18. Analipa swalah ambaye aliiacha kusudi?

Swali 18: Je, swalah inalipwa kwa ambaye ameiacha kwa makusudi pindi Allaah anapomuwafikisha kutubu ni mamoja ameacha kipindi kimoja au vingi?

Jibu: Haimlazimu kulipa kama aliacha kwa makusudi kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Kwa sababu kuiacha kwa makusudi kunamtoa katika duara ya Uislamu na kunamfanya ni katika makafiri. Kafiri halipi yale aliyoacha katika kipindi cha ukafiri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Baina ya mtu na shirki na ukafiri na shirki ni kuacha swalah.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

Vilevile (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ahadi iliopo kati yetu sisi na wao ni swalah. Hivyo basi, yule atakayeiacha amekufuru.”

Ameipokea Imaam Ahmad na watunzi wa nne wa Sunan kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kupitia kwa Buraydah bin al-Huswayb (Radhiya Allaahu ´anh).

Isitoshe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwaamrisha makafiri walipe yale waliyoacha pindi waliposilimu. Vivyo hivyo Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) hawakuwaamrisha walipe wale walioritadi wakati waliporudi katika Uislamu. Hata hivo hapana vibaya kwa ambaye atalipa baada ya kuacha ilihali hakupinga ulazima wake. Hivo ni kwa ajili ya tahadhari zaidi na kutoka nje ya tofauti ya wale wenye kuona kuwa hakufuru muda wa kuwa hakupinga ulazima wake, kwani hivo ndivo wanavoona wanazuoni wengi.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 21
  • Imechapishwa: 16/08/2022