1- Ni jambo limesuniwa kwa mfungaji kutumia Siwaak. Imependekezwa kwake kufanya hivo wakati wa kila swalah na wakati wa kila wudhuu´. Imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyeeeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Lau isingelikuwa kuwatilia uzito Ummah wangu basi ningeliwaamrisha Siwaak pamoja na kila swalah.”

Katika Hadiyth ya Zuhayr bin Harb iliyopokelewa na Muslim imekuja:

“Lau isingelikuwa kuwatilia uzito Ummah wangu basi ningeliwaamrisha Siwaak wakati wa kila swalah.”

Ibn Khuzaymah amesema katika “as-Swahiyh” yake:

“Hakupambanua ambaye hakufunga na aliyefunga.”

at-Tirmidhiy, Abu Daawuud na Ahmad wamepokea kupitia kwa ´Ammaar bin Rabiy´ah aliyesema:

“Nilimwona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mara nisizoweza kuzihesabu akipiga Siwaak ilihali amefunga.”

Katika cheni ya wapokezi wake yupo ´Aaswim bin ´Ubaydillaah bin ´Aaswim bin ´Umar bin al-Khattwaab. al-Bukhaariy, Ibn Ma´iyn na wengineo wamemdhoofisha. Lakini hata hivo at-Tirmidhiy amesema:

“Wanachuoni ni wenye kulitendea kazi jambo hili. Hawaoni ubaya wowote kwa mfungaji kutumia Siwaak. Ni mamoja mwanzoni mwa mchana na mwishoni mwake.”

Maoni sahihi ni kwamba imesuniwa kupiga Siwaak mwanzoni na mwishoni mwa mchana. Lakini kwa sharti Siwaak hiyo isiwe yenye kuumiza wala kutoa chembechembe zikaingia kooni mwake. Kadhalika mswaki usiwe mkali kwa njia ya kwamba ukaondosha fizi na wala kusiwe kitu kingine miongoni mwa vile vitu vinavyowekwa na watu [kwenye mswaki huo] ukaufanya ukawa na utamtam.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswaru fiy Ahkaam-is-Swiyaam, uk. 32
  • Imechapishwa: 23/05/2019