18. Masuala matatu ambayo ni lazima kwa kila muislamu kujifunza nayo


Tumefika katika somo lililotangulia katika maneno ya mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah):

Tambua – Allaah Akurehemu – kwamba ni wajibu kwa kila muislamu mwanaume na mwanamke, kujifunza masuala haya matatu na kuyatendea kazi:

La kwanza: Allaah Ametuumba, akaturuzuku na Hakutuacha bure tu bila ya malengo. Bali Amewatumia Mtume; mwenye kumtii, ataingia Peponi, na yule mwenye kumuasi, ataingia Motoni.”

Maneno yake mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah):

“Tambua.”

Ni uzinduzi, maelekezo na mwongozo kwa mwanafunzi ili ayatilie umuhimu mambo haya. Elimu ndio kitu bora ambacho mtu anaweza kukitilia umuhimu na kuuelekeza moyo na viungo vya mwili ili mtu aweze kuyafahamu kwa njia sahihi na baadaye akayatendea kazi. Kwani matendo ndio matunda ya elimu. Maneno yake:

“Allaah akurehemu.”

anamzungumzisha kila yule msomaji na msikilizaji. Ni jumla inayofahahamisha ni namna gani mtunzi wa kitabu anawatakia kheri ndugu zake waislamu na waumini. Anawaombea du´aa mbele ya masuala muhimu ili wayafahamu, wayaelewe na watendee kazi muqtadha yake. Hiyo ni adabu nzuri katika utunzi wa vitabu, mazungumzo, Khutbah na mihadhara kwa aina zake mbalimbali. Wanachuoni wa ki-Salaf wanapita njia hii katika maelekezo yao – wakati wa kutunga vitabu, Khutbah na nasaha imara – mkondo huu ili kumzindua msikilizaji, msomaji na kuwaombea du´aa.

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Twariyqal-Usuwl ilaa idhwaah-ith-Thalaat-il-Usuwl, uk. 42-43
  • Imechapishwa: 25/11/2021