18. Mfumo wa Ahl-us-Sunnah juu ya Mtume (صلى الله عليه وسلم)

3- Mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya haki ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

Ni jambo linalotambulika kwamba Uislamu hautimii isipokuwa kwa kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Shahaadah ya mtu haihakikishwi isipokuwa kwa kutimia mambo matatu:

1- Imani ndani ya moyo.

2- Kutamka kwa ulimi.

3- Matendo ya viungo.

Kwa ajili hii wanafiki walikuwa wakisema kumwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale anapowaendea:

نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللَّـهِ

“Tunashuhudia kwamba wewe kweli ni Mtume wa Allaah.”

Allaah (Jalla Dhikruh) anasema juu yao:

وَاللَّـهُ يَعْلَمُ إِنَّكَ لَرَسُولُهُ وَاللَّـهُ يَشْهَدُ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَكَاذِبُونَ

“Allaah anajua kwamba hakika wewe ni Mtume Wake na Allaah anashuhudia kwamba hakika wanafiki bila shaka ni waongo.”[1]

Kwa nini? Kwa sababu ushuhuda huu ndani yake kumekosekana nguzo kubwa ambayo ni imani. Wanatamka kwa ndimi zao wasiyoyaamini ndani ya mioyo yao. Mwenye kusema ´nashuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah` lakini hata hivyo moyo wake ni mtupu kutokamana na ushuhuda huu, basi hakuhakikisha kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Mwenye kuyaamini hayo lakini asiyaseme kwa mdomo wake hakuhakikisha kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Mwenye kuyasema hayo lakini asimfuate katika Shari´ah yake hakuhakikisha kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Vipi utakwenda kinyume naye na wewe unaamini kuwa ni Mtume wa Mola wa walimwengu na kwamba Shari´ah ya Allaah ni yale aliyokuja nayo? Vipi unasema kuwa ni mwenye kushuhudia kuwa Muhammad ni Mtume wa Allaah kwa njia ya kihakika? Kujengea juu ya haya tunasema kwamba kila yule mwenye kumuasi Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuhakikisha kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Simaanishi kuwa hakutamka hivo. Ninachomaanisha ni kwamba hakuhakikisha. Amepunguza katika kuhakikisha kwa kiwango cha vile alivyokhalifu.

[1] 63:01

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manhaj Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah fiy-´Aqiydah wal-´Amal, uk. 28-30
  • Imechapishwa: 05/08/2019