18. Allaah amewaumba viumbe na matendo yao

Kuna ngazi nyingine, nayo ni utashi. Hakuna kitu kinachokuwa ulimwenguni isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amekitaka kiwe. Kinakuwa kwa uwezo wa Allaah. Hakuna kitu kinachotoka nje ya utashi Wake, hakuna kitu kinachotoka nje ya uwezo Wake.

Katika hayo kunaingia matendo ya waja. Allaah ameumba matendo ya waja. Pamoja na kuwa yameumbwa na Allaah lakini amewapa wale viumbe wenye jukumu akili, usikizi, uoni, uwezo na utashi. Kwa ajili hiyo watahesabiwa kwa ajili ya mambo haya. Kila mmoja anafanya matendo mema kwa khiyari yake. Kila mmoja anafanya madhambi kwa khiyari yake. Hakuna kugongana kati ya utashi wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na matendo ya waja. Hakuna mgongano kati ya Allaah kuumba matendo na kuyataka. Hakuna mgongano baina ya waja wanafanya matendo yao na kisha wakahesabiwa kwayo.

Waja ni waumini, makafiri, wema, watenda dhambi, waswalaji, wafungaji, waaminifu na waongo. Hivi ndivyo zilivyo sifa zao, matendo yao na madhambi yao. Hakuna wenye kusifiwa nazo isipokuwa wao. Allaah (Subhanaahu wa Ta´ala) hasifiki kwa sifa hizi hata kama Yeye ndiye kayataka na kuyakadiria yapitike. Kutokana na ukubwa na utukufu Wake hakupitiki katika ulimwengu huu isipokuwa kwa utashi Wake. Hakuna kiumbe isipokuwa Allaah (Subhanaahu wa Ta´ala) ndiye Muumbaji wake.

Waja ni watendaji. Allaah amewaumba wao na matendo yao. Ni wenye majukumu juu ya matendo yao. Ni wenye kuamrishwa, ni wenye kukatazwa na wao ndio wataofanyiwa hesabu juu ya matendo yao.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qurrat-ul-´Aynayn bi Tawdhwiyh Ma´aaniy ´Aqiydat-ir-Raaziyayn, uk. 29-30
  • Imechapishwa: 15/10/2016