17. Uso wa Allaah (Ta´ala)


Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaamini kuwa Allaah ana uso wa kihakika unaolingana na utukufu na ukarimu Wake. Qur-aan na Sunnah umeyathibitisha hayo. Ama kuhusu dalili za Qur-aan, Allaah (Ta´ala) anasema:

وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ

Na utabakia Uso wa Mola wako wenye Utukufu na Ukarimu.”[1]

Kuhusu dalili za Sunnah, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika du´aa iliyopokelewa:

وَأَسْأَلُكَ لَذَّةَ النَّظَرِ إِلَى وَجْهِكَ وَالشَّوْقَ إِلَى لِقَائِكَ

“Na ninakuomba ladha na kuutazama uso Wako na shauku ya kukutana Nawe.”[2]

Uso wa Allaah (Ta´ala) ni katika sifa Zake za kidhati. Ni ya kihakika kwa njia inayolingana Naye.

Haijuzu kupotosha maana yake na kufasiri kuwa ni thawabu kwa sababu zifuatazo:

Ya kwanza: Ni jambo linaenda kinyume na udhahiri wa andiko. Jambo lenye kwenda kinyume na udhahiri wa andiko linahitajia dalili, na hakuna dalili ya hilo.

Ya pili: Uso huu umeegemezwa kwa Allaah (Ta´ala) na kile chenye kuegemezwa kwa Allaah ima kiwe ni kitu kinachoweza kuwepo kivyake au kisiweze kufanya hivo.

Ikiwa kinaweza kuwepo kivyake, basi kimeumbwa na sio katika sifa za Allaah. Mfano wa hilo ni kama nyumba ya Allaah na ngamia wa Allaah. Kimeegemezwa ima kwa sababu ya kukitukuza au kwa sababu ya kukiegemeza kitu kwa mmiliki au muumbaji wake.

Ikiwa kitu hakiwezi kuwepo kivyake, basi ni katika sifa za Allaah (Ta´ala) na hakikuumbwa. Mfano wa hilo ni kama elimu ya Allaah, uwezo wa Allaah, utukufu wa Allaah, maneno ya Allaah, mkono wa Allaah, macho ya Allaah na kadhalika. Haina shaka kuwa Uso ni miongoni mwa sampuli hizi. Unaponasibishwa na Allaah, unanasibishwa kama kuinasibisha sifa kwa yule msifiwa.

Ya tatu: Thawabu ni kitu kimeumbwa na chenye kutengana na Allaah (Ta´ala). Uso ni sifa miongoni mwa sifa za Allaah na haukuumbwa na wala haukutengana Naye. Vipi basi mtu anaweza kufasiri uso kwamba ni thawabu?

Ya nne: Uso huo umesifiwa kwa utukufu na ukarimu na kwamba una nuru ambayo mtu anajilinda nayo na kwamba unaunguza kila kile Anachokiona lau ataufunua[3]. Sifa zote hizi zinapingana na kufasiri kwamba ni thawabu.

[1] 55:27

[2] an-Nasaa’iy (1305) na ni Swahiyh kwa mujibu wa Ibn Hibbaan (509 – al-Mawaarid) na al-Albaaniy katika ”as-Sunnah” (424).

[3] Tazama Muslim (178).