64)

Hadiyth imepokelewa na maimamu. Tunaiamini kama ilivyosimuliwa pasi na tafsiri wala kuifanyia namna. Hivo ndivo walivosema maimamu akiwemo Sufyaan ath-Thawriy, Maalik bin Anas, Ibn ´Uyaynah na Ibn-ul-Mubaarak; inatakiwa kusimuliwa na kuaminiwa bila kuifanyia namna.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 56-57
  • Imechapishwa: 30/04/2020