18. Hii ndio sababu ya waliopinda katika Qadar

Kuamini Qadar ni katika misingi ya imani. Imethibiti katika Hadiyth ya Jibriyl ambapo alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amweleze kuhusu imani. Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Imani ni kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, siku ya Mwisho na kuamini Qadar kheri na shari yake.”[1]

Amesema (Ta´ala):

إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ

“Hakika sisi Tumekiumba kila kitu kwa makadirio.”[2]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Pupia yale yenye kukunufaisha na utake msaada kwa Allaah. Ikiwa utafikwa na kitu basi usisemi “lau ningefanya kadhaa ingelikuwa kadhaa”. Badala yake unatakiwa useme: “Amekadiria Allaah na akitakacho huwa.” Kwani hakika ya “lau…” inafungua matendo ya shaytwaan.”[3]

Hadiyth na maandiko juu ya haya ni mengi. Msingi huu ni wenye kujulikana. Haki ndani yake inajulikana. ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu yake iko wazi. ´Aqiydah yao imejengwa juu ya yale yaliyokuja katika Qur-aan na Sunnah. Kuhusu wale waliopinda na msingi huu hilo limetokamana na kufuata nafsi zao na matamanio yao na wakati huohuo wakaipa mgongo Qur-aan na Sunnah. Hali inakuwa namna hii kwa kila ambaye anajaribu kutoka nje ya dalili za Qur-aan na Sunnah. Natija yake hutumbukia katika upotevu. Amesema (Ta´ala):

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ

“Na kwamba hii njia Yangu iliyonyooka – hivyo basi, ifuateni – na wala msifuate vijia vya vichochoro vikakufarikisheni na njia Yake.”[4]

[1] al-Bukhaariy (4499), Muslim (10), an-Nasaa´iy (4991), Ibn Maajah (64) na Ahmad (02/426).

[2] 54:49

[3] Muslim (2664), Ibn Maajah (79) na Ahmad (02/370).

[4] 06:153

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mujmal ´Aqiydat-is-Salaf as-Swaalih, uk. 16
  • Imechapishwa: 24/05/2022