18. Kurusha mawe


86- Minaa ataokota/ataokokta mawe ambayo anataka kuvirusha katika nguzo ya ´Aqabah. Hii ndio nguzo ya mwisho na ndio maeneo yaliyo karibu zaidi na Makkah.

87- Atapofika hapo, aelekee Qiblah na aifanye Makkah iwe upande wake wa kushoto na Minaa iwe upande wake wa kuume.

88- Atairushia vijiwe saba. Vijiwe hivyo ni vikubwa kidogo kuliko changarawe.

89- Kila jiwe anaporusha aseme “Allaahu Akbar”[1].

90- Talbiyah itakatika pale ataporusha jiwe la mwisho[2].

91- Asirushe mawe isipokuwa baada ya jua kuchomoza. Haya yanawahusu hata wale wanawake na wadhaifu ambao wameruhusiwa kuondoka Muzdalifah baada ya nusu ya usiku. Kwani hiki ni kitu kimoja na kurusha mawe ni kitu kingine[3].

92- Inaruhusu kwake kurusha mawe baada ya kupinduka jua mpaka usiku akipatwa na uzito wa kurusha mawe kabla ya jua kupinduka. Hivo ndivyo ilivyothibiti katika Hadiyth.

93- Akimaliza kurusha mawe kitahalalika kwake kila kitu isipokuwa tu wanawake ijapokuwa hakuchinja wala hakunyoa [kichwa chake]. Kwa hiyo avae mavazi yake na ajitie manukato.

94- Kama anataka kuendelea katika Tamattu´ yake iliyotajwa, basi analazimika kutukufu Twawaaf-ul-Ifaadhwah siku ileile. Kama hatowahi kufanya Twawaaf kabla ya jua kuzama, basi atatakiwa kurudi katika hali ya Ihraam kama alivyokuwa kabla ya kurusha mawe. Hivyo atalazimika kuvua nguo zake na kuvaa nguo za Ihraam. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika siku hii mna ruhusa, iwapo mtarusha mawe, basi mnaweza kumaliza Ihraam zenu mkafanya kila mlichokuwa mmeharamishiwa isipokuwa [kuwaingilia] wanawake. Ikiwa hamkuweza kutufu Nyumba hii kabla ya jua kuzama, basi mtarudi tena katika hali zenu za Ihraam kabla hamjarusha nguzo ya kurusha mawe mpaka pale mtapofanya Twawaaf.”[4]

[1] Kuhusu nyongeza isemayo:

اللهم اجعله حجا مبرورا

“Ee Allaah! Ifanye kuwa ni hajj yenye kukubaliwa… “

inayotajwa na baadhi ya watunzi wa vitabu, haikuthibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hilo nimelibainisha katika “adh-Dhwa´iyfah” (1107).

[2] Ameipokea Ibn Khuzaymah katika ”as-Swahiyh” yake. Amesema:

“Hadiyth hii ni Swahiyh. Inafasiri yale mapokezi mengine yaliyopokelewa hali ya kutofasiriwa. Inaweka wazi maneno yake:

“… mpaka ataporusha mawe kwenye nguzo ya ´Aqabah.”

bi maana mpaka atapokamilisha kurusha kwake mawe.” (Fath-ul-Baariy (3/426))

[3] Maoni haya nimeyapambanua katika “asili”, uk. 80. Rejea huko kama unataka kubainikiwa na jambo.l

[4] Ni Hadiyth Swahiyh. Wako maimamu wengi, akiwemo Ibn-ul-Qayyim, ambao wameifanya kuwa na nguvu. Hilo nimelibainisha katika “Swahiyh Abiy Daawuud” (1745). Pindi baadhi ya wanachuoni waheshimiwa walipoiona Hadiyth hii kabla ya kitabu kuchapishwa waliona kuwa ni jambo geni. Kuna ambao walifikia mpaka kuidhoofisha, kama ambavyo na mimi vilevile nilifanya katika baadhi ya vitabu vyangu. Nilijengea hilo juu ya cheni ya wapokezi iliyoko kwa Abu Daawuud pamoja na kwamba Ibn-ul-Qayyim aliipa nguvu katika “at-Tahdhiyb” na Haafidhw katika “Talkhiys-ul-Habiyr” kwa kuacha kuiwekea taaliki. Nimepata njia yake nyingine inayomfanya mtu kuwa na yakini na kuiondosha udhaifu wake na badala yake kuinyanyua katika ngazi ya usahihi. Kwa vile iko katika kitabu ambacho hakikuenea kwa wengi – nacho ni “Sharh Ma´aaniy al-Aathaar” ya Imaam at-Twahaawiy – ilifichikana kwao kama ilivyofichikana kwangu pia hapo kabla. Kwa ajili hiyo ndio maana wakakimbilia kuiona kuwa ni geni na kuidhoofisha. Kadhalika walipata ushujaa wa kufanya hivo kwa sababu waliwapata baadhi ya wanachuoni wakisema:

“Simjui mwanachuoni yeyote wa Fiqh aliyeitendea kazi.”

Hata hivyo haya ni makanusho, sio elimu. Ni jambo lenye kutambulika kwa wanachuoni ya kwamba mtu kutokukijua kitu, hilo halipelekei kwamba jambo hilo halipo. Hadiyth ikithibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ikawa ni dalili ya wazi kama ilivyo hii, basi itawajibika kuitendea kazi. Mambo hayahusiani na kujua msimamo wa wanachuoni katika hilo. Imaam ash-Shaafi´iy amesema:

“Mapokezi yanakubaliwa katika ule wakati ambao yamethibiti japokuwa maimamu hawatoyatendea kazi. Hadiyth kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) inathibiti kivyake. Ikiwepo, basi hakuna chengine kinachostahiki kutendewa kazi.”

Hadiyth ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni tukufu zaidi kuliko kuitumia kama ushahidi kwa sababu ya matendo ya wanachuoni wa Fiqh. Hadiyth ni msingi uliosimama barabara unaohukumu na usiohukumiwa. Pamoja na hivyo wapo wanachuoni wengi waliofanyia kazi. Miongoni mwao ni Taabiy´ mtukufu ´Urwah bin az-Zubayr. Je, baada ya haya yote kuna yeyote ana udhuru wa kuacha kuitendea kazi?

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَذِكْرَىٰ لِمَن كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ

“Hakika kuna katika hayo mazingatio kwa yule mwenye akili au akatega sikio naye mwenyewe awe hadhiri.” (50:37)

Vilevile tambua kwamba kurusha mawe kwa mahujaji ni sawa na swalah ya ´Iyd za wengine. Kwa ajili hiyo Ahmad amependekeza swalah ya ´Iyd hii iswaliwe wakati wa kunapochinjwa huko Minaa. Kwa ajili hii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoa Khutbah siku ya Nahr baada ya kurusha mawe. Kama ambavyo alikuwa akikhutubu al-Madiynah baada ya swalah ya ´Iyd. Kule baadhi yao kupendekeza kuswali swalah ya ´Iyd Minaa kwa kuchukulia matamshi ya kijumla na vipimo kama dalili, ni kosa na ni kuwa na ughafilikaji juu ya Sunnah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na makhaliyfah wake hawakupatapo kamwe kuswali swalah ya ´Iyd Minaa. Hayo yamebainishwa katika “al-Fataawaa” (26/180) ya Ibn Taymiyyah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manaasik-ul-Hajj wal-´Umrah, uk. 30-32
  • Imechapishwa: 19/07/2018