18. ´Aqiydah ambayo siku zote imejengeka juu ya dalili

Tumekwishasoma kuhusu Qadar na ngazi zake kwa dalili zake na I´tiqaad mbalimbali za watu juu yake. Vivyo hivyo kuhusiana na kuonekana na I´tiqaad mbalimbali za watu juu yake. Mmejua kwamba wako ambao wako kati na kati na wengine wamezembea na kwamba Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ndio wako kati na kati. Kutokana na dalili za Qur-aan na Sunanh wanathibitisha kuonekana kwa Allaah Aakhirah na wanakanusha kuonekana Kwake hapa duniani kwa sababu jambo hilo halina dalili.

Ahl-ul-Bid´ah wapotofu wamegawanyika mafungu mawili yenye kujigonga. Wako ambao wanapinga uonekanaji duniani na Aakhirah ilihali wengine wanathibitisha duniani na Aakhirah. Wote wawili hawana dalili. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ambao wanathibitisha kuwa waumini watamuona Mola wao Aakhirah ndio wenye dalili. Watamuona kwenye uwanja wa hesabu siku ya Qiyaamah na ndani ya Pepo. Hii ndio neema kubwa watayoburudika nayo watu wa Peponi.

Moja katika dalili za Ahl-us-Sunnah kuhusu kuonekana ni maneno Yake (Ta´ala):

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ

“Nyuso siku hiyo zitang´ara – zikimtazama Mola wake.”[1]

Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika nyinyi mtamuona Mola wenu kama mnavyouona mwezi huu mwandamo – hamtosongamana katika kumuona. Kama mtaweza kuswali kabla ya jua kuchomoza na kabla ya jua kuzama basi fanyeni hivo.”[2]

I´tiqaad za mapote mawili yote zinaraddiwa kwa ´Aqiydah sahihi ya Al-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na dalili zenye kutia nguvu.

[1] 75:22-23

[2] al-Bukhaariy (554) na Muslim (633).

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 70
  • Imechapishwa: 08/10/2019