18. Hakuna magomvi na majadiliano ya kidini

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Asigombane wala kujadiliana na yeyote. Asijifunze mijadala. Mizozo juu ya Qadar, Kuonekana, Qur-aan na mambo mengine ya ´Aqiydah yamechukizwa na yamekatazwa. Mwenye kufanya hivo sio katika Ahl-us-Sunnah – hata kama atazungumza kwa ´Aqiydah – mpaka pale atakapoacha mijadala na kujisalimisha na kuamini mapokezi.”

Anashauri mtu aache mijadala:

“Mizozo juu ya Qadar, Kuonekana, Qur-aan na mambo mengine ya ´Aqiydah yamechukizwa na yamekatazwa.”

Kuna Hadiyth ambazo zinakataza mijadala na malumbano. Kuna wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoka akasikia jinsi watu wanavyozozana juu ya Qadar. Akakasirika mpaka uso wake ukageuka mwekundu kama mbegu za mkomamanga na kusema:

“Mnataka kusababisha migongano katika Kitabu cha Allaah?”[1]

Aliwakemea kwa ukali. Ni dalili yenye kuonesha kuwa mijadala juu ya Qadar imekatazwa na mambo mengine ya ´Aqiydah.

Imaam Ahmad amesema:

“Mwenye kufanya hivo sio katika Ahl-us-Sunnah – hata kama atazungumza kwa ´Aqiydah… “

Imaam Ahmad alikuwa ni mkali katika mambo ya mijadala. Alikuwa anaona kuwa mwenye kuonelea kuwa mijadala ndio njia pekee ya kushinda kwa Sunnah amekosea. Hata hivyo maneno yake yasifahamiki kwa njia isiyofungamanishwa. Allaah ameturuhusu kujadili kwa njia nzuri. Ikiwa mijadala itatimiza masharti yake na lengo la mjadili ni haki iweze kushinda na sio kudanganya, kuwa na kiburi na kufanya ukaidi, wewe jadiliana naye kwa njia ilio nzuri. Ama ikiwa amemili kwenye ghadhabu, magomvi na kutaka matapo, usijadiliane naye.

Kuna baadhi ya Khawaarij waliokuja kwa Shaykh Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) ili kujadiliana naye; hajadiliani nao. Kulikuja baadhi ya Raafidhwah kujadiliana naye; hajadiliani nao.

Imaam Ahmad amesema:

“… mpaka pale atakapoacha mijadala na kujisalimisha na kuamini mapokezi.”

Hili ndio la wajibu kwako. Unachotakiwa ni kuamini mapokezi, kuwafikishia nayo watu, kuwawekea nayo wazi na kuwabainishia nayo ikiwa kuna uzito wa kuweza kuyafahamu. Ikiwa kuna mtu ambaye anataka kujadiliana na wewe kwa njia ilio nzuri na ili apate faida, mbainishie. Ikiwa yuko na utata muondoshee nao kwa upole, hekima na uzuri. Na ikiwa lengo lake anachotaka tu ni malumbano, usijadiliana naye. Mtu kama huyo anachotaka sio haki na hutofikia natija yoyote kwake.

[1] Ibn Maajah (85).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 382-383
  • Imechapishwa: 06/08/2017