Hakika wajibu na faradhi ilio kubwa kwa ambaye ´ibaadah ni yenye kumuwajibikia ni yeye kumuabudu Mola Wake (Subhaanah), Mola ambaye ndiye muumba wa mbingu na ardhi na ´Arshi kubwa aliyesema katika Kitabu Chake kitukufu:

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ يُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ يَطْلُبُهُ حَثِيثًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ وَالنُّجُومَ مُسَخَّرَاتٍ بِأَمْرِهِ ۗ أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗ تَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Hakika Mola wenu ni Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ´Arshi. Anafunika usiku kwa mchana, unaufuatia upesiupesi na jua na mwezi na nyota vyote vimetiishwa kwa amri Yake. Tanabahi! Ni Vyake pekee uumbaji na amri. Amebarikika Allaah, Mola wa walimwengu.” (07:54)

Vilevile ameeleza (Subhaanah) sehemu nyingine katika Kitabu Chake ya kwamba amewaumba majini na wanaadamu ili wamuabudu. Amesema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.” (51:56)

´Ibaadah hii ambayo Allaah kawaumba majini na wanaadamu kwa ajili yake ni kumpwekesha Yeye katika aina zote za ´ibaadah kama swalah, swawm, zakaah, hajj, rukuu, sujuud, kutufu, kuchinja, kuweka nadhiri, kuwa na khofu, kutaraji, kutaka uokozi, kutaka msaada, kutaka kinga na aina nyenginezo za du´aa. Katika hayo kunaingia vilevile kumtii (Subhaanah) katika yale yote aliyoamrisha na kuacha makatazo Yake kutokamana na vile Qur-aan na Sunnah vilivyofahamisha. Allaah (Subhaanah) amewaamrisha majini na watu wote ´ibaadah hii waliyoumbwa kwayo na akawatuma Mitume wote na akateremsha Vitabu kwa ajili ya kubainisha ´ibaadah hii, kuipambanua, kulingania kwayo na kuamrisha kumtakasia ´ibaadah Allaah peke yake. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu ambaye amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kucha.” (02:21-22)

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ

“Mola wako ameamrisha, kwamba asiabudiwe yeyote isipokuwa Yeye pekee.” (17:23)

Maana ya “amehukumu” katika Aayah hii ni ameamrisha na ameusia. Amesema (Ta´ala):

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamuabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia yeye dini, wenye kupondoka kwenye haki na kuiacha batili, na wasimamishe swalah na watoe  zakaah – na hiyo ndio dini iliyosimama imara.” (98:05)

Aayah zilizo na maana kama hii katika Qur-aan ni nyingi. Amesema (´Azza wa Jall):

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ

“Yale alokupeni Mtume, basi yachukueni, na yale alokukatazeni, yaacheni. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni mkali wa kuadhibu.” (59:07)

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wale wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa kweli mnamwamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni njia bora na matokeo mazuri zaidi.” (04:59)

مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ

“Atakayemtii Mtume, basi amemtii Allaah.” (04:80)

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“Hakika tulituma katika kila ummah Mtume [awaamrishe watu wake] kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na twaaghuut [miungu ya uongo].”” (16:36)

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana mungu wa haki isipokuwa Mimi – basi niabuduni!”” (21:25)

الر ۚ كِتَابٌ أُحْكِمَتْ آيَاتُهُ ثُمَّ فُصِّلَتْ مِن لَّدُنْ حَكِيمٍ خَبِيرٍ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا اللَّـهَ ۚ إِنَّنِي لَكُم مِّنْهُ نَذِيرٌ وَبَشِيرٌ

“Alif Laam Miym. Hichi ni Kitabu ambacho Aayah Zake zimetimizwa barabara kisha zikapambanuliwa vizuri kutoka kwa Mwenye hikmah, Mjuzi wa yote; ili msiabudu yeyote isipokuwa Allaah. Hakika mimi ni muonyaji kwenu na mbashiriaji.” (11:01-02)

Hizi ni Aayah ambazo ziko wazi kabisa. Kuna Aayah nyenginezo katika Qur-aan zilizo na maana kama hiyo ambazo zote zinafahamisha juu ya uwajibu wa kumtakasia ´ibaadah Allaah peke yake na kwamba huo ndio msingi wa dini na mila. Vilevile zinafahamisha kuwa hiyo ndio hekima ya kuumbwa majini na watu, kutumwa Mitume na kuteremshwa Vitabu.

Kwa hiyo ni wajibu kwa wale wote ambao ´ibaadah ni yenye kuwawajibikia kulitilia umuhimu jambo hili na kulielewa na kutahadhari na yale waliyotumbukia wengi wenye kujinasibisha na Uislamu katika kupetuka mipaka kwa Mitume, waja wema, kujenga juu ya makaburi yao, kufanya makaburi yao ni mahali pa kuswalia, kuyajengea makuba, kuwaomba, kuwataka uokozi, kuwategemea, kuwaomba watatue haja na matatizo, kuwaponya wagonjwa, wawanusuru dhidi ya maadui na aina nyenginezo katika shirki kubwa. Imesihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yenye kuafikiana na yale yenye kufahamishwa na Qur-aan. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea ya kwamba Mu´aadh (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia:

“Je, unajua Allaah ana haki ipi juu ya waja na waja wana haki ipi kwa Allaah?” Mu´aadh akasema: “Allaah na Mtume Wake ndio wanajua zaidi.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Haki ya Allaah juu ya waja wamuabudu na wala wasimshirikishe Yeye na chochote. Haki ya waja kwa Allaah asimuabudu yule asiyemshirikisha Yeye na chochote.”[1]

Kumepokelewa katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy ya kwamba Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atayekufa hali ya kuwa anamuomba mwenza na Allaah, ataingia Motoni.”[2]

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atayekutana na Allaah hali ya kuwa hamshirikishi Yeye na chochote ataingia Peponi, na atayekutana na Allaah hali ya kuwa anamshirikisha Yeye na chochote ataingia Motoni.”[3]

Kuna Hadiyth nyingi zenye maana kama hii. Haya ndio masuala muhimu na makubwa zaidi.

[1] al-Bukhaariy (5912), Muslim (30), at-Tirmidhiy (2643), Ibn Maajah (4296) na Ahmad (05/238).

[2] al-Bukhaariy (4227), Muslim (92) na Ahmad (01/374).

[3] al-Bukhaariy (129), Muslim (32) na Ahmad (03/157).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah as-Swahiyhah wa maa yudhwaadduhaa, uk. 15
  • Imechapishwa: 31/05/2023