Imaam al-Barbahaariy (Rahimahu Allaah) amesema:

8- Zingatia – Allaah akurehemu – kila ambaye utasikia maneno yake miongoni mwa watu wa zama zako usifanye haraka na wala usijiingize katika chochote katika hayo mpaka kwanza uulize na uchunguze: Je, Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) waliyazungumza au kuyafanya? Ukipata upokezi kutoka kwao kuhusu hayo, basi shikamana nayo. Usiyavuke na ukachagua kitu kingine ukaja kutumbukia Motoni.

MAELEZO

Usifanye haraka kwa yale utayosikia kutoka kwa watu na khaswa zama za mwisho. Wazungumzaji, wenye kujibu maswali na wenye kujifanya ni wanachuoni wamekuwa wengi. Khaswa hii leo ambapo vyombo vya mawasiliano vimekuwa vingi. Leo imekuwa kila mmoja anazungumza kwa jina la elimu na dini. Hali imefikia kiasi cha kwamba hata wapotevu, mapote potevu na yaliyopinda yamekuwa yakizungumza kwa jina la dini kupitia TV. Kuna khatari kubwa.

Ni lazima kwa muislamu na khaswa mwanafunzi ahakikishe kwanza na usiwe na haraka kwa kila utachokisikia. Ni juu yako kuhakikisha kwanza; ni nani kayazungumza? Fikira hizi zimetoka wapi? Yako wapi mashiko na dalili zake kutoka katika Qur-aan na Sunnah? Aliyosema hayo amesoma kwa nani? Ni lazima kuhakikisha mambo haya na khaswa hii leo.

Usidanganyike na kila mzungumzaji hata kama atakuwa ni mwenye ufaswaha na mzungumzaji vizuri mpaka kwanza uhakikishe ni uelewa na elimi ipi alonayo. Huenda mtu akawa na maneno machache lakini akawa ni msomi. Upande mwingine huenda mtu akawa na maneno mengi lakini hata hivyo akawa ni mjinga na hana elimu yoyote.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Sharh-is-Sunnah, uk. 41
  • Imechapishwa: 03/12/2017